Mbinu mojawapo ya kuongeza faida katika kampuni au biashara yako ni kwa kupunguza matumizi ya kampuni yako. Suala la kupunguza matumizi ya pesa ni muhimu zaidi hasa pale ambapo kampuni inakuwa inakabiliwa na changamoto za kifedha.
Kwa hakika kupunguza matumizi ya uendeshaji wa kampuni ni jambo linalowezekana ikiwa mikakati na hatua stahiki zitachukuliwa.
Ikiwa unapenda kufahamu jinsi ya kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni, basi fahamu njia 12 unazoweza kuzitumia kufanikisha lengo hili.
1. Tathimini upya matumizi
Kuna matumizi mbalimbali kwenye kila kampuni lakini siyo yote ni ya muhimu. Matumizi mengine ni ya lazima lakini yamepewa kipaumbele kuliko umuhimu wake.
Kwa kupunguza matumizi ya vitu kama vile simu, umeme, maji, mafuta au hata intaneti, kutaokoa kiasi kikubwa cha pesa.
Hakikisha huduma hizi zinatumiwa vyema tena kwa matumizi ya muhimu ya kampuni na si vinginevyo.
Soma pia: Njia 8 za Kuokoa Mafuta Unapoendesha Gari
2. Punguza gharama za uzalishaji
Uzalishaji wa bidhaa au utoaji wa huduma hugharimu pesa. Hata hivyo kuna mambo unayoweza kuyafanya ili kupunguza gharama za uzalishaji.
Kwa mfano kama unatumia vifungashio vya bidhaa vya bei kubwa, basi tumia vifungashio mbadala vya bei nafuu.
Inawezekana pia unatumia nishati ya umeme kufanya kila kitu, unaweza kutumia nishati mbadala kama vile umeme jua (solar) au gesi.
3. Ongeza matumizi ya teknolojia
Teknolojia ni muhimu sana kwa ajili ya kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni pamoja na kurahisisha utendaji kazi wa kampuni.
Ikiwa kampuni yako inatumia mawasiliano ya posta, fax, vikao vya kawaida pamoja na utunzaji wa kumbukumbu kwa njia ya karatasi, sasa ni wakati wa kuacha mifumo hiyo.
Matumizi ya barua pepe (email), mikutano kwa njia ya mtandao (online meetings), hazina pepe (cloud storages) kutapuguza gharama kubwa za uendeshaji wa kampuni.
4. Ajiri kupitia mtandao wa intaneti
Hivi leo kampuni nyingi huajiri wafanyakazi kwenye mtandao kwa lengo kubwa la kupunguza gharama za wafanyakazi.
Unapoajiri mtu kwenye mtandao, utamlipa malipo ya kazi husika pekee, lakini unapoajiri mtu moja kwa moja ofisini kwako utamlipa gharama mbalimbali kama vile mafao, bima, gharama za uhamisho, malipo ya likizo, n.k.
Unaweza kutumia tovuti mbalimbali kuajiri wafanyakazi kote duniani kadri upendavyo. Kwa mfano unaweza kutumia tovuti kama vile Upwork na Fiverr.
5. Uza vitu vya zamani
Je kampuni yako ina samani, vyombo, mashine, magari, au hata vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta za zamani?
Badala ya kuweka vifaa hivi viharibikie ghalani (store), unaweza kuviuza kama vifaa chakavu kwa bei nafuu na ukapata pesa ambazo zingepunguza gharama za uendeshaji wa kampuni yako.
6. Tafuta watoa huduma wa bei nafuu
Kuna watoa huduma tofauti na wenye gharama tofauti pia. Ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni unaweza kutafuta watoa huduma kama zile za simu, mtandao au hata wale wanaokuletea bidhaa mbalimbali ambao gharama zao ni nafuu.
7. Fanya biashara kwenye mtandao
Biashara kwa njia ya mtandao inaweza kuzalisha faida kubwa na kupunguza kiasi kikubwa cha gharama za uendeshaji wa kampuni ikiwa itafanywa jinsi ipasavyo.
Kwa kutumia tovuti, blog au mitandao ya kijamii unaweza kujitangaza na kuwafikia wateja wengi kwa urahisi zaidi kuliko njia ya kawaida.
Soma pia: Makosa 8 ya Kuepuka Unapofanya Biashara Kwenye Mtandao
8. Nunua vitu kwa ujumla
Kila mfanya biashara anafahamu wazi kuwa kununua vitu kidogokidogo ni hasara zaidi kwani kodi huwa kubwa na punguzo huwa dogo.
Ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni, ni muhimu kuzingatia kununua vitu kwa ujumla kuliko rejareja.
9. Tumia njia mbadala za matangazo
Zipo njia nyingi za kutangaza kampuni au biashara yako. Baadhi ya njia ni za gharama kubwa wakati nyingine ni rahisi na za bei nafuu.
Unaweza kutumia mitandao ya kijamii, tovuti, blog au hata vipeperushi ili kujitangaza; kwa njia hii utapunguza gharama za matangazo ya televisheni au redio.
Soma pia: Njia 9 za Kutangaza Biashara Yako Bila Pesa
10. Lipa madeni kwa wakati
Unapochelewa kulipa deni, hasa deni la taasisi za kifedha, husababisha riba kuongezeka. Jambo hili litakusababishia gharama na matumizi makubwa kwenye kampuni yako.
Ikiwa unatumia mikopo kuendesha kampuni yako, hakikisha mikopo hiyo inalipwa kwa wakati.
Soma pia: Sababu 13 za Kwa Nini Biashara Nyingi Hufa
11. Ruhusu likizo zisizokuwa na malipo
Likizo zisizokuwa na malipo hazimpi tu mfanyakazi faida ya kuwa na muda mrefu wa kutosha wa likizo, bali zinanufaisha pia kampuni kwa kuipunguzia gharama za malipo ya likizo.
Ikiwa kampuni yako haitopata shida kutoa muda mrefu wa likizo kwa wafanyakazi usiokuwa na malipo, basi ruhusu wafanyakazi waweze kuomba likizo za aina hii.
12. Punguza wafanyakazi
Njia hii siyo nzuri hasa kwenye maisha ya wafanyakazi, lakini wakati mwingine inabidi kutekelezwa.
Ikiwa kuna wafanyakazi ambao siyo lazima kuwa nao, au ambao majukumu yao yanaweza kufanywa na wafanyakazi wengine, basi wanaweza kupunguzwa ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni.
Hitimisho
Kwa hakika matumizi mazuri ya pesa pamoja na mipango endelevu ni mikakati muhimu itakayowezesha kupunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa. Ni muhimu kuhakikisha pesa zote zinazoingia kwenye matumizi ya kampuni zinaleta faida kwa kampuni husika.
Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kujiunga nasi kwa barua pepe au kwa kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
Naitwa abdallah mussa nataka kuanzisha biashara Ila watu ambao nawaomba ushauri wananivunja moyo ndomana nimeamua kutumia mtandao kupata msaada.
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Mawasiliano:
Email: fahamuhili[at]gmail.com
Simu: 0758 444 771
Vitu vipi vya kuzingatia katika uendeshaji kampuni