Makosa 10 ya Kuepuka Unapotengeneza Logo au Nembo - Fahamu Hili
Saturday, April 20Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Makosa 10 ya Kuepuka Unapotengeneza Logo au Nembo

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kutengeneza Logo

Nembo au logo ni jiwe la msingi la bidhaa na kampuni yako. Utambulisho wa biashara, kampuni yako au bidhaa unaonyeshwa kupitia nembo yako, ambayo ni pamoja na jina la kampuni yako. Hivyo, nembo ni moja kati ya mambo makuu ambayo yanafanya biashara yako kukumbukwa na kutambulika.

Kwa kutambua umuhimu huu, kampuni na watu mbalimbali wamekuwa wakiwekeza fedha nyingi ili kupata nembo bora. Pamoja na kuwekeza pesa nyingi, bado kampuni na watu wengi hawapati nembo bora.

Kwa mfano kampuni ya Pepsi iliwekeza dola milioni 1 lakini wakaishia kupata nembo iliyokumbana na ukosoaji mkubwa.

Ni wazi kuwa kuna mambo unayotakiwa kuyazingatia kabla ya kuamua kulipia au kutengeneza nembo yako. Fahamu makosa 10 ambayo kama utayaepuka wakati wa kutengeneza au kuchagua nembo, basi utaweza kuwa na nembo bora.

1. Kosa la kuchagua nembo inayofanana na nyingine

Ni rahisi kujikuta unatengeneza nembo inayofanana na ya kampuni au mtu mwingine. Hili linaweza kusababishwa na mambo kama vile kutumia programu au mfumo wa aina moja kutengeneza nembo husika; pia linaweza kusababishwa na kutaka kwa makusudi kufananisha nembo ili utambulike haraka.

Hili ni kosa baya, kwani linaweza kukuletea matatizo mbalimbali kama vile mgogoro wa kisheria wa hakimiliki pamoja na kuwachanganya wateja.Logo inayofanana

Soma pia: Mambo ya Kuzingatia Kabla ya Kuchagua Jina la Biashara.

2. Uchaguzi mbaya wa rangi

Watu wengi hawajui kuchagua na kutumia rangi mbalimbali ipasavyo. Hili huwasababisha watu wengi kushindwa kufahamu maana ya rangi husika na kama inafaa au laa katika nembo zao. Ni vyema ukazingatia haya:

  • Maana ya rangi husika.
  • Ubora wa rangi husika.
  • Kufaa kwa rangi katika matumizi mbalimbali kama vile kazi za uchapishaji, mtandao, video, picha n.k Ni vyema ukahakikisha kuwa rangi ya nembo itafaa kwenye kazi tajwa hapo juu na nyinginezo.

Naamini ukizingatia haya utaweza kuchagua rangi itakayofaa kulingana na kazi au biashara yako.

3. Kuchagua mwandiko wowote

Kama ilivyo kwa rangi, mwandiko una umuhimu na maana kubwa kwenye nembo yako. Hivyo ni vyema ukachagua mwandiko bora utakaokidhi matumizi na kuitambulisha biashara yako vyema. Hakikisha mwandiko wako ni wa kipekee, haumilikiwi kisheria na mtu au kampuni nyingine pia unasomeka vyema katika matumizi yote.

4. Kuweka kila kitu kwenye nembo au logo

Ni kweli kuwa nembo ni kitambulisho cha biashara au kile unachokifanya, lakini haiwezi kueleza kila kitu. Hakikisha nembo yako haina vitu vingi visivyokuwa na sababu. Hakikisha inaeleweka vyema bila tatizo lolote. Kwa mfano kama kauli mbiu (slogan) yako ni ndefu sana, basi hakuna haja ya kuiweka kwenye nembo yako.Kila kitu

5. Kuhusisha matukio ya muda

Mara nyingi kuna watu na matukio yanayoibuka kwa muda fulani. Si vyema kuhusisha matukio au watu hawa katika nembo yako; kwani ni muhimu kutengeneza nembo itakayofaa muda mrefu au wote. Ni wazi kuwa watu au matukio haya yatakapopita na nembo yako itakuwa pia imepitwa na wakati.

