Sababu 10 za Kwanini Baadhi ya Watu Kamwe Hawatafanikiwa - Fahamu Hili
Friday, May 24Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Sababu 10 za Kwanini Baadhi ya Watu Kamwe Hawatafanikiwa

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kutofanikiwa

Kila mtu anatamani kufanikiwa, lakini siyo wote wanatimiza lengo hili. Ni wazi kuwa hakuna njia ya mkato ya kufika kwenye kitu kizuri.

Ukiwachunguza sana watu waliofanikiwa, utagundua kuwa kuna tabia au mambo kadhaa yanayoshabihiana kati yao. Pia ukiwachunguza watu walioshindwa au ambao hawajafanikiwa, utabaini pia kuna tabia au mambo kadhaa yanayofanana kati yao.

Je unatamani kufanikiwa? Basi fahamu sababu 10 zinazowafanya baadhi ya watu kamwe wasifanikiwe kwenye maisha yao.

1. Kutokujali muda

Mafanikio yamefugwa kwenye muda. Ili mtu aweze kufanikiwa ni lazima ajifunze kutumia muda wake vyema. Watu wasiofanikiwa hawana mipaka; huchelewa kila mahali, pia hawathamini muda wa wengine.

Hawana vipaumbele wala muda wa kuweka malengo na vipaumbele kwenye maisha yao; wao huishi tu kulingana na lile linalokuja mbele yao.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda.

2. Kuwa na visingizio

Walioshindwa hutoa visingizio vikubwa; husingizia na kulaumu kila kitu. Kila mara watu hawa hutafuta njia ya kuficha udhaifu wao kwa njia ya visingizio.

Watu waliofanikiwa nao wanakosea, lakini hujifunza kutokana na makosa yao na siyo kutengeneza visingizio.

Soma pia: Mambo 25 Unayoweza Kujifunza Kutokana na Makosa.

3. Kutokuwa na malengo

Malengo ni ramani muhimu ya kukuongoza kufika kwenye mafanikio au kutimiza ndoto zako. Watu walioshindwa hawana malengo wala hawafahamu faida za kujiwekea malengo maishani mwao.

“Maisha bila malengo ni sawa na kuanza safari bila kujua unakokwenda au unakotakiwa kufika.”

Soma pia: Faida 10 za Kuwa na Malengo Maishani.

4. Kutokuchagua mwenzi sahihi wa maisha

“Nina bahati sana kuwa na Melinda kama mpenzi wangu katika maisha na kazi. Ananihamasisha kila siku.”

Bill Gates

Swala la mwenzi sahihi wa maisha linapuuzwa na watu wengi bila kufahamu umuhimu wake. Mwenzi sahihi kwenye maisha atakuwezesha kufanya mambo mbalimbali kama vile:

  • Kukusaidia kuweka na kutimiza malengo yako.
  • Kukushauri na kukutia moyo.
  • Kukusaidia katika mipango na mikakati ya kutimiza ndoto zako.
  • Kujali na kuheshimu hisia na utu wako.

Ni wazi kuwa watu waliofanikiwa wanafamu umuhimu wa kuwa na wenzi sahihi kwenye maisha. Unapokosa mwenzi sahihi utapata mwezi ambaye hana malengo wala maono; vipaumbele vyake ni matumizi na anasa.

5. Kutokuweka kwenye matendo

Watu wengi ni wazungumzaji kuliko watendaji. Hili ni kinyume kwa watu waliofanikiwa kwani wao huweka kwenye matendo zaidi bila hata kujali kama watakwama au laa.

Ni muhimu kujifunza kuweka kwenye matendo mawazo na mipango yetu mbalimbali kuliko kuizungumzia pekee.

“Njia ya kuanza ni kuacha kuzungumza na kuanza kutenda.”

Walt Disney

6. Kuahirisha

“Nitafanya kesho”, “Bado kuna muda”, “Ni mapema sana kufanya hili”, “Bado najifikiria”, n.k. Ni baadhi ya kauli zinazopendwa na watu wanaopenda kuahirisha mambo.

