Mambo 10 ya Kujifunza Kama Mjasiriamali Kutokana na Anguko la Nokia - Fahamu Hili
Thursday, May 23Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 ya Kujifunza Kama Mjasiriamali Kutokana na Anguko la Nokia

Washirikishe Wengine Makala Hii:
Nk

Kama wewe uliwahi kidogo kwenye ulimwengu wa simu za mkononi, utakuwa umetumia au hata kusikia juu ya uimara, umaarufu na ubora wa simu za Nokia. Mnamo mwaka 1998 Nokia ilikuwa ndiyo kampuni bora ya kutengeneza na kuuza simu za mkononi duniani kote.

Faida ya kampuni ya Nokia ilikwea kutoka dola za kimarekani bilioni 1 mwaka 1995 hadi dola bilioni 4 mwaka 1999; huku simu yake ya Nokia 1100 ikiwa ndiyo simu iliyowahi kuuzwa zaidi duniani.

Nokia 1100 (Chanzo cha Picha: marketplace.citify.ca)

Pamoja na mafanikio haya Nokia iliyoyapata, kwa kipindi kisichozidi miaka sita kuanzia mwaka 2007, hisa za Nokia ziliporomoka kwa asilimia 90.
Kwa kutambua nafasi Nokia iliyokuwa nayo ikilinganishwa na anguko kubwa lililoipata, ni wazi kuwa kuna mengi ya kujifunza kama mjasiriamali au kiongozi. Karibu ufuatilie makala hii ili ujifunze mambo haya 10 niliyoyajadili kuhusu anguko hili.

1. Ni muhimu kuelewa mahitaji ya soko na wateja

Moja kati ya kosa lililochangia kuporomoka kwa kampuni ya simu ya Nokia ni kushindwa kutambua na kukidhi mahitaji ya soko na wateja.

Mnamo mwaka 2007 kampuni ya Apple ilikuja na smartphone yake ya kwanza ambayo ilibadili kabisa upepo wa simu za mkononi. 

Lakini jambo la kusikitisha ni kuwa Nokia walieendelea kubaki kwenye simu za zamani; na hata walipokuja na smartphone, mfumo endeshi (Operating system) wao wa Symbian haukuweza kumudu ushindani wa mifumo mingine kama ule wa Android wa Google.

Hivyo basi, ni muhimu kujifunza umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya soko na wateja kutokana na hili lililoikumba kampuni ya Nokia.

2. Ubunifu ni msingi muhimu kwenye biashara

Watu wanapenda vitu vya kisasa na vyenye muonekano na utendaji mzuri; haitoshi tu kutengeneza kifaa imara lakini cha kizamani.

Ni ukweli usiopingika kuwa Nokia walikuwa watengenezaji wa simu imara sana lakini wakakosa ubunifu pamoja na kushindwa kwenda na wakati. Wakati wenzao wakihamia kwenye smartphone pamoja na mifumo endeshi ya kisasa, wao bado waiendelea kung’ang’ania uzamani.

Ni muhimu kuhusisha ubunifu katika mradi wowote unaoufanya ili uweze kujitofautisha na wengine na kufikia malengo yako.

3. Unapofanikiwa si vyema kujisahau

Mafanikio yanadanganya sana, hasa kama yasipotawaliwa vyema au ikiwa hukujiandaa kuyapokea. 

Watu wengi au biashara nyingi zinapokuwa kwenye kipindi cha mafanikio makubwa hujisahau na huona kuwa kila kitu kiko sawa na kitaendelea kuwa hivyo; mwishowe washindani wao huja na mbinu mpya na kunyakua mafanikio yao.

Kampuni ya Nokia ilikuwa kwenye mafanikio makubwa sana na ikajisahau na kujiamini kupita kiasi. Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa walikataa hata kupokea ushauri na mabadiliko kwa kuwa waliamini kuwa imani ya wateja  na soko lao vipo tu na vitaendelea kuwepo.

