Sababu 13 za Kwa Nini Biashara Nyingi Hufa - Fahamu Hili
Saturday, April 20Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Sababu 13 za Kwa Nini Biashara Nyingi Hufa

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Biashara iliyokufa

Hakuna mtu anayeanzisha biashara akitegemea ife, lakini wakati mwingine hili hutokea. Utafiti umebaini kuwa biashara na kampuni nyingi hufa ndani ya kipindi cha miaka miwili hadi mitano tangu kuanzishwa kwake.

Kufa kwa biashara siyo jambo zuri, ni wazi kuwa kila mtu nayefanya biashara atatamani kufanya juu chini ili ainusuru biashara yake isife.

Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha biashara mbalimbali kufa. Fahamu sababu 13 zinazosababisha biashara nyingi kufa pamoja na jinsi ya kuziepuka.

1. Mipango duni

Ili ufanikiwe katika biashara unahitaji mpango mzuri wa biashara. Biashara nyingi zinazoanzishwa Afrika hazina mipango madhubuti ya kibiashara inayoonyesha maswala kama vile muundo wa utawala, mtaji, mikakati au mipango ya mauzo, n.k Biashara nyingi pia hukosa lengo; jambo ambalo hufanya biashara nyingi kufa.

Soma: Mambo 7 ya Kufanya Kabla ya Kuanzisha Kampuni au Biashara.

2. Uongozi na usimamizi mbaya

Kufanikiwa kwa biashara kunategemea usimamizi mzuri. Uwekaji wa mipango na kuisimamia ili itimie hufanywa na uongozi mzuri. Ni wazi pia rasilimali nyingi za kampuni zitapotea kutokana na kukosa uongozi na usimamizi mzuri. Biashara nyingi za Afrika huendeshwa kwa mazoea au kuendeshwa na watu wenye uwezo mdogo katika utawala.

Soma pia: Sifa 10 Zitakazokufanya Kuwa Kiongozi Bora.

3. Kupuuza wateja na mahitaji yao

Naamini unafahamu msemo usemao kuwa “Mteja ni mfalme”. Biashara nyingi za kiafrika hufa kutokana na kupuuza wateja pamoja na mahitaji yao. Unaweza kuona mfanyabiashara anamjibu mteja vibaya au hamkaribishi kwa furaha bila sababu yoyote ya msingi. Wakati mwingine wafanyabiashara hawasikilizi maoni na mahitaji ya wateja jinsi ipasavyo. Mfanyabiashara kujihisi kuwa yeye ndiyo mwenye faida kwa mteja ni kosa kubwa litakalogarimu biashara yake.

4. Kutokujifunza kutokana na makosa

Makosa ni shule muhimu inayotuwezesha kuboresha viwango vya utendaji. Ni wazi kuwa yapo makosa yanayofanyika mara kwa mara kwenye uendeshaji wa biashara. Wakati mwingine makosa haya huleta athari mbaya kwa biashara. Wafanyabiashara wengi hawapendi kujifunza kutokana na makosa haya ili wayaepuke mbeleni; hivyo yanapotokea tena huwakuta hawajajiandaa vyema.

5. Kujipanua bila mipango

Upanuzi wa biashara ni jambo linalohitaji mipango madhubuti. Kuongeza ukubwa wa biashara kunahitaji kutazama mambo kama vile mtaji, watumishi, vitendeakazi, uendeshaji na usimamizi, masoko n.k. Biashara nyingi hujipanua bila kutazama mambo haya; jambo ambalo linapelekea biashara nyingi kufa.

Soma pia: Makosa 15 Ambayo Kila Mjasiriamali Anatakiwa Kuyaepuka.

6. Eneo baya la kibiashara

Uchaguzi mbaya wa eneo la kibiashara hupelekea biashara nyingi kufa kutokana na kukosa wateja. Biashara nyingi hushindwa kubainisha eneo ambalo linafaa kwa ajili ya biashara zao na hatimaye hukosa wateja na kufa. Kwa mfano kufungua biashara ya kuuza vifaa vya magari katikati ya soko la vyakula ni wazi kuwa mauzo yatakuwa duni sana.

7. Kukosa faida

Biashara ni lazima iwe na faida ili isife. Kama biashara inauza bidhaa za shilingi 10,000 ni lazima pia ipate zaidi ya 10,000 katika mauzo yake. Wafanyabiashara wengi hujifariji kuwa kufanya biashara bila faida ni jambo la kawaida. Ni kweli swala hili linaweza kutokea lakini lisiwe ni swala la mazoea. Ni muhimu kuhakikisha biashara inatengeneza faida ili iweze kujiendesha vyema.

