Mbinu 10 za Uhakika za Kufahamu Kiingereza/English kwa Muda Mfupi - Fahamu Hili
Monday, May 25Maarifa Bila Kikomo

Mbinu 10 za Uhakika za Kufahamu Kiingereza/English kwa Muda Mfupi

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kufahamu Kiingereza

Kujifunza lugha mpya kunaweza kuwa ni kugumu, lakini inawezekana. Je unatamani kufahamu na kumudu lugha ya Kiingereza kwa muda mfupi? Kumudu Kiingereza inawezekana lakini kuna mambo kadhaa unatakiwa kuyafahamu na kuyafanya kwa uhakika.

Ikiwa unapenda kuwa wa kimataifa, basi fuatilia mbinu 10 za uhakika zitakazo kuwezesha kufahamu Kiingereza/English kwa muda mfupi.

1. Penda na furahia Kiingereza

Ili uweze kufanya au kujifunza kitu chochote ni lazima kwanza ukipende. Ikiwa unataka kufahamu Kiingereza kwa muda mfupi ni lazima ukipende kwani ndipo utaweza kujifunza kila mara bila kuchoka wala kukata tamaa. Kila mara jihamasishe kwa kutafakari manufaa utakayoyapata baada ya kufahamu Kiingereza vizuri.

2. Jifunze Kiingereza kila siku

Huwezi kufahamu Kiingereza kama hutojifunza kila siku. Hakikisha unaongeza misamiati, unajifunza matamshi pamoja na kanuni mbalimbali za lugha.

Mambo ya kukumbuka hapa:

  • Nunua kamusi ya Kiswahili na Kiingereza.
  • Soma vitabu na machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
  • Tumia tovuti za kujifunza lugha kama vile Duolingo, Babbel, BBC Learning English n.k. kujifunza Kiingereza.
  • Kama inawezekana, tafuta mwalimu au chuo cha kujifunza Kiingereza.

3. Zungumza Kiingereza

Huwezi kumudu kuzungumza Kiingereza kama hutozungumza. Jitahidi katika kutumia Kiingereza katika mazungumzo yako hata kama utakosea.

Jifunze maneno uliyoyazoea kuyatumia mara kwa mara na uyafahamu kwa Kiingereza ili uyatumie katika mazungumzo.

Jambo la kuzingatia ni kuangalia tu mtu unaye ongea naye; ikiwa mtu hajui Kiingereza basi usitumie Kiingereza kwani anaweza kuona unamdharau.

Hata kama huna mtu wa kuzungumza nae, unaweza kuzungumza mwenyewe tu kwa sauti ndogo bila shida; kwani ni mambo mangapi unayokuwa unanayawaza na kuyajadili akilini mwako peke yako? Anza kuzungumza sasa.

4. Andika Kiingereza

Kuandika kwa Kiingereza kutakusaidia sana kuboresha uwezo wako wa Kiingereza cha kuandika. Ikiwa unaandika ujumbe, machapisho (posts) kwenye mitandao ya kijamii, kadi, au hata shajara (diary); basi tumia lugha ya Kiingereza.

5. Usiogope kukosea

Ni rahisi mtu kushindwa kujifunza Kiingereza kwa kigezo tu cha kuogopa kufanya makosa. Makosa ni hatua muhimu katika kujifunza kitu chochote.

Unapofanya makosa na kuyabaini, ni wazi kuwa mbeleni hutoyarudia tena. Hivyo, tumia Kiingereza katika kila eneo bila kuogopa kufanya makosa.

6. Sikiliza na tazama vitu au vipindi vya Kiingereza

Najua wengi ni wafuasi wa miziki na filamu; miziki na filamu za Kiingereza zinaweza kukusaidia kwa kiasi kikubwa kujifunza lugha. Usipende kutazama filamu zilizotafsiriwa; jitahidi kujifunza maana za maneno unayosikia kwenye filamu na miziki kwa kutumia kamusi niliyoitaja kwenye hoja namba moja.

Jitahidi pia kutazama vipindi au hotuba mbalimbali zilizoandaliwa kwa lugha ya Kiingereza kupitia televisheni au mtandao wa YouTube. Jifunze jinsi watu wanavyotamka maneno pamoja na kuchunguza maana zake.

7. Waza kwa Kiingereza

Kuwaza kwa Kiingereza? Ndiyo, kuwaza kwa Kiingereza kutaongeza uwezo wako wa lugha kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano badala ya kuwaza “Nitakwenda mjini kesho…” unaweza kuwaza “I will go to town tomorrow…” n.k. Kwa kufanya hivi kutakujengea uwezo wa kutumia na kufahamu Kiingereza zaidi.