Ni muhimu sana kwa mjasiriamali au mwekezaji yoyote kufikiri nje ya boksi; na kujiuliza maswali kama vile:

  • Je biashara hii isipokuwa na mafanikio haya ya sasa nitafanyaje? 
  • Je mawazo yangu yakipitwa na wakati nitafanyaje? 
  • Je mshindani wangu akitokea nitammudu vipi?
  • Je nina wazo au mpango gani wa akiba?

4. Maono ni muhimu sana

Moja ya jambo lililoigharimu sana kampuni ya Nokia ni kukosa maono sahihi, hasa ndani ya viongozi wake. Maono sahihi ni msingi wa kufanikiwa kwenye mradi au jambo lolote. Hata kama unakutana na changamoto nyingi kiasi gani ni rahisi kufanikiwa ikiwa utafuata maono sahihi uliyojiwekea.

Kampuni ya Nokia ilifika mahali ikawa inachukua maamuzi au mipango ya zimamoto (yaani ya kukabili tu ile hali iliyoko mbele yake) na si mipango yenye tija na malengo ya muda mrefu. 

Kwa mfano Nokia walikuja na bidhaa mpya, mara wakaja na sera mpya ya masoko, mara wauze kampuni, mara wainunue tena n.k. Haya yote yalizidi kuidhoofisha kuliko ambavyo ingekuwa kama wangekuwa na maono sahihi wanayoyafuata.

5. Maamuzi sahihi ni msingi wa mafanikio

“ Maamuzi yako ni matokeo ya kesho .”

Ni wazi kuwa maamuzi unayoyachukuwa leo ndiyo huamua kesho yako, na si kesho yako moja tu bali kesho zako zote. Na ikumbukwe kuwa maamuzi mengi yakishafanyika hayarekebishiki tena.

Kampuni ya Nokia ilikosea katika maamuzi mengi iliyokuwa inayafanya hasa baada ya kuanza kuporomoka. Moja kati ya maamuzi mabaya kabisa waliyoyafanya ni kuiuza kampuni ya Nokia ikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 50 ikauzwa kwa bei ya dola za Marekani bilioni 7 mwaka 2014 kwa kampuni ya Microsoft.

Hebufikiri kampuni yenye thamani ya dola bilioni 50 inauzwa kwa dola bilioni 7, je haya si maamuzi kichaa?

Hata hivyo haikuishia hapo; kwani baada ya kununuliwa na kampuni ya Microsoft, Nokia ilianza kutumia mfumo endeshi wa Windows na kuifanya kuporomoka zaidi. Microsoft nao waliathiriwa na ununuzi huu wa Nokia kwani mara tu baada ya kuinunua walipoteza dola bilioni 15 kutoka kwenye hisa zake sokoni.

Maruweruwe hayakuishia hapo kwani mnamo mwaka 2016 Nokia ilinunuliwa na kampuni ya HMD Global kwa thamani ya dola milioni 350.

Ni wazi kuwa maamuzi mabaya yanaweza kugharimu biashara au mradi ule unaoufanya, hivyo ni vyema kuwa makini wakati wa kuchukua maamuzi mbalimbali.

6. Kinga ni bora kuliko tiba

Mara nyingi miradi ya kiafrika huathiriwa sana na changamoto mbalimbali kwani mingi huwa haina mipango ya kujikinga na changamoto zinazoweza kutokea bali husubiri changamoto zitokee ndipo suluhisho litafutwe.

Ndivyo ilivyokuwa kwa kampuni ya Nokia kwani haikuwa na mipango madhubuti ya kukabili changamoto kama vile mabadiliko ya tekenolojia, soko, ongezeko la ushindani, n.k.

7. Ungozi sahihi ni msingi wa mafanikio

“Uongozi ni ufunguo wa asilimia 99 ya jitihada zote za mafanikio. ”

Erskine Bowles

Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa kulikuwa na tatizo kubwa kwenye uongozi wa kampuni ya Nokia. Inaelezwa kuwa kulikuwako na mgawanyiko mkubwa kati ya watawala wa juu na wale wa kati; huku wale wa kati wakikabiliwa na hofu kubwa ya kutoa maoni au kueleza hali halisi iliyokuwa ikiikabili kampuni.

