Fahamu Njia 6 za Kulinda Akaunti Zako za Mitandao ya Kijamii - Fahamu Hili
Thursday, February 22Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Fahamu Njia 6 za Kulinda Akaunti Zako za Mitandao ya Kijamii

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Usalama wa Mitandao ya Kijamii

Mitandao ya kijamii ni kitu muhimu sana kwenye maisha binafsi na shughuli za kiuchumi kama vile biashara. Kutokana na umuhimu huu, kuna haja ya kuhakikisha akaunti zako za mitandao ya kijamii zinakuwa salama.

Je ulishawahi kufikiri nini kitatokea ikiwa mtu mbaya atapata nafasi ya kuingia kwenye akaunti zako? Ni wazi kuwa mambo kama haya hapa chini yanaweza kutokea:

  • Kuiba wafuasi wako utakaokuwa umewakusanya muda mrefu.
  • Kutapeli watu mbalimbali wanaokufahamu katika mitandao ya kijamii kwa kutumia akaunti yako.
  • Kuchafua taswira yako; kumbuka mtu mbaya anaweza kuweka maudhui mabaya yatakayoshusha hadhi yako.
  • Kuiba ama kutumia vibaya taarifa zako binafsi zilizoko kwenye akaunti yako.

Ni wazi kuwa ipo sababu ya kuhakikisha akaunti zako za mitandao ya kijamii zinakuwa salama. Fuatilia njia 6 za kuhakikisha akaunti zako ziko salama.

1. Kuwa makini na programu za nje (third-party applications)

Hivi leo zipo programu nyingi ambazo zinaweza kuruhusiwa kuingia kwenye akaunti zako za mitandao ya kijamii. Programu hizi huweza kuchapisha au kutumia taarifa mbalimbali zilizoko kwenye akaunti yako.

Wengi hutumia programu hizi kutengeneza vitu kama vile “Maana ya jina lako” “Raisi anasema nini kukuhusu”, “Role model wako ni” n.k; lakini ukumbuke kuwa siyo programu zote hizi ni salama, nyingine ni za wadukuzi hivyo kuwa makini.

2. Tumia nywila (password) imara

Watu wengi hudukuliwa kutokana na kutumia nywila dhaifu. Wengi hutumia miaka ya kuzaliwa, majina ya utani au ndugu, majina ya maeneo n.k. Ni muhimu ukajifunza kutengeneza nywila imara ili kuhakikisha kuwa akaunti zako ziko salama. Kumbuka nywila ni ufunguo wa kulinda akaunti zako.

Soma pia: Mambo 8 ya Kufanya ili Kuwa na Nywila (password) Imara na Salama.

3. Tumia kinga-virusi (antivirus) bora

Kinga-virusi hukuwezesha kukulinda na wadukuzi au programu hatari ambazo zingeweza kuiba taarifa zako za siri na kusababisha kudukuliwa kwa akaunti zako. Hakikisha unatumia kinga-virusi katika vifaa vyako vyote kwani kuna kinga virusi karibu kwa kila aina ya kifaa.

Soma pia: Usalama wa Msingi wa Kompyuta: Jinsi ya Kujilinda na Virusi, Wadukuzi na Wezi.

4. Wezesha muidhinisho mara mbili (two factor authentication)

Kwa njia hii utaifanya akaunti yako kuwa salama zaidi kwani itahitajika mtu kuwa na nywila pamoja na maandishi yaliyotumwa kwako kwa simu au barua pepe ili kuingia kwenye akaunti yako.

Hivyo si rahisi kwa mtu mbaya kuvipata vyote viwili ili aweze kuingia kwenye akaunti yako; unaweza kutazama miongozo ya kuwezesha mudhinisho mara mbili hapa Facebook, Twitter, LinkedIn na Instagram.

5. Zinagatia vifaa unavyovitumia

Ikiwa utatumia akaunti zako za mitandao ya kijamii kwenye tarakilishi za uma au vifaa vya mtu mwingine, hakikisha unatoka kwenye akaunti zako kabla ya kuondoka ili kuhakikisha hautoi mwanya kwa mtu mwingine kuingilia akaunti zako.

Pia ni muhimu kutokupendelea kuacha akaunti zako wazi kwani lolote linaweza kutokea hata kama kifaa kilichotumika ni cha kwako; je ulishawahi kufikiri ukipoteza simu itakuwaje wakati akaunti zako ziko wazi? Chukua hatua ya kujilinda sasa.

6. Tawala mpangilio wako wa faragha (privacy settings)

Kupitia mpangilo wa faragha wa akaunti zako za mitandao ya kijamii unaweza kutawala mambo kama vile nani anaweza kufanya nini au kuona nini kwenye akaunti zako. Kwa kuzingatia hili utaweza kuzuia watu kufanya vitu usivyovitaka kwenye akanti zako; pia utaweza kuzia watu wasiohusika kuona mambo yako.

Hitimisho:

Naamini ukizingatia maswala haya kwa makini utaweza kulinda akaunti zako za mitandao ya kijamii. Kumbuka usalama ni muhimu sana katika huduma za mtandao; jambo unaloliona dogo linaweza kukuathiri kuliko jinsi unavyo fikiri. Chukua hatua sasa, usitoe mwanya kwa wahalifu kuingilia akaunti zako kwa sababu tu hukuchukua hatua za kiusalama mapema.

Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha usisahau kutufuatilia kupitia Fecebook pamoja na kuwashirikisha wengine makala hii.

3.3 4 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x