Watu wengi hufikiri kuwa usalama wa kompyuta ni swala gumu lenye changamoto kubwa. Inaweza kuwa hivyo kama hukuchukua hatua sahihi mapema. Katika makala hii utafahamu hatua tano muhimu ambazo zitakuwezesha kujilinda na virusi, wadukuzi na wezi katika kifaa chako cha kielektroniki.
1. Wezesha automatiki sasishi (automatic updates)
Programu mbalimbali za kompyuta hutoa masasisho (updates) mara kwa mara ili kuziba mianya mbalimbali hasa ya kiusalama iliyobainika katika matoleo ya awali. Program kama Microsoft Window, Mozilla na Chrome ni baadhi ya programu muhimu zinazohitajika kusasishwa kwa wakati.
Hivi leo programu mbalimbali huja na usasishaji wa automatiki lakini watu wengi hupenda kuuzima usasishaji huu bila kuzingatia umuhimu wake wa kiusalama. Hivyo basi, ili kuwa salama zingatia masasisho ya programu zako kwa wakati.
2. Tumia programu ya kukinga virusi na malware
Watu wengi wamekuwa wakipuuza utumizi wa programu hizi bila kujali umuhimu wake au kutokana na kukwepa gharama wengi hawazitumii.
Ili kuimarisha usalama wa kompyuta au kifaa chako hakikisha unatumia programu madhubuti kama vile Kaspersky, Bitdefender au Malwarebyte. Kama unashindwa kumudu gharama basi unaweza kutumia toleo la karibuni la window defender au baadhi ya kinga virusi (antivirus) za bure zinazoaminika.
3. Tengeneza na tumia Nywila (password) imara
Nywila ni kama ufunguo wako katika sehemu mbalimbali katika vifaa vyako vya kielektroni ikiwemo akaunti zako za mtandao. Hivyo kama ilivyo kwa ufunguo wa nyumba au offisi ndivyo inavyotakiwa pia kulinda nywila zako.
Mambo ya kuzingatia kuhusu nywila
- Tengeneza nywila imara isiyorahisi kubuniwa (usitumie mwaka wa kuzaliwa wala majina rahisi kubuniwa).
- Usimpe mtu mingine nywila yako.
- Usitume nywila moja kila mahali.
- Badili nywila yako kila baada ya kipindi fulani cha muda.
Kama utazingatia hili itakuwa ni vigumu kwa mdukuzi au mwizi kuingilia vifaa au akaunti zako.
Soma pia: Mambo 8 ya Kufanya ili Kuwa na Nywila (password) Imara na Salama.
4. Kuwa makini na viunganishi unavyo bofya mtandaoni
Ni jambo la kawaida kupokea barua pepe yenye viunganishi mbalimbali. Mara nyingine tunapokea barua pepe zenye viunganishi zilizotoka kwa watu mbalimbali hata tusiowajua.
Jihadhari na viunganishi unavyovibofya kwani vingine vinaweza vikawa vimetoka kwa watu wasiokuwa na nia njema au vimeambatanishwa na virusi au programu za kidukuzi.
Fungua tu viunganishi unavyovielewa vyema na hakikisha vina kitu cha kufaa kabla hujavifungua ili kuepuka kuibiwa taarifa zako muhimu.
5. Usiamini kila kitaarifu popu (Pop notification)
Mara nyingi umewahi kuona kitaarifu popu kikitokea unapotembelea tovuti fulani. Vitaarifu hivi hukutaka kusasisha ama kuweka flash player au kikikuambia kuna virusi kwenye kifaa chako. Katu usiviamini hivi kwani mara nyingi hutumika kudanganya watu ili waingize program fulani kwenye vifaa vyao ambazo zinaweza kuwa chanzo cha virusi au kudukulia.
Unapoona vitaarifu kama hivi kagua kifaa chako wewe mwenyewe kwa kutumia programu yako ya kukinga virusi au sasisha porgramu zako kwa kufuata utaratibu uliozoeleka.
Hitimisho
Zilizoelezwa hapa ni baadhi ya njia ambazo ukizifuata utaweza kuimarisha ama kuongeza usalama wa kompyuta ama kifaa chako. Naamini kuyafanya haya hakuhitaji utaalamu wa hali ya juu bali ni maamuzi na muda wako tu.
Je umesaidika kwa makala hii au una swali au mchango wowote? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini. Pia usisahau kuwashirikisha na wengine makala hii. Ili kufahamu mengi zaidi unaweza kufuatilia ukurasa wetu wa Facebook.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.