Kuna taarifa nyingi tunazoweka kwenye mtandao; lakini je, sasa ni wakati wa kuweka mipaka juu ya ni lipi la kuweka na kutoweka kwenye mitandao? Ndiyo; huu ni wakati sahihi. Hivyo basi, tambua vitu 11 ambavyo haupaswi kuviweka kwenye mitandao ya kijamii.
1. Tarehe kamili ya kuzaliwa
Wakati mwingine unaweza kuvutiwa na namna marafiki zako wanavyoweka taarifa za kuzaliwa kwenye mtandao, au hata misisitizo ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook juu ya kukamilisha akaunti yako kwa kuweka tarehe ya kuzaliwa.
Kuweka tarehe halisi au kamili ya kuzaliwa kwenye mitandao ya kijamii kunaweza kutoa mwanya kwa wahalifu kupata taarifa zako muhimu na hata kufungua au kuingilia akaunti zako zinazotumia tarehe yako ya kuzaliwa.
Mambo ya kufanya:
- Ficha au ondoa tarehe yako halisi ya kuzaliwa
- Unaweza kuweka taarifa halisi nusu badala ya kuweka taarifa zote kamili. Mf. Kama umezaliwa 20/10/1990 ukaweka tarehe 20/10/1970 au 20/05/1820, n.k.
2. Eneo ulipo kwa wakati husika
Kuna uwezekano unapoweka chapisho (post) mtandaoni likaonyesha pia eneo ulilopo; hii linategemeana na mpangilio wako wa faragha. Pia watu wenyewe wamekuwa wakionyesha wako maeneo gani katika machapisho (post) zao mbalimbali.
Hiki si kitu kizuri kwani kinawajulisha watu wabaya ulipo; hivyo wanaweza kwenda kukuibia nyumbani, au ofisini au hata kukuteka kwani wanajua eneo ulilopo.
Hivyo ni vyema kubadili mpangilio wako wa faragana (privacy settings), pia kutokuchapisha eneo ulilopo kwa ajili ya usalama wako.
3. Picha za watoto wako au wa jirani
Watu wengi hupenda kuweka picha za watoto kwenye mitandao tena wakiwatagi hata majina. Kwa hakika huwezi kujua ni nani ataziona hizo picha na atazitumiaje.
Ulishiwahi kufikiri kama akaunti ya rafiki yako itaibiwa na mtu mbaya ni nini kinaweza kutokea? Piacha unazoziona leo zikitumika katika matangazo, hata yale mabaya si zote zimenunuliwa; nyingine zimechukuliwa tu kwenye mitandao.
Je ungependa picha za mtoto wako au wa jirani zitumike vibaya? Kama hupendi zitumike vibaya, basi ondoa picha za watoto kwenye mitandao, au kama utaweka basi hakuna haja ya kuwatagi majina.
4. Anwani ya mahali unapoishi
Kama ilivyo kwa eneo ulipo kwa wakati husika, si vyema kuonyesha anwani kamili ya mahali unapoishi.
Je unajua akaunti yako itaonwa na nani? Inawezekana wahalifu wakakufwatilia kwa kutumia taarifa ulizoweka kwenye akaunti yako. Hatari huzidi kwa wale watu wanaopenda kuonyesha wanaishi maisha ya kifahari nyumbani wakiwa na vitu vya thamani kubwa vinavyovutia wezi.
5. Namba yako ya simu
Kama nilivyotangulia kusema katika dondoo zilizotangulia kuwa huwezi kujua taarifa zako zinaonwa na kutumiwa na nani. Epuka kuweka namba yako ya simu kwenye mitandao kwani inaweza kutumia na watu wabaya kufanya uhalifu au hata kukufwatilia.
Je ulishawahi kufikiri nini kitatokea ikiwa wezi watamwibia mtu pesa kwa kutumia namba inayofanana na ya kwako? Ni wazi kuwa utafikishwa katika mikono ya sheria kwani namba yako imetumika katika tukio la uhalfu.
6. Mahusiano
Watu wengi hupenda kuonyesha hali za mahusiano yako kwenye mitandao ya kijamii. Hebu fikiri umeonyesha kuwa uko kwenye mahusiano na mtu ambaye amemwacha mpenzi wake; ni dhahiri kuwa kuna uwezekano huyo mpenzi wa awali akataka kufanya kitu kibaya juu yenu.
