Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamebadili maisha ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa. Sekta ya ajira nayo imepokea mabadiliko mengi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Hivi leo ni rahisi mtu kuishi Afrika akafanya kazi Marekani au mtu akaishi India akaajiriwa Tanzania. Haya yote ni kutokana na teknolojia kuwezesha watu kuajiri au kuajiriwa kwa kupitia njia ya mtandao wa intaneti.
Kwa kutambua kuwa kuajiri kwa njia ya mtandao ni njia nzuri ya kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni pamoja na kupata mtu mwenye sifa stahiki kwa kazi husika, basi fahamu mambo matano ya kuzingatia kabla ya kuajiri mtu kupitia mtandao.
1. Maarifa sahihi
Kuna wafanyakazi wengi kwenye mtandao wa intaneti, lakini siyo wote ni bora au wana maarifa stahiki. Ni muhimu sana kufanya utafiti wa kina juu ya maarifa unayoyahitaji kutoka kwa mtu unayetaka kumwajiri.
Unaweza kuzingatia haya:
- Tafiti kwa kina kiwango cha uwezo wake kwa kazi unayotaka afanye.
- Tazama kazi zake za awali alizozifanya ili uone ubora wake.
Ukizingatia haya utaweza kupata mtu mwenye maarifa stahiki kwa ajili ya kazi yako na siyo tapeli au mwanafunzi.
2. Vifaa stahiki
Kufanya kazi kwenye mtandao kunahitaji vifaa stahiki na bora kama vile kompyuta, mtandao wenye kasi nzuri, simu, n.k. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa mtu unayetaka kumwajiri anavifaa vyote vinavyohitajika kwenye kazi yako.
Unaweza kumpa kazi ya majaribio ili uone ubora wa vifaa vyake au ukamuuliza moja kwa moja akuambie vifaa alivyonavyo.
3. Uwezo mzuri wa mawasiliano
Mawasiliano ndiyo msingi mkuu wa kufanya kazi na mtu yeyote kwenye mtandao. Hakikisha lugha unayoielewa inaeleweka pia kwa mtu unayemwajiri, usiajiri mtu ambaye hamuwezi kuwasiliana vyema.
Kumbuka utahitaji kumpa maelezo kadha wa kadha kuhusu kazi, naye atahitaji kukuuliza masuala kadhaa kuhusu kazi husika.
4. Mrejesho wa waajiri wengine
Mifumo ya kufanya kazi kwenye mtandao huwa inaonyesha wafanyakazi bora zaidi kutokana na mrejesho wa waajiri wa awali. Hivyo ni muhimu kufuatilia mrejesho (reviews and responses) wa awali wa waajiri wengine juu ya ubora wa utendaji kazi wa mtu unayemwajiri.
Hata hivyo, unaweza kuajiri mtu yoyote kwa kuzingatia tu uchunguzi wa kina bila kutegemea sana mrejesho wa waajiri wa awali kwani wakati mwingine unaweza usiwe halisi.
5. Gharama
Hakikisha unaajiri mtu ambaye gharama zake unazimudu vyema. Wafanyakazi wengine wana gharama za juu sana huku wengine wakiwa na gharama ndogo sana.
Hata hivyo ni muhimu kutokudanganywa na wafanyakazi wa gharama ndogo sana kwani wanaweza kuwa na uwezo mdogo.
Soma pia: Njia 12 za Kupunguza Gharama za Uendeshaji wa Kampuni
Hitimisho
Pasipo shaka unaweza kuajiri watu kupitia mtandao na ukarahisisha kazi zako pamoja na kuokoa gharama nyingi za kuajiri mtu moja kwa moja kwenye ofisi yako. Lakini ni muhimu sana ufanye utafiti na ukaguzi wa kutosha kwa mtu unayetaka kumwajiri.
Kwa kufanya hivi utapata mtu bora atakayefanya kazi kwa ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu.
Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali andika maoni yako hapo chini. Unaweza kuwashirikisha wengine makala hii au kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.