Kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari mawasiliano (TEHAMA), mfumo wa biashara pia umebadilika. Hivi leo ni rahisi kutuma na kupokea pesa, kuuza au hata kununua bidhaa kwa njia ya mtandao. Watu wengi hupenda kufanya manunuzi na mauzo ya bidhaa kwenye mtandao kutokana na urahisi wa upatikanaji wa bidhaa na huduma kupitia mtandao.
Pamoja na nafasi hii kubwa ya mtandao katika maswala yanayohusu fedha, zipo changamoto mbalimbali zinazoandamana na miamala na manunuzi ya kwenye mtandao. Fahamu jinsi unavyoweza kujilinda unapofanya miamala au manunuzi mbalimbali kupitia mtandao.
1. Tumia kinga-virusi (antivirus) bora
Mtandao wa intanet ni chanzo kikubwa cha virusi na wadukuzi. Hivyo ni vyema ukatumia programu madhubuti kwa ajili ya kukukinga na virusi na wadukuzi mara unapofanya manunuzi kwenye mtandao. Zipo pragramu mbalimbali nzuri, za bure ama za kununuliwa kama vile Kaspersky, Bitdefender, AVG, n.k Programu hizi hulinda kifaa chako na mawasiliano yako ili kuhakikisha viko salama.
Soma pia: Usalama wa Msingi wa Kompyuta: Jinsi ya Kujilinda na Virusi, Wadukuzi na Wezi.
2. Hakikisha tovuti husika inaaminika
Siyo tovuti zote ni salama. Nyingine ni bandia au hazijatengenezwa kwa kuzingatia kanuni na mifumo ya usalama kwenye mtandao. Hakikisha tovuti unayotaka kufanya miamala inaaminika na inafahamika vyema. Pia hakikisha kuwa inalinda taarifa na mawasiliano yako kwa njia kama vile Secure Sockets Layer (SSL). Kwa kufanya hivi utakuwa na uhakika wa fedha na taarifa zako muhimu.

3. Tumia hudama zitakazokulinda zaidi wewe
Usiamini sana mambo unayoyaona kwenye mtandao. Ni vyema siku zote ukatafuta huduma ambazo zitakulinda zaidi wewe na fedha au mali zako. Kwa mfano badala ya kuingiza taarifa za kadi yako ya benki moja kwa moja ili kufanya miamala, unaweza kutumia huduma kama vile Paypal, Skrill, Google wallet n.k ili kutunza fedha zako na kufanyia miamala. Kwa njia hii huduma hizi zitailinda akaunti yako kufikiwa moja kwa moja wakati wa kufanya miamala mbalimbali.
4. Usitoe taarifa za siri au muhimu ovyo
Unapotoa taarifa zako muhimu kama vile nywila (password), jina la mtumiaji (username), namba za akaunti za benki, barua pepe n.k kwa watu wabaya unawapa nafasi ya kukufanyia uhalifu. Ni lazima ujiepushe na watu wanaotumia njia za ujanja ujanja kukudanganya uwape taarifa zako muhimu. Hakikisha unaweka taarifa zako sehemu unapopaamini na kupafahamu vyema.
Soma pia: Mambo 8 ya Kufanya ili Kuwa na Nywila (password) Imara na Salama.
Neno la mwisho
Kutokana na kushamiri kwa matendo makubwa ya kihalifu kwenye mitandao, watu wengi wameogopa kufanya kitu chochote kinachohusu fedha kwenye mtandao. Lakini ni muhimu ukazingatia usalama kwanza kabla ya mambo yote unapotaka kufanya miamala kwenye mtandao. Chunguza tovuti na biashara husika vyema; fahamu maoni ya watu wengine (reviews) kuhusu tovuti au biashara husika ndipo ufanye miamala yako. Kwa kuzingatia haya utaweza kujilinda na kuwa salama kwenye miamala yako utakayofanya kwa njia ya mtandao.
Je wewe umeshafanya miamala kwenye mtandao? Je huwa unajilinda kwa njia gani? Je ulishawahi kupata tatizo? Tafadhali tuandikie maoni yako kisha washirikishe wengine.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.