
Katika jaamii zetu za kiafrika suala la mikopo ya bidhaa au fedha kutoka kwenye biashara kwenda kwa wateja limezoeleka sana. Ingawa jambo hili linaweza kuwa na manufaa kwa upande fulani, hata hivyo kutokana na kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watu wengi jambo hili limekuwa na athari nyingi kuliko faida.
Inawezekana umekuwa ukiwakopesha wateja wako wa maana sana, au umekuwa ukitumia mikopo kama njia ya kuuza huduma au bidhaa zako, lakini karibu nikushirikishe athari tano za mikopo hiyo.
1. Kumpoteza mteja
Kuna usemi usemao kumkopesha mteja ni kumfukuza. Nimesikia mara kadhaa wafanyabiashara wakisema tangu ni mkopeshe haji tena dukani kwangu, au tangu nimkopeshe anapita mbali tu. Mara nyingi mteja akishakopeshwa pesa au bidhaa haji tena kwenye biashara husika ili kukwepa kulipa deni.
Kuliko umpoteze mteja kwa kumkopesha ni bora umueleze ukweli kwa kutumia busara; ingawa hatofurahi kwa wakati ule lakini baada ya muda atakuelewa na ataendelea kuwa mteja wako.
Soma pia: Mbinu 10 za Kuongeza au Kuvutia Wateja Kwenye Biashara
2. Ugomvi au kuharibu mahusiano
Kuna msemo usemao kukopa harusi kulipa matanga. Mara nyingi watu huja kwa uso mzuri uliojaa furaha na uaminifu wakati wa kukopa. Mara tu baada ya kukopa maisha ya shari na kusumbuana yanaweza kutokea hasa kwa wale wateja wasio waaminifu kulipa deni.
Kuna wafanyabiashara walioishia kugombana vibaya au hata kuvurugika kabisa kwa mahusiano yao na baadhi ya wateja wao kutokana na kuwakopesha bidhaa au pesa kutoka kwenye biashara zao.
Hivyo basi, kuliko uishie kugombana na wateja wako au watu wako muhimu, ni vyema ukaepuka suala hili la mikopo katika biashara yako.
3. Athari katika mzunguko wa pesa
Pesa za biashara zinatakiwa kuzunguka na si kukaa eneo moja. Mtaji wa biashara unapokuwa bidhaa katika biashara, bidhaa hizo zinapaswa kuuzwa; baada ya bidhaa hizo kuuzwa tunatakiwa kupata mauzo ambayo hujumuisha sehemu ya mtaji na faida. Mtu anapokopa pesa au bidhaa kutoka kwenye biashara yako, moja kwa moja anavuruga mzunguko huu.
Hili husababisha matatizo kama vile kukosa pesa timilifu kwa ajili ya manunuzi au gharama nyingine. Tatizo hili limewasababishia wengine kuchukua pesa zao binafsi au zilizoko nje ya biashara ili kuzipa pengo lililotokana na mikopo ili biashara isiyumbe.
4. Kupoteza fedha na mali
Kwa hakika hakuna hakikisho la asilimia mia moja kuwa pesa au bidhaa ulizomkopesha mteja zitalipwa. Ikizingatiwa kuwa watu wengi hukopeshana pesa na bidhaa kienyeji bila kufuata taratibu za kisheria zinazoweza kuwalinda baadaye iwapo mkopaji hatokuwa mwaminifu.
Hivyo basi, mikopo inaweza kukusababishia kupoteza fedha na mali ulizowakopesha wateja iwapo wateja hao hawatakuwa waaminifu kulipa, jambo ambalo linaweza kukuathiri pia kibiashara.Â
Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema
5. Kufilisika au kufa kwa biashara
Hoja hii ni hitimisho tu la hoja zilizotangulia; ikiwa mikopo haitalipwa kwa wakati au haitolipwa kabisa, biashara yako inaweza kufilisika au kufa kabisa. Imeshuhudiwa wafanyabiashara wakiwa na mikopo wanayodai kutoka kwa wateja wao ambayo inazidi hata nusu ya mitaji yao; huku wakiwa hawana uhakika kama watalipwa pesa hizo au laa. Ni muhimu sana kulichukulia swala la mikopo kwa tahadhari kubwa lisije likasababisha biashara yako kufa.
Soma pia: Kanuni 15 za Ujasiriamali Ambazo ni Lazima Uzifahamu
Je kuna lolote unaloweza kufanya? Ndiyo, Mueleze mteja ukweli kwa njia ambayo ni ya busara na hekima ili aelewe lengo lako. Hatakama hatokuelewa kwa wakati huo, usihofu, kadri muda unavyokwenda ataelewa hata kupitia mfanyabiashara mwingine mwenye msimamo kama wa kwako. Kumbuka uhai wa biashara yako ni muhimu kuliko mikopo ya wateja.
Je una swali au maoni yoyote kuhusu makala hii? Tafadhali andika hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii kwa kubofya kitufe cha mtandao wako wa kijamii.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
1
Hakika mteja anapotea akikopeshwa. Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Nahitaji kuwa mfanya biashara mzuri
Endelea kujifunza kupitia tovuti hii ili ufikie lengo lako. Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Gooood
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Habari za kazi na hongera kwa yote na elimu yenu nzuri mimi nimtu wakawaida nikweli tunakopa sana pesa za hawa watu ila tunakwama sehemu ndogo wakati wakurudisha ndio maana tunapata shida na hawa wakopeshaji(Aibu ukutanapo njiani chakujieleza hakuna) nasisi tunapenda kuwa na mitaji ili tuwalipe wanaotudai unakopa unajua nafanya kitu flani baadae unafeli ndo shida inapoanzia kwa sie wakopaji
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; na kwa kuwa msomaji wetu. Karibu sana Fahamuhili.com
nahitaji kuwa mfanya biashara mkubwa hasa upande wakuku unanishaurije
NI KWELI kikopesha kuna haribu mahusiano we we na mteja wako
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; na kwa kuwa msomaji wetu. Karibu sana Fahamuhili.com
Niliwahi funga biashara yangu kwa kukopesha watu ukienda kudai wanakuwa wakali kweli hapo nimejifunza kitu
Pole sana kwa changamoto hiyo. Asante sana kwa maoni yako ya thamani; na kwa kuwa msomaji wetu. Karibu sana Fahamuhili.com