Kwa mfano nembo kama vile “Kanumba Barber Shop”, “Spartan Studio”, “Prison Break Elctronics” “Obama Supermarket” ni baadhi tu ya mifano ya nembo ambazo zimehusisha matukio na watu wa muda.

6. Nembo za maumbo dhahania

Yapo maumbo yanayopatikana katika programu mbalimbali za kutengenezea logo; maumbo mengine hayana maana inayoeleweka; yaani yana maana dhahania tu (maana inayofahamika na mbunifu pekee).

Unapotumia maumbo kama haya ni rahisi kumchanganya mtu anayeona nembo yako, kwani hataweza kupata maana au ujumbe lengwa. Tumia maumbo ambayo yanasadifu kile kinachofanywa na kampuni au bidhaa yako.

7. Kutokuhariri

Ni vyema ukafahamu kuwa kazi ya kibunifu na kitaalamu ni lazima ihaririwe. Ni vyema ukahariri kwa makini nembo yako ili kuhakikisha haina makosa kama vile makosa ya tahajia (spelling) n.k

8. Kuweka alama za kipekee

Alama kama TM, LLC, INC, LTD, n.k kwenye nembo yako hakuifanyi nembo kuwa ya kisasa bali ya kizamani. Hii ndiyo sababu hata google wameondoa alama hizi katika nembo yao. Mara nyingi alama hizi huwa hazionekani au kusomeka vyema kwenye maeneo ambayo nembo inatumika kwa vipimo vidogo.Kutumia alama za pekee

9. Kutumia huduma za logo za bure

Mara nyingi kutengeneza nembo kwa kutumia huduma au programu za bure, kunakufanya utengeneze logo ambayo siyo ya kipekee. Hili linatokana na watu wengi kupendelea na kutumia huduma hizi. Kosa hili linaweza pia kukusababisha kuingia kwenye migogoro ya kisheria na watu au kampuni nyingine.

10. Kukosa ubunifu

Kutengeneza nembo ni kazi nyeti ambayo inahitaji ubunifu na uzoefu mzuri ili kuwa na matokeo mazuri. Ni ukweli usiopingika kuwa hii ndiyo sababu watu hulipwa kiwango kikubwa cha pesa ili kutengeneza nembo mbalimbali.

Watu wengi wamekuwa wakijikuta wakitengeneza nembo mbaya kutokana na kukosa ubunifu. Ninakushauri ikiwa unaona ni vigumu kutengeneza nembo yako mwenyewe ni vyema ukamtumia mtu mwenye uwezo mzuri wa ubunifu.

Hitimisho

Naamini umefunguka macho kwani umefahamu makosa ya kuepuka unapotengeneza nembo. Ni wazi kuwa umeona ni kwa nini watu wengi hutengeneza nembo mbaya ambazo zinashindwa kutangaza au kuwakilisha biashara na huduma zao vyema. Tafiti na tumia muda wa kutosha kubuni na kuhariri nembo yako kadri uwezavyo ili iwe bora kabisa.

Soma pia: Nembo/Logo za Kibiashara Zilizobeba Maana Usizozijua.

Naamini una swali au maoni; tafadhali tuandikie maswali na maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Usisahau kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

3.6 7 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

7 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
BARAKA MAKONGORO
BARAKA MAKONGORO
3 years ago

nafurahiwa sana na muongozo wa makala zako nimependa sana kujifunza zaidi ili namimi niwe mubunifu kama wew swahi ninamna gani naweza kukuata ili namimi niweze kufanya kama wew ahsante

pray god
pray god
3 years ago

habar bro


Jeremiah tango
Jeremiah tango
1 year ago

Naomba kufaham Jeh wewe unatengenezaga nembo

Helton
Helton
10 months ago

Kw mfano logo ikawa na picha ya mlima kilimanjaro je inaruhusiwa au ni alama ya taifa

7
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x