
Madhara 8 ya Kusikiliza au Kutazama Mziki
Kwa hakika kila jambo lenye uzuri au faida lina hasara zake. Nafahamu umekuwa ukisikia faida kede kede za kusikiliza mziki, lakini haujasikia kuwa kwa upande mwingine mziki unaweza kuwa na madhara kwako. Ikiwa wewe ni mpenzi wa muziki, ni vyema ukafahamu madhara ya kusikiliza au kutazama mziki ili uutawale mziki usikuathiri.
1. Huathiri afya ya masikio
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kumeibuka vifaa mbalimbali katika swala la utengenezaji, usambazaji na hata usikilizaji wa mziki. Kutokea kwa teknolojia ya vifaa vya kusikilizia mziki vijulikanavyo kama headphones au earphones kumesababisha watu wengi hasa vijana kusikiliza mziki karibu kila mahali na kila wakati. Taarifa mbalimbali za kitabibu zinaeleza kuwa vifaa hivi vimechangia sana kuharibu masikio au mfum...