8. Elewa na usikariri kanuni

Kila lugha ina kanuni zake. Usipoteze nguvu kubwa kukariri kanuni, bali elewa matumizi ya kanuni zinazotawala mpangilio wa maneno na matumizi yake.

Kwa mfano sentensi nyingi za Kiingereza huwa na (Mtenda-Tendo-Mtendwa au Kitendwa) yaani (Subject-Verb-Object)

Mf. Mary killed the dog.

John is cooking the food.

Kufahamu kanuni kama hii na nyinginezo, kutakuwezesha kuelewa kwanini mtenda huanza kisha kufuatiwa na tendo pamoja na mtendwa au kitendwa katika sentensi za Kiingereza.

9. Tafuta rafiki au mshirika

Ikiwa kuna mtu ambaye mnaweza kujifunza kwa pamoja, basi mshirikishe ili mjifunze kwa pamoja. Au ikiwa kuna mtu anamudu vyema Kiingereza, unaweza kumwomba akusaidie katika mchakato wako wa kujifunza.

Kwa kufanya hivi utaweza kuuliza maswali au hata kuzungumza moja kwa moja na mshirika wako. Kama wewe ni mtumiaji mzuri wa mtandao, unaweza kupata mshirika kwenye mtandao pia.

10. Kuwa na subira na usikate tamaa

Ni wazi kuwa zipo chngamoto katika kujifunza lugha mpya hasa Kiingereza. Lakini ni muhimu ukafahamu kuwa ni swala la muda, uvumilivu, mazoezi na nia tu ndivyo vitakavyokuwezesha kufahamu Kiingereza vyema. Hakuna kitu kizuri kinachotokea kwa usiku mmoja, fanya bididi usikatishwe tamaa na changamoto; nawe kwa hakika utafikia lengo.

Soma pia: Hatua 7 za Maumivu Zisizoepukika Kabla ya Kufanikiwa.

Hitimisho

Ni ukweli usiopingika kuwa kufahamu Kiingereza siyo lazima uwe umezaliwa kwenye nchi ya watu wanaozungumza Kiingereza, bali ni kuzingatia mbinu tajwa hapo juu pekee. Naamini ukizingatia mbinu zilizojadiliwa hapo juu kwa bidii utaona matokeo mazuri katika uwezo wako wa lugha ndani ya muda mfupi.

Je bado umekwama kwenye kujifunza Kiingereza? Je una swali au maoni? Tafadhali tuandikie hapo chini; pia usisahau kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook pamoja na kuwashirikisha wengine makala hii.

Washirikishe Wengine Makala Hii:

12
Tafadhali tuandikie maoni yako:

avatar
5 Comment threads
7 Thread replies
0 Followers
 
Most reacted comment
Hottest comment thread
7 Comment authors
lilian danieShabaniKornelio Maangasam ckiperSimon daniel Recent comment authors
newest oldest most voted
Shukuru mohamed shabani
Guest
Shukuru mohamed shabani

Na shukuru sana kwa muongozo

Kornelio Maanga
Admin

Nashukuru sana kwa kutembelea blog yetu ya Fahamuhili; tunashukuru pia kwa maoni yako mazuri.

Mussa Mc
Guest
Mussa Mc

Vizuri sana na je vipi kama mtu huna hata mtu mmoja mshiriki inawezekana kujifunza kiingereza?

Kornelio Maanga
Admin

Ndiyo, unaweza kujifunza kwa kutumia mbinu nyingine tajwa; Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com

Simon daniel
Guest
Simon daniel

Nimependezewa na maarifa mbalimbali mnayotoa

Kornelio Maanga
Admin

Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com

lilian danie
Guest
lilian danie

asante sana kwa ushauri mzuri wa namna ya kujifunza kingereza

Kornelio Maanga
Admin

Asante sana; karibu sana Fahamuhili.com

sam ckiper
Guest
sam ckiper

kwanza kabisa nianze kwa kuwashukuru kwa kazi ya kuelimisha jamii pia namimi ni mmoja kati ya wanao jifunza kiingereza kwa bidii sana ila nilikuwa naomba msaada zaidi

Kornelio Maanga
Admin

Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com tukupe ushauri.

Shabani
Guest
Shabani

Nashukuru mungu kwa elim mlio nipatia hakika tufkie malengo bi~ithin Allah

Kornelio Maanga
Admin

Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com