Athari au Madhara 10 ya Intaneti Unayopaswa Kuyafahamu - Fahamu Hili
Friday, March 29Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Athari au Madhara 10 ya Intaneti Unayopaswa Kuyafahamu

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Intaneti

Katika dunia hii ya leo ni vigumu kuishi bila kutumia intaneti kwa namna moja au nyingine. Watu hutumia intaneti kuwasiliana, kupata taarifa na habari au hata  kujipatia kipato.

Kuwepo kwa intaneti kumerahisisha maisha ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa na kufanya utendaji kazi wake uwe bora zaidi.

Pamoja na intaneti kuwa na manufaa kadha wa kadha, intaneti ina athari mbalimbali. Hivyo basi fahamu madhara 10 ya intaneti.

1. Taarifa za uongo

Kila mtu anaweza kuweka taarifa kwenye mtandao wa intaneti, hivyo ni rahisi kukumbana na taarifa zisizo za kweli.

Swala hili limepelekea baadhi ya nchi na mashirika mbalimbali kujaribu kukabili taarifa mbalimbali zinazopatikana kwenye mtandao ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na taarifa hizo.

Ni vyema kuhakikisha tovuti au blog unayochukua taarifa inaaminika ili usije ukapotoshwa na taarifa za uongo.

2. Kichaka cha wahalifu

Wahalifu wengi hasa wale wanaotumia teknolojia hufanya uhalifu wao kwa hutumia mtandao wa intaneti au kuutumia kama kichaka chao cha kujificha.

Mtu anaweza kuwa Iran akamdukua mtu au tovuti iliyoko Marekani bila kizuizi chochote. Hivyo ni muhimu kuwa makini pamoja na kuzingatia kanuni za usalama kwenye mtandao ili uwe salama mara utumiapo intaneti.

3. Humfanya mtu kuwa mtawaliwa (addicted)

Ni rahisi mtu kuwa mtawaliwa wa mtandao wa intaneti (internet addict). Baadhi ya watu hukaa siku nzima kwenye mtandao wa intaneti au hushindwa kutimiza majukumu yao ya kila siku kwani wao kila mara wako kwenye mtandao.

Ni muhimu kuwa na kiasi katika matumizi yako ya intaneti ya kila siku ili usiwe mtawaliwa wa intaneti.

Soma pia: Mambo 18 ya Kushangaza Kuhusu Intaneti Usiyoyajua

4. Husambaza picha za ngono

Picha nyingi za ngono husambaa kwa kasi kubwa kupitia mtandao wa intaneti. Hatari zaidi ni kuwa picha hizi zinaweza kupatikana bure tena kwa urahisi kwa kila mtu.

Hili limesababisha picha za ngono kuwa rahisi kufikiwa na watoto, jambo ambalo huwaathiri kimwili na kisaikolojia.

Soma pia: Vitu 10 Vinavyoharibu Maadili ya Watoto

5. Kupoteza muda

Moja kati ya vitu vinavyopoteza muda mwingi ni mtandao wa intaneti. Watu hutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii au kutazama video au picha mbalimbali; muda huu ungeweza kutumiwa kwenye mambo mengine yenye tija zaidi.

6. Hurahisisha udanganyifu wa kitaaluma

Mtandao wa intaneti umekuwa ni chanzo kikubwa cha udanganyifu wa kitaaluma. Wanafunzi hununua na kupakua mitihani, insha au hata maandiko mengine ya kitaaluma kutoka kwenye mtandao ili wafaulu vyema masomo yao.

Swala hili limewafanya wanafunzi wengi wasifanye bidii kwenye masomo yao pamoja na kutumbukia kwenye wizi wa kazi za kitaaluma.

7. