Mambo 9 ya Kuzingatia Wakati Wa Kuchagua Kampuni ya Matangazo Kwenye Blog - Fahamu Hili
Sunday, December 3Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 9 ya Kuzingatia Wakati Wa Kuchagua Kampuni ya Matangazo Kwenye Blog

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Matangazo

Kuweka matangazo kwenye blog ni njia mojawapo ya kupata pesa kupitia blog ambayo inafahamika kwa watu wengi. Kuna baadhi ya blog au tovuti ambazo zimefanikiwa kutengeneza pesa nyingi sana wakati nyingine zikiwa hazipati pesa za maana au hazipati kabisa kupitia njia hii ya matangazo.

Kwa hakika watu wengi huchagua njia ya kuweka matangazo ya kampuni mbalimbali kwenye blog zao ili kujipatia kipato kutokana na kutokufahamu njia nyingine za kupata pesa au kutokana na kuona blog nyingine zikitumia njia hiyo.

Ikiwa basi wewe ni mmojawapo wa watu wanaotaka kutumia njia ya kuweka matangazo kwenye blog ili kupata pesa, basi fahamu mambo 9 ya kuzingatia wakati wa kuchagua kampuni ya matangazo kwenye blog au tovuti yako.

1. Wakati sahihi

Kuna wakati sahihi wa kujiunga na kampuni ya matangazo kwenye blog yako. Ikiwa blog yako haisomwi (pageviews) mara 1,000 au zaidi kwa siku, ni vyema ukatafuta njia nyingine ya kupata pesa tofauti na matangazo.

Ili upate angalau kuanzia dola 1 kwa siku, ni muhimu sana uwe na kiasi cha kusowa kwa blog yako kinachozidi 1,000.

Badala ya kupoteza muda kuweka matangazo kwenye blog yako ambayo hayakulipi, bi bora ukaandaa maudhui bora ili uongeze wasomaji wako kwanza.

2. Fanya utafiti

Utafiti ni jambo muhimu sana kwenye kuchagua kampuni ya kutangaza matangazo kwenye blog yako. Hii ni kutokana na sababu kuwa kuna kampuni nyingi lakini siyo zote ni bora, hivyo ni vyema kuchunguza mambo yafuatayo:

  • Hakikisha ina vyanzo ya matangazo vya kutosha. Ukijiunga na kampuni isiyokuwa na matangazo ya kutosha haitaweza kuweka matangazo ya kutosha yatakayokupa faida.
  • Hakikisha siyo matapeli. Kumekuwa na tabia ya baadhi ya kampuni kutokomea na pesa za wamiliki wa blog, hivyo fanya uchunguzi kwa kusoma maoni ya watumiaji wengine.
  • Hakikisha wana miundombinu ya uhakika. Kampuni kama Google Adsense wana miundombinu ya uhakika inayoweza kuwahudumia wateja wake vyema.
  • Matangazo yanayoendana na eneo, wasomaji au hata maudhui yanayolengwa na blog yako. Kwa mfano kama blog yako inalenga Afrika, ukichagua kampuni ya matangazo ya Ulaya pekee hutopata pesa kwani hawana matangazo ya Afrika.

3. Ubora wa matangazo

Je unataka kila aina ya tangazo litokee kwenye tovuti yako? Kuna kampuni za matangazo zinazoweka matangazo ya hovyo yenye picha za uchi au hata nguo za ndani; matangazo mengine pia yanatumia teknolojia mbaya ambayo inaathiri utendaji kazi wa tovuti yako.

Kumbuka! Unapoweka matangazo kwenye blog yako, mara nyingi wasomaji wako wanaamini unahusiana nayo, hivyo ni muhimu kuhakikisha unaweka matangazo yanayoendana na blog yako.

Soma pia: Makosa 25 ya Kuepuka Unapotengeneza Tovuti (website) au Blog

4. Uwekaji wa matangazo

Kuna baadhi ya kampuni zinazolazimisha uweke tangazo lao eneo fulani kwenye blog yako au kutokuruhusu kuchanganya matangazo yao na ya kampuni nyingine. Hii ina maana kuwa utashindwa kutumia eneo hilo kwa kazi nyingine au kwa matangazo mengine.

Hakikisha unaelewa sheria ya uwekaji (ad placement) ya matangazo ya kampuni husika kabla ya kujiunga nao ili usije ukafungiwa au kupoteza pesa zako.