Swala hili lilipelekea ugumu katika kutatua changamoto za kiuchumi na kiutendaji zilizokuwa zikiikabili kampuni ya Nokia.

Ni muhimu kuhakikisha kuna uongozi mzuri katika mradi au ofisi yoyote ili maono yabebwe vyema na watu stahiki.

“ Kiongozi ni yule anayefahamu njia, anakwenda kwenye njia hiyo, na anaonyesha njia. ”

John C. Maxwell

Soma pia: Sifa 10 Zitakazokufanya Kuwa Kiongozi Bora

8. Kupuuza mabadiliko ya teknolojia ni uangamivu

Lengo la teknolojia ni kurahisisha maisha ya kila siku; hivyo hata miradi, biashara au hata taasisi mbalimbali zinapaswa kutopuuzia mabadiliko ya teknolojia kama zinataka kufikia malengo yake.

Hivi leo watu wanataka vitu bora vya kisasa vinavyorahisisha maisha yao; ndiyo maana Nokia walipoyapuuzia mabadiliko ya teknolojia au kuchelewa kuyapokea walipoteza asilimia 90 ya hisa za thamani yake. 

9. Ushindani si jambo la kupuuziwa

Kama nilivyotangulia kusema kuwa mafanikio yanadanganya; ni wazi kuwa mara nyingi watu wanapofanikiwa hupuuzia pia swala la ushindani. Mwaka 1999 wakati Nokia ikiwa kinara wa kutengeneza simu duniani haikuwahi kufikiri kuwa washindani wake kama vile Sumsung, Vivo, Oppo, Tecno, n.k. Wangekuja na mbinu mpya na kuipita Nokia kwa kasi kubwa.

Hivyo basi, unapotekeleza mradi wowote hakikisha unatupa jicho kwa washindani wako, si kwa nia mbaya ila jifunze kusoma upepo na weka mikakati madhubuti ya kukabili ushindani kwa namna njema na halali.

10. Kurudi kwenye nafasi iliyopotezwa siyo rahisi

Kuna siku niliona gari limeandikwa “Chunga sana ulicho nacho, kikipotea sahau!”; baada ya kutafakari sana nikajua kuwa usemi huu una mashiko sana. Mara nyingi tukiwa na vitu hatutambui thamani yake; na ni vigumu sana kuvipata tena tukivipoteza.

Nokia wangejua kuwa kurudi kwenye nafasi waliyokuwa nayo kungekuwa jambo gumu sana wangelinda sana nafasi yao kwa kuchukua mikakati sahihi mapema. Ingawa sasa Nokia imeanza kujikongoja kujijenga tena chini ya HMD Global na kuanza kutoa simu mpya za kisasa kama vile Nokia 8, lakini bado wanasafari ndefu.

Hivyo, ni muhimu kuchukua mikakati mapema ya kulinda tulichonacho kwani kukipata tena inaweza isiwezekane kabisa au iwe ni kwa gharama kubwa. Ikiwa ni wateja, wazo la biashara, soko, imani ya wateja, au hata fursa basi vinatakiwa kulindwa sana.

Neno la Mwisho

Naamini yapo mambo mengi sana ya kujifunza kutokana na anguko hili la iliyowahi kuwa kampuni mashuhuri ya vifaaa vya mawasiliano ya Nokia. Nimeorodhesha machache tu lakini naamini kwa jicho la pili nawe unaweza kuwa umejifunza au umesikia jambo jingine ambalo linaweza kuwa funzo pia.

Karibu utoe maoni yako hapo chini kuhusiana na makala hii, pia usisahau kuwashirikisha wengine makala hii.

4.7 3 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

6 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Danie
Danie
3 years ago

Facts Bro..keep up the good work

Joseph
Joseph
2 years ago

That’s good

Abuu dharry
Abuu dharry
1 year ago

Shukran sana kwa elimu yako nzuri

6
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x