Sababu 7 za Kwanini Kila Mwanaume Anatakiwa Kujua kupika - Fahamu Hili
Friday, April 19Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Sababu 7 za Kwanini Kila Mwanaume Anatakiwa Kujua kupika

Washirikishe Wengine Makala Hii:
Kupika
Chanzo cha picha hii ni Genesmart.com

Kutokana na asili ya utamaduni wa Kiafrika, bado kwa kiasi kikubwa swala la kupika linachukuliwa kama kazi ya mwanamke. Wanaume wengi hawafahamu kupika wala hawataki kujifunza kupika.

Nimeshuhudia wengi wakiwa tayari kula hotelini au kula mikate pindi wakosapo watu wa kuwapikia chakula. Kwa hakika yapo mambo mengi mazuri ambayo mwanaume asiyejua kupika anayakosa.

Karibu nikushirikishe sababu 7 za kwanini kila mwanaume anatakiwa kujua kupika; nami naamini baada ya makala hii utajifunza mengi na kuhamasika.

1. Kuweza kula unachokitaka

Kwa njia ya kufahamu kupika unaweza kula chakula unachotaka ambacho isingekuwa rahisi kukipata hotelini au kupikiwa na mtu mwingine.

Ikiwa pia kuna aina fulani ya upishi unaipenda, basi kwa njia ya kufahamu kupika utaweza kuifanya wewe mwenyewe.

2. Kuokoa pesa

Kununua chakula hotelini au kwenye migahawa ni gharama kubwa kuliko kujipikia wewe mwenyewe. Ukifahamu kupika hutohitaji kununua mikate au chakula hotelini bali utapika chakula chako wewe mwenyewe kwa gharama nafuu.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema.

3. Hutegemei mtu

Mwanaume anapokuwa hujui kupika, ni wazi kuwa utakuwa unamtegemea mtu mwingine ampikie; hivyo mtu huyo asipo kuwepo ni lazima upate shida.

Kwa njia ya kufahamu kupika hatakama ni vyakula rahisi, utaweza kuishi bila kumtegemea mtu. Kwa kufahamu kupika unaweza pia kuanza maisha popote bila tatizo lolote.

4. Unalinda afya yako

Chakula ulichokipika wewe mwenyewe utakifahamu vyema. Hivyo chakula unachokipika wewe utahakikisha ni salama na bora kwa ajili ya afya yako. Hili ni tofauti na vyakula vinavyoandaliwa na mtu mwingine au katika mazingira ya kibiashara kwani kwa kiasi kikubwa huandaliwa kwa lengo la kupata pesa na si kulinda afya yako.

5. Uwezo wa kuhudumia familia

Hebu fikiri mama ni mgonjwa au amesafiri, watoto wanahitaji kula na kunywa lakini baba hajui kupika; je unafikiri nini kitatokea?

Ni ukweli usiopingika kuwa utunzaji wa familia katika swala la lishe utakuwa na changamoto kama njia mbadala hazitatumiwa. Hivyo mwanaume kujua kupika kunakupa uwezo wa kuhudumia familia vyema wakati wowote bila shida yoyote.

6. Hukuongezea maarifa ya maisha

Maarifa ya maisha (life skills) ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku. Mwanaume mwenye ujuzi wa kupika ni tofauti kabisa na mwanaume asiyejua kupika.

Mwanaume anayejua kupika anaweza kuandaa chakula popote na wakati wowote ambao atatakiwa kufanya hivyo bila shida yoyote.

7. Hurahisisha kupunguza uzito

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa vyakula vya kwenye hoteli na migahawa, vinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzito wa mwili.

Hivyo ikiwa mwanaume anajua kupika, anaweza kujipikia chakula chake mwenyewe ambacho hakitaathiri uzito wake.

Neno la Mwisho:

Naamini kama hujui na hupendi kupika, umeona jinsi unavyokosa mengi. Jifunze kupika leo na ufanye mazoezi ya kutosha ili unoe uwezo wako. Fahamu kuwa kupika hakukufanyi kuwa mwanamke bali kunakufanya kuwa mwanaume aliyekomaa zaidi.

Kumbuka, unaweza kujifunza kupika kupitia vitabu na tovuti mbalimbali kama vile http://www.misosi.co.tz/.

Je bado hutaki kupika? Je wewe unajua kupika na unaipenda kazi hiyo? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii; usisahau pia kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

0 0 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x