Watu ambao hawatafanikiwa huahirisha kila jambo, huamini kuwa maisha yao yanajengwa kesho na si leo. Hili ni tofauti kwa watu waliofanikiwa kwani wao huamini kuwa maisha ya kesho huandaliwa leo.

“Baadaye inamilikiwa na wale wanaoiandaa leo.”

Malcolm X

7. Kutokusema hapana

Kila mara nimekuwa nikisisitiza kuwa jibu la hapana lina nguvu na umuhimu sana. Kusema hapana ni jambo linalofanywa sana na watu waliofanikiwa kuliko wale wasiofanikiwa.

Jibu la hapana humtenga mtu na mipango, watu, na hata vitu visivyokuwa na umuhimu kwenye maisha na malengo ya mtu husika.

Hivyo watu wasioweza kusema hapana, kamwe hawawezi kufanikiwa kwani huchukuliwa na kila mawimbi kisha hushindwa kufanikiwa.

Soma pia: Faida 5 za Kusema “Hapana”.

8. Kutokupenda maarifa

“Uwekezaji katika maarifa hulipa maslahi bora.”

Benjamin Franklin

Ni watu wachache sana ndiyo wanaofahamu umuhimu wa maarifa katika mchakato mzima wa kufanikiwa.

Watu waliofanikiwa hujifunza mambo mengi kadri wawezavyo ili kuongeza maarifa na uelewa wao. Maarifa sahihi na ya kiwango cha kutosha, yatakuwezesha kufanya maamuzi sahihi na bora kwenye maisha yako.

Ikiwa husomi vitabu, makala (mfano hii), kusikiliza na kutazama vipindi vinavyoongeza kiwango chako cha maarifa; kamwe huwezi kufanikiwa.

Soma pia: Tabia 10 Unazotakiwa Kijifunza Kutoka kwa Watu Waliofanikiwa.

9. Matumizi mabaya ya pesa

Hili ni janga linalowakabili watu wengi ambao bado hawajafanikiwa. Watu wengi hupata pesa lakini zinakwisha bila kujua wamefanya nini chenye manufaa kwao.

Ni muhimu kama mtu anapenda kufanikiwa akajifunza matumizi mazuri ya pesa. Hii itamwezesha kutumia pesa kuendeleza na kufikia ndoto zake.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema.

10. Mawazo ya kutokuweza au kushindwa

“Badili kufikiri kwako na utakuwa umebadili ulimwengu.”

Norman Vincent Peale

Maisha yetu ni matokeo ya vile tunavyofikiri. Ikiwa unafikiri kuwa huwezi, wewe ni maskini, hutofanikiwa n.k. Basi utakuwa hivyo.

Mara nyingi utasikia watu wakisema “mimi siwezi hili”, “huu ni udhaifu wangu”, “hili limeshanishinda”, “nikishindwa jambo nimeshindwa” n.k. Haya ni mawazo ya kujikwamisha wewe mwenyewe.

Ikiwa hutaacha mawazo haya, basi ni vigumu sana kufanikiwa kwani yatakuwa ni kizuizi kwako. Amini kila kitu kinawezekana; ni fikra zako tu ndiyo zinakukwamisha.

Soma pia: Nukuu (Quotes) 50 Zitakazo Kuhamasisha Maishani Mwako.

Neno la mwisho

Je una tabia hizi? Naamini kama una tabia au mambo haya yaliyoelezwa hapa, sasa utaweza kuyaacha ili uweze kufanikiwa kwenye maisha yako. Kumbuka ili ufanikiwe unahitaji mikakati na maamuzi thabiti yanayofanywa bila kukata tamaa.

Je una swali au maoni? Tafadhali tuandikie hapo chini. Karibu ufuatilie ukurasa wetu wa Facebook pamoja na kuwashirikisha wengine makala hii.

3.5 6 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

1 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
waukawa
waukawa
11 months ago

mm tabia zote hapo ninazo

1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x