Mara nyingi umekuwa ukijiuliza ufanyeje ubadili maisha yako? Je umekuwa ukitamani kuboresha maisha yako kutoka kiwango cha chini kwenda katika kiwango bora zaidi? Kama jibu ni ndiyo basi una mawazo wazuri sana.
Unatakiwa kuchukua hatua kadhaa ili basi uweze kuboresha maisha yako kutoka kiwango kimoja kwenda kingine. Katika makala hii nitakujuza tabia kumi ambazo kama utajitahidi kuwa nazo hakika utayabadili maisha yako na kuyafanya kuwa bora zaidi.
1. Epuka marafiki au watu wasiofaa
Wahenga walisema “ndege wanaofanana huruka pamoja”. Je kwanini ukae na watu wavivu au wazembe kama wewe huna tabia hizo au zingine zinazofanana na hizo? Jijengee tabia ya kuwaepuka marafiki au watu wasiofaa katika maisha yako kwani hawatakusaidia kufikia malengo yako bali watakudidimiza.
Tafuta watu ambao watakutia moyo na kukupa hamasa ya kutimiza malengo yako. Hata kama ni watu mnaopendana kiasi gani, kama hawana tabia zinazofaa basi ni bora uwaepuke.
Soma pia: Aina 8 za Watu Ambazo ni Sumu za Kuepuka Maishani Mwako.
2. Jifunze kuridhika
Je umewawahi kufikiri labda ukiwa na trilioni mia moja kwenye akaunti yako ndipo utakaporidhika? Kama jibu ni ndiyo, basi unakosea. Usipokuwa na uwezo wa kuridhika na ulicho nacho, hutaweza kuwa na utulivu katika fikra zako hata kama utapata vitu vingi kiasi gani.
Nikukumbushe kuwa simaanishi uridhike na hali mbaya uliyonayo kwa kutojishughulisha kuiboresha, bali jitahidi kuepuka tamaa zisizo na masingi. Jifunze kuwa maisha yana hatua mbalimbali ambazo nyingine ni duni na nyingine ni bora.
Ukijizoeza kuwa na tabia ya kuridhika utayabadili na kuyaboresha maisha yako hatua kwa hatua.
3. Pata muda wa kutosha wa kupumzika
Kufanikiwa katika maisha au kufikia malengo yako si kutopumzika. Umewahi kufikiri usipolala au kupumzika kwa namna moja au nyingine ndipo utakapo badili maisha yako? Tafadhali usiwaze hivi tena, kwani ili uwe mtu mwenye ufanisi unahitaji muda wa kutosha wa kupumzika ili kuufanya mwili wako kuwa wenye afya njema.
Epuka tabia za kutumia simu na mitandao ya kijamii wakati wa kumpumzika hasa wakati wa kulala. Wengi hupenda kulala saa nane usiku kutokana na matumzi ya simu na mitandao. Jambo hili limewafanya wengi kuamka wachovu hivyo kushindwa kufanya kazi za siku sawasawa.
Soma pia: Faida 10 za Kupumzika.
4. Tekeleza mambo hata kama utakwama
Watu waliofanikiwa duniani ni wale waliopata mawazo na kuyafanyia kazi bila kuogopa kuwa watakwama au la. Epuka tabia ya woga na kulalamika. Jifunze kufanyia kazi mawazo uliyonayo ili uweze kuona matokeo yake katika maisha.
Kama una wazo la biashara au ujasiriamali mwingine anza kulitekeleza leo. Kama una woga sana anza taratibu; unaweza ukaanza kwa kuuza hataa vitu 20 – 50 kama unaogopa kuwa na vitu vingi mwanzoni. Usiogope kuhusu mtaji; anza na mtaji ulionao hata kama ni elfu kumi kwani utaendelea kukua taratibu.
Soma pia: Jinsi ya Kuanza Biashara na Mtaji Mdogo.
5. Tunza muda
Mambo yote tuyafanyayo hufungwa katika muda; mambo tuliyonayo ni mengi sana hivyo unahitajika kutunza muda vyema. Jifunze kujiwekea ratiba na kuifuata kila siku. Epuka mambo yasiyokuwa ya lazima kwenye muda wako.
Badala ya kutumia saa 6 kuangalia filamu, kucheza gemu au kutumia mitandao ya kijamii tumia muda huo kufanya vitu vingine vyenye tija zaidi. Unaweza kufanya shughuli nyingine mbadala kama vile ubunifu, kusoma vitabu, kujifunza maarifa mapya usiyokuwa nayo, kilimo cha bustani n.k.
Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda.
6. Jikite kwenye malengo yako
Je una malengo binafsi? Je unafanya bidii kuyafikia? Je umeshayatimiza? Kama huna malengo na hujaanza kuyafanyia kazi, basi unatakiwa kuchukua hatua mapema. Malengo yatakuongoza kujua unaelekea wapi na unataka kuwa nani katika maisha maisha yako.