8. Usimamizi mbaya wa fedha

Usimamizi wa fedha ni tatizo kubwa linaloua biashara nyingi. Hili linatokana na maarifa duni ya utunzaji wa pesa pamoja na tabia ya baadhi ya watumishi kukosa uaminifu katika swala la kusimamia na kutunza pesa. Watu hawajui kutunza pesa zao binafsi, hivyo hata wanapokabidhiwa pesa za biashara huzitumia hovyo hovyo.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema.

9. Washirika wabaya wa kibiashara

Mshirika mzuri wa kibiashara ni yule anayeweza kukuunga mkono katika maono na malengo yako ya kibiashara. Biashara nyingi hufanya kazi na washirika wabaya wasioweza kuendeleza maono na malengo ya biashara husika; hili husababisha biashara nyingi kukwama kwa kukosa ushirikiano stahiki.

10. Mambo yasiyo ya kiuchumi

Kuna mambo yanayoweza kuua biashara ambayo mengi siyo ya kiuchumi na mara nyingi hayazuiliki. Maswala kama vile majanga ya asili (mafuriko, ukame, tetemeko n.k), mabadiliko ya hali ya uchumi wa nchi na dunia, sera mbovu za kisiasa, vita, n.k. Ni baadhi ya mambo ambayo yanaweza kusababisha biashara kufa. Pamoja na hali hii biashara mbalimbali zinaweza kuweka mipango mapema ya kujiokoa katika hali hizi kama vile kuhakikisha uwepo wa akiba ya kutosha ya rasilimali hasa fedha.

11. Mbinu duni za masoko

Masoko ni taaluma rasmi inayofanywa na watu waliofuzu vyema. Ni tatizo kubwa sana kupuuza swala la masoko. Biashara nyingi hazifahamu jinsi ya kutafuta na kutawala soko, hivyo hujikuta wakipoteza soko la bidhaa zao na hatimaye kufa kwa kukosa mapato. Ni muhimu kujifunza mbinu sahihi za masoko kulingana na bidhaa na wakati husika.

12. Kuajiri watumishi duni

Biashara nyingi hupendelea watumishi duni (cheap labour) ili wawalipe malipo kidogo. Ni ukweli usiopingika kuwa mtumishi duni atafanya kazi duni. Biashara nyingi hazioni mafanikio wala matokeo chanya, kutokana na kuajiri watu wasiokuwa na uwezo wala ubunifu wa kufanya biashara husika kwa njia yenye tija. Ni heri kuajiri mtumishi mmoja bora kuliko watano duni.

13. Matatizo ya kisheria

Kuna wakati biashara au kampuni huingia kwenye matatizo ya kisheria yanayoigharimu biashara au kampuni husika fedha nyingi. Migogoro na matatizo haya yanaweza hata kupelekea kufilisiwa kwa biashara husika. Kwa mfano kampuni ya Shell ilikumbana na kesi mbalilimbali ikiwemo ya uchafuzi wa mazingira iliyoigarimu zaidi ya  dola za kimarekani 291,000.  Kesi hizi zimeiathiri Shell kwa kiasi kikubwa hadi kufunga vituo vyake sehemu mbalimbali duniani. Ni muhimu kuzingatia sheria katika ufanyaji wa biashara ili kuepuka kutumbukia kwenye matatizo kama haya.

Hitimisho

Zilizoelewa hapa ni sabau 13 za kwanini biashara nyingi hufa. Ni matumaini yangu kuwa sasa umefahamu makosa ambayo kama utayaepuka kwenye biashara, basi biashara yako inaweza kudumu na kuwa na tija zaidi. Mipango, sera na usimamizi madhubuti ni msingi muhimu katika kufanikiwa kwa biashara yoyote.

Je unafahamu sababu nyingine au una swali au maoni? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

4.8 6 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

4 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Abel Dominick
Abel Dominick
4 years ago

Nahitaji mafunzo zaidi ya kibiashara maana ni mfanyabiashara mwenye mtaji wa kawaida tu. Ila nataka niukuze

Prince mnyimbi
Prince mnyimbi
3 years ago

NIMEPENDA SANA MUONGOZO WAKO KWA KWELI MUONGOZO WAKO UMENIFANYA NIPIGE HATUWA KUBWA NA KUPATA MAFANIKIE, PIA NAOMBA MAWASILIANO YAKO ILI NIPATE FURA YAKUBADILISHANA MAWAZO NA WEWE

4
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x