Hivyo epuka kuweka maswala yako ya mahusiano kwenye mitandao kwani hujui anayeona ni nani na atafanya nini kutokana na taarifa hizo.
7. Safari au mapumziko
Unapoandika kuwa umesafiri au uko kwenye mapumziko, kwa ufupi umesema “Sipo nyumbani au ofisini hivyo mnaweza kufanya chochote”.
Kumbuka taarifa kama hizi ni muhimu katika kufanikisha uhalifu. Jitahidi kuweka picha au taarifa kama hizi baada ya safari au mapumziko ili kulinda usalama wako.
8. Vitu ambavyo usingependa watu wengine wavione
Kuchapisha kitu kwenye mtandao wa kijamii na kukifuta haina maana kuwa hakijaonwa au hata kupigwa picha na mtu mwingine.
Nimeshuhudia watu wakilia kwa kujikuta kwa bahati mbaya waajiri, wafanyakazi wenzao au wanafamilia wakiona taarifa zao ua vitu ambayo wasingepaswa kuviona.
Kumbuka taarifa katika mitandao ya kijamii husambaa kwa kasi sana; hivyo ni rahisi kuonwa na watu wengi hata wasiokusudiwa.
9. Taarifa za kazi au zinazohusiana na kazi yako
Watu wengi hupenda kujionyesha wakiwa ofisini, pia wengi hupenda kuchapisha maswala mbalimbali yahusuyo kazi zao. Huwezi kujua nani anaona taarifa hizo na atazitumiaje.
Namkumbuka dada mmoja aliyekuwa akieleza marafiki zake kwenye mtandao anavyomdanganya mwajiri wake katika manunuzi ya kampuni; kumbe kuna mtu alitaka ile nafasi ya yule dada.
Mara siku moja yule mtu akamwonyesha mwajiri mambo aliyokuwa akiyafanya yule dada na kuyaweka kwenye mtandao wa Facebook. Kilichotokea yule dada alipoteza kazi yake. Hivyo basi tenganisha kazi yako na mitandao ya kijamii.
10. Maisha binafsi au ya faragha
Kuna ulimbukeni umeibuka siku hizi, hasa kwa wakina dada wa kuweka picha na video mbalimbali wakiwa faragha.
Siku hizi watu huweka picha wakiwa bafuni, wakiwa wamelala, wakiwa baa, wakifanya tendo la ndoa, n.k. Huwezi kujua ni nani ataiona akaunti yako na atachukua maamuzi gani.
Nakumbuka siku moja nilikuwa naomba kazi fulani kutoka kwa wazungu; nakumbuka walitaka pia akaunti zangu zote za mitandao ya kijamii palepale. Fikiri ningekuwa naweka picha za ngono au za ajabu ajabu; ingekuwa aibu wala kazi nisingepata.
11. Mali na utajiri
Akaunti nyingi za watu hupambwa kwa mali na maisha ya anasa na kifahari. Watu wamekwenda mbali zaidi na kuweka kila kitu walichonacho kwa piacha, maandishi na hata zideo.
Nimeshuhudia watu wakiweka magari, nyumba, viwanja, mishahara, kiasi cha matumizi yayo, bei za vitu walivyo navyo n.k. Ulishawahi kujiuliza haya yote ni kwa ajili ya nini? Je ni wote wanaburudishwa na taarifa hizi?
Fungua macho; hapa ni sawa na kumpeleka swala katika bunge la simba. Tambua unawajulisha wahalifu palipo na vya kuiba; hivyo ficha maswala yahusuyo mali na utajiri wako katika mitandao ya kijamii.
Hitimisho
Naamini umefunguka macho; kwani hutoweka tena vitu tajwa hapo juu ili kuimarisha usalama wako na kulinda nafasi na heshima yako. Mitandao ya kijamii ikitumiwa vyema inaweza kuwa na manufaa makubwa sana. Jifunze kutumia mitandao hii kwa manufaa na si kwa mzoea na kufuata mkumbo.
Je una swali au maoni yoyote kuhusiana na makala hii? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.