5. Mrejesho wa faida

Huwa ninaamini kuwa nikionyesha tangazo la kampuni fulani kwa wasomaji wangu mara 1,000 ni sawa na mimi kutembea mtaa kwa mtaa nikiwa nimebeba bango la bidhaa ya kampuni husika ili niwafikie watu 1,000.

Hivyo ni lazima nihakikishe gharama na nguvu niliyoitumia inarudi. Ni  muhimu kuhakikisha kampuni husika inakulipa kile unachostahili, kama umewatangazia bidhaa au tangazo lao vyema, basi uhakikishe nao wanakulipa vyema pia.

Baadhi ya kampuni huwanyonya wamiliki wa tovuti na blog, kumbuka blog nzuri huandaliwa kwa gharama, hivyo usikubali mtu akunyonye.

6. Matangazo wakati hakuna watangazaji

Kampuni kama Google Adsense haiwezi kuishiwa matangazo lakini kampuni ndogo ndogo huishiwa matangazo.

Kampuni bora hujiunga moja kwa moja na kampuni nyingine yenye matangazo ikiwa matangazo yao yamekwisha. Hivyo kwa njia hii hutoacha kupata pesa kwani kila mara kuna matangazo.

Ni vyema ukachunguza kama kampuni ya matangazo unayotaka kuichagua imejiunga na kampuni nyingine kubwa za matangazo.

Mara uonapo tangazo la kutangaza kampuni ya matangazo badala ya matangazo ya makapuni mbalimbali, fahamu kuwa kampuni hiyo haina matangazo kwa muda husika.

7. Vigezo vya malipo na njia ya malipo

Baadhi ya kampuni zina vigezo vizuri pamoja na njia nzuri zinazoeleweka za malipo.

Baadhi ya kampuni huruhusu kutoa pesa kuanzia dola 50 wakati nyingine huanzia dola 100; baadhi ya kampuni pia hutumia mifumo mbalimbali ya kimataifa ya kutuma na kutoa pesa hivyo kukurahisishia wewe kupata pesa zako.

Kwa mfano ukijiunga na kampuni inayotumia PayPal pekee kutoa pesa, ni wazi kuwa kama uko nchini Tanzania hutoweza kupata pesa zako kwani PayPal hairuhusu kutoa pesa nchini Tanzania. Hivyo ni muhimu kufanya utafiti wa kina.

8. Takwimu

adse
Ukurasa mkuu wa Adsense ukionyesha takwimu muhimu.

Kampuni zilizokomaa kama vile Google Adsense, hukupa takwimu kamili za matangazo yao uliyoweka kwenye blog yako. Kampuni bora nilazima ikuonyeshe taarifa kamili tena hata kwa wakati uliopo (real time), ili utathimini ufanisi wa matangazo uliyoweka.

9. Vigezo na masharti

Kila kampuni ina vigezo vyake vya kujiendesha. Ni muhimu kuchunguza na kuhakikisha unavimudu vigezo vya kampuni husika vyema.

Hii ni kutokana na baadhi ya kampuni kutaka mikataba ya siri au kuficha kanuni fulani kwenye mikataba yao na kupelekea wamiliki wa tovuti au blog kupoteza pesa zao pale wanapovunja kanuni hizo.

Hitimisho

Kwa hakika kuweka matangazo kwenye blog au tovuti yako kunaweza kuwa na manufaa makubwa kama kutafanywa jinsi ipasavyo; lakini ikiwa kutakosewa basi kunaweza kukuletea hasara na athari nyingi.

Ni muhimu kuzingatia pia njia nyingine za kupata kipato kwenye blog, kwani njia ya matangazo huwaondoa watembeleaji kwenye blog yako na kuwapeleka kwenye tovuti nyingine.

Soma pia: Njia 14 Halali za Kupata Pesa Kupitia Blog

Hata hivyo naamini ikiwa una lengo la kuweka matangazo kwenye blog yako, utazingatia mambo yaliyoelezwa hapa nawe utapata kampuni nzuri ya matangazo.

Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

4 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Ali A Porini
Ali A Porini
5 years ago

Je nawezaje kujiunga na Google Adsense kuweka vitabu vyangu vitangazwe na kusomwa?

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x