Kama wewe unataka kuwa na kiwanda cha kutengeneza nguo ni lazima ujue ni hatua zipi stahiki za kuchukua ili kukamilisha lengo lako.
Mambo yatakayokuwezesha kutimiza malengo yako
- Jipatie maarifa stahiki.
- Jifunze kutunza fedha.
- Tunza muda.
- Jenga uthubutu.
Soma pia: Faida 10 za Kuwa na Malengo Maishani.
7. Jifunze kusema hapana
Hapana ni jibu rahisi pia dogo sana lakini lina nguvu kubwa. Usikubali kuwa mtu anayepokea na kukubaliana na kila kitu. Twende sokoni, unaenda; twende disko, unaenda; kunywa pombe, unakunywa; nakupenda, unakubali; twende tukatembee unaenda.
Jifunze kusema hapana hata kama hutamfurahisha unayempa jibu hilo. Tabia hii litakuepusha na mipango isiyo sahihi au ya lazima katika maisha yako. Jitahidi kujenga tabia ya kukubali na kufuata yale yanayolenga kukuwezesha kuyafikia malengo yako.
Soma pia: Faida 5 za Kusema “Hapana”.
8. Bainisha mambo yaliyo na kipaumbele kwako
Kuna mambo mengi ya muhimu kwako lakini baadhi ni muhimu zaidi. Hakuna haja ya kutumia kila pesa unayoipata kwa ajili ya vitu kama vile simu, nguo, viatu, au vyakula vya bei kubwa wakati huna uwekezaji wowote wa uhakika unaokuza kipato chako.
Hakikisha unajijengea tabia ya kubainisha mambo yaliyo na kipaumbele kwako na kuyafanyia kazi. Kila siku itokayo kwa Mungu hakikisha unafanya kitu katika kusogelea au kutimiza ndoto zako.
9. Jifunzae kutunza fedha
Kutafuta pesa ni jambo moja na kuzitumia vyema ni jambo lingine. Wapo watu wanaopata pesa nyingi sana lakini kwa kutokuwa na uelewa juu ya utunzaji wa pesa haziwasaidii. Kama nilivosema kwenye hoja iliyopita, yakupasa kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.
Upatapo pesa hakikisha unaweka akiba kwa ajili ya wakati ujao. Ni vyema pia kuwaza juu ya nini na niwapi uwekeze pesa zako badala ni nini huna au ni wapi utumie pesa zako. Ukiwa na tabia ya kutunza pesa utaboresha maisha yako kwani hata wakati huna kipato utakuwa na akiba ya kutosha.
Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema.
10. Ongeza maarifa kila wakati.
Watu wengi ni wavivu kusoma, hasa mambo ambayo si ya kustarehesha. Huwezi kubadili maisha yako kama hutakuwa na tabia ya kuongeza maarifa yako kila wakati. Jitahidi kusoma vitabu, sikiliza na tazama video zenye kukuza maarifa, pia soma tovuti mbalimbali zitakazopanua maarifa yako Mf. Fahamuhili.com.
Tafuta tovuti au vitabu vinavyoendana na malengo na maono yako; hivi vitakupa hamasa, mwanga na mwongozo wa jinsi ya kufikia malengo yako. Usisahau pia kusoma vitabu na habari mbalimbali zihusuzo watu waliofanikiwa kama vile Bill Gates, Warren Buffet, Mark Zuckerberg, Reginald Mengi na wengine wengi.
Soma pia: Tabia 10 Unazotakiwa Kijifunza Kutoka kwa Watu Waliofanikiwa.
Hitimisho
Kubadili maisha yako ni maamuzi yako wewe mwenyewe. Ukitaka uwe na maisha duni toka mwanzo hadi mwisho wa maisha yako ni maamuzi yako mwenyewe. Nakushauri kufanyia kazi hoja nilizozifafanua katika makala hii juu ya tabia 10 zitakazobadili masiha yako; nami nakuhakikishia utaona mabadiliko.
Ningependa kupata maoni yako juu ya mada jadiliwa hapa juu. Karibu pia uwashirikishe wengine makala hii. Usisahau pia kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
Asanteni mmefundisha vizuri
Tunashukuru sana; karibu sana Fahamuhili.com
Tunashukuru kwa darasa zuri
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Kwakwelii tunashukuru Sana kwa elim hizi mnozotupatia Kila siku tunajifunza mengi Sana .na kwakwelii hata tunafanya wengi wetu tunaonakabisa mwanga wabadae wakuitwa mabilionea .tunashukuru Sana kwaelim hizii tenaa sanaaaa!!!!
Tunashukuru sana kwa kuwa msomaji wetu; pia tunashukuru kwa maoni yako ya thamani; tunakutakia kila la heri katika kutimiza malengo yako…karibu sana Fahamuhili.
nimependa
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Nime waelewa sana
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com