Mara nyingi tunanunua vitu na bidhaa mbalimbali bila kuzifahamu au kuzichunguza vyema. Hili limepelekea watu wengi kununua bidhaa zisizofaa kwao au zenye madhara kwenye afya zao. Kutokana na ukosefu wa elimu pamoja na kuishi kwa mazoea, watu wengi hawajui wala hawachunguzi vyema bidhaa wanazozinunua ili kuhakikisha ubora wake.
Madhara ya kutumia bidhaa feki au bandia:
- Matatizo ya kiafya kama vile saratani na ulemavu.
- Upotevu wa fedha.
- Ajali (Milipuko, shoti ya umeme, n.k).
- Huathiri uchumi.
Ni wazi kuwa yapo madhara mengi yatokanayo na matumizi ya bidhaa feki. Hivyo ni vyema ukafahamu njia za kubaini bidhaa hizi.
1. Ofa na matangazo yasiyo ya kawaida
Wahenga walisema “Chema chajiuza kibaya chajitembeza”; ni vyema ukawa makini na bidhaa zenye punguzo kubwa la bei kuliko kawaida, kwani mara nyingi bei hupungua sana kutokana na ubora duni. Pia ni vyema ukaepuka kuvutiwa na maneno ya kibiashara kama vile “Oringinal” “…Colection”, “King size”, “Royal”, “genuine,” “real,”, “authentic”, “Mpya”, “Kali” n.k Kumbuka simaanishi usinunue bidhaa yenye punguzo au maneno haya bali yasiwe ndiyo yanatawala au kutumiwa kama mbinu ya mauzo.

2. Fahamu bidhaa yako
Ni vyema ukaichunguza na kuifahamu bidhaa ambayo unainunua au kuitumia mara kwa mara. Hili litakuwezesha kubaini bidhaa ambayo ni feki au bandia kwa urahisi zaidi. Chunguza na bainisha vitu vya msingi ambavyo ni lazima viwepo kwenye bidhaa husika. Hivyo kabla ya kununua bidhaa hakikisha inafanana na ile uliyoizoea; kama hujawahi kuinunua unaweza kumwomba mtu anayeifahamu vyema akusaidie kuikagua.

3. Kagua vifungashio kwa makini
Kubaini bidhaa feki au bandia kunahitaji utulivu, chukua muda kukagua vifungashio vya bidhaa husika kwa makini. Hili litakuwezesha kubaini kukosekana kwa taarifa muhimu kama vile jina la mtengenezaji, mahali pa utengenezaji, tarehe ya kuzalishwa na ya mwisho wa matumizi pamoja na taarifa nyingine muhimu. Ni wazi kuwa bidhaa iliyokosa taarifa muhimu inaweza kuwa bandia au yenye ubora duni.
4. Hakikisha kila kilichotakiwa kuwepo kipo

Mara nyingi unaweza kununua kifaa au bidhaa yenye kitu zaidi ya kimoja. Kwa mfano, ikiwa unanunua simu au kamera hakikisha kama huwa inauzwa pamoja na vifaa kama vile betri, chaja, kadi ya kumbukumbu (memory card), waya wa USB n.k vipo vyote tena kwenye hali nzuri. Mara nyingi bidhaa feki hukosa badhi ya vifaa muhimu ambavyo kwa kawaida huwepo kwenye vifaa au bidhaa halisi.
5. Uliza kuhusu Warranty (Garantii)
Warranty (Garantii) ni mkataba maalumu baina ya mnunuzi na mtengenezaji wa bidhaa husika. Warranty (Garantii) hukuwezesha kutengenezewa au kubadilishiwa bidhaa husika ikiwa itapata matatizo ndani ya muda fulani. Bidhaa bandia au feki kamwe huwa hazitoi Warranty (Garantii); na zikitoa basi ni feki pia. Hivyo ni vyema ukatazama kama bidhaa husika (Hasa vifaa vya kielektroniki) zina Warranty (Garantii) ya uhakika.
6. Tembelea tovuti ya mzalishaji
Hivi sasa karibu kila kampuni imejitahidi kufungua tovuti kwa ajili ya kuwafikia wateja wake kwa urahisi zaidi. Pia kampuni nyingi zimekuwa zikijitahidi kuwawezesha wateja wake kubaini bidhaa feki. Wakati mwingine, baadhi ya bidhaa huwekwa namba ambazo unaweza kuziingiza kwenye tovuti yao na kuona kama bidhaa ni bandia au laa. Hivyo, unaweza pia kutumia njia hii ili kubaini na kuepuka bidhaa feki.

7. Nunua kutoka kwa wakala aliyeidhinishwa
Ili kurahisisha na kuhakikisha ubora wa huduma, kampuni nyingi zimekuwa zikisajili mawakala kwenye maeneo mbalimbali. Unaponunua bidhaa kutoka kwa wakala aliyeidhinishwa, ni rahisi zaidi kupata bidhaa halisi; pia upatapo tatizo utapata msaada kwa urahisi zaidi. Kwa mfano, ikiwa unataka kununua simu ya Nokia au Sumsung, basi tafuta wakala aliyeidhinishwa na Nokia au Sumsung katika eneo lako.
8. Epuka bidhaa na vifaa vilivyoigwa
Hivi leo unaweza kuona simu inayoitwa NOKLA, lakini ukiitazama kila kitu kinafanana na simu ya NOKIA N97. Kwanini kama watengenezaji wa simu hii wanalengo zuri wasibuni muundo wao wenyewe? Ni dhahiri kuwa wanataka kuwadanganya na kuwachanganya wanunuzi; huko kubadili jina na kuiita NOKLA ni mbinu tu ya kukwepa mkono wa sheria. Ni wazi kuwa bidhaa hizi ni feki, hivyo yakupasa kuziepuka.

Hitimisho
Bidhaa feki zinaongezeka sokoni kila siku, ni vyema ukajifunza kukagua bidhaa vyema kabla hujainunua ili kuepuka madhara yatokanayo na bidhaa feki. Ni wazi kuwa kubaini bidhaa hizi kunahitaji utulivu, umakini na hata uchunguzi wa kutosha.
Naamini una maoni au maswali kuhusiana na makala hii, tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza pia kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
Asante kwa ushauri tutafanyia kazi
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; na kwa kuwa msomaji wetu. Karibu sana Fahamuhili.com