Mambo 8 ya Kuzingatia Wakati wa Kuchagua Eneo la Kufanyia Biashara - Fahamu Hili
Thursday, February 22Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 8 ya Kuzingatia Wakati wa Kuchagua Eneo la Kufanyia Biashara

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Je ni maeneo gani sahihi ya kufungua biashara ili uweze kupata wateja, kukuza biashara na kutengeneza faida. Je, kila eneo linafaa kwa biashara? Hivyo basi, ili tuweze kujibu maswali haya vyema, hatuna budi kuangalia mambo 8 muhimu ya kuzingatia wakati wakuchagua eneo la kufanyia biashara ili ipate soko na kukua kila wakati.

1. Ushindani

Ushindani ni jambo muhimu sana linaloweza kufanya eneo la biashara kuwa zuri au baya. Hebu fikiri mtu mchanga kabisa anaanzisha biashara mahali ambapo tayari kuna wafanyabiashara wengine wakubwa wenye uzoefu, mtaji, vitendeakazi au hata mtandao mzuri wa washirika. Bila shaka, itakuwa vigumu sana kwa mtu huyo kukua kibiashara. Ni lazima mtu apime na achague eneo amabalo lina ushindani ambao anaweza kuumudu na kukua.

2. Uhusiano kati ya biashara na eneo/mazingira

Mara nyingi biashara huhusiana na mazingira husika. Kwa mfano ni rahisi kufanikiwa kwenye biashara ya stationary kwenye maeneo ya vyuo, shule au taasisi kuliko nje ya mazingira hayo. Kwa mfano pia ni rahisi mtu kuendesha biashara ya vyinywaji na vitafunwa, vipodozi na simu kwenye kituo cha mabasi kuliko biashara ya nafaka au pembejeo. Hivyo ni muhimu kupima kama biashara yako itaendana na eneo husika unalotaka kulichagua.

3. Mtindo wa maisha katika eneo husika

Kila eneo lina mtindo wake wa maisha. Itakuwa jambo la kusikitisha sana wewe kufungua biashara ambayo bidhaa yake ndogo kabisa ni shilingi 100,000 na wakati nguvu ya ununuzi ya watu wa eneo husika ni 1,000.

Ngoja nikupe mfano rahisi zaidi, kwa mfano watu waliozoea kununua mafuta ya mia tano, unga robo na sabuni kipande, ukifungua supermarket katika eneo hilo ni wazi kuwa utakosa wateja hatakama unauza bidhaa nzuri kiasi gani.

4. Wingi wa waakazi

Wingi wa watu katika eneo husika ni sawa sawa na mauzo zaidi au kuonekana zaidi kwa biashara yako. Haijalishi eneo lina fremu nzuri au za gharama nafuu kiasi gani, kama halina wakaazi wa kutosha litakuchelewesha sana kufikia malengo yako.

Ikiwa ni eneo ambalo watu wanahamia kwa kasi kubwa kwa kipimo kuwa ndani ya muda mfupi utakuwa na wateja wengi basi hapo unaweza kuvumilia; lakini kama eneo ndivyo lilivyo nyumba moja ipo baada ya mita 500 basi hilo halikufai.

5. Miundombinu na huduma za kijamii

Unapoangalia eneo la kufanyia biashara ni zaidi ya kile chumba au nyumba unayoichagua kuitumia kama ofisi yako. Itakuwa si jambo la busara kuendesha biashara inayohitaji maji au umeme wa kutosha mahali ambapo hakuna huduma hizo. Pima hili mapema lisije likakusababishia changamoto au gharama kubwa za uendeshaji zisizokuwa na ulazima.

Hakikisha pia eneo hilo linafikika katika vipindi vyote vya mwaka. Kwa mfano itakuwa nijambo la ajabu mtu kufungua biashara ya kuuza gesi kwenye eneo ambalo liko uchochoroni; kiasi kwamba hata yale magari ya gesi hayawezi kufika au hata wateja wake wanamfikia kwa taabu. Hivyo, fanya tathimini ya miundombinu kwa kina.

6. Usalama na majirani

Usalama ni nguzo muhimu sana katika kujenga mazingira mazuri ya kibiashara.  Hakuna mteja atakayependa kuja kwenye biashara ambayo atajihisi kutokuwa salama. Mfanyabiasha naye hawezi kufanikiwa ikiwa anafanya biashara kwenye mazingira ambayo siyo salama kwake na mali zake.

Hakikisha pia mazingira yanayokuzunguka, majirani pamoja na biashara za jirani hazitaathiri biashara yako. Kwa mfano siyo biashara zote zinaweza kufanywa karibu na biashara kama vile baa, karakana ya ufundi n.k. Nimeshuhudia watu wakiacha fremu zao kutokana na kuzungukwa na majirani wabaya; nimeshuhudia watu wakigomeana kulipa luku, maji n.k. hadi kufikia kuziacha biashara zao. Hivyo tafakari sana kabla ya kuchagua eneo la biashara.

7. Uhusiano kati ya gharama za uendeshaji na eneo husika

Haijalishi eneo la biashara ni zuri au umelipenda kwa kiasi gani, ni lazima ulinganishe kama gharama za uendeshaji zinazotokana na kufanya biashra kwenye eneo husika zitalipa. Inawezekana umekutana na mwenye nyumba anayepangisha fremu yake nzuri sana kwa shilingi 500,000 kwa mwezi, kumbe ni ili alipe mkopo wake wa bank; lakini katika uhalisia biashra katika eneo hilo haiwezi kufikisha mauzo ya 50,000 kwa siku.

Ukidanganyika kwa  mazingira hapa bila kupima uhusiano wake na gharama za uendeshaji utakuwa na wakati mgumu sana.

8. Mahitaji ya kipekee ya biashara husika ya sasa na baadaye

Suala hili hupuuziwa sana na watu wengi wanapotaka kuanzisha biashara, lakini huwaletea changamoto kubwa. Ni muhimu sana ufahamu biashara yako ina mahitaji gani ya kipekee ya sasa na baadae. Kwa mfano, ikiwa biashara yako itahusisha upokeaji na upakuaji wa mizigo au hata kuhudumia wateja wengi wenye magari ni lazima uhakikishe eneo unalolichagua litamudu mahitaji hayo. Jiulize maswali je biashara yangu inataka mazingira ya aina gani? Je ofisi na eneo nililolichagua litakidhi mahitaji hayo sasa na baadaye? Baada ya kupata jibu fanya maamuzi.

Hadi kufikia hapa naamini umefahamu wazi kuwa ni mambo gani unayopaswa kuyazingatia wakati wa kuchagua eneo la kufanyia biashara ili uweze kupata wateja, kukuza biashara na hata kutengeneza faida kutokana na biashara yako. Kamwe usichague eneo labiashara kwa kufuata mkumbo. Kumbuka! Kupata soko zuri la biashara yako kunachangiwa sana na uchaguzi wa eneo la biashara.

Soma pia: Mambo 5 ya Kuzingatia Kabla ya Kuchagua Wazo la Biashara

Je una swali au maoni yoyote kuhusu makala hii? Tafadhali andika hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii kwa kubofya kitufe cha mtandao wako wa kijamii.

3.9 17 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Khadija
Khadija
3 years ago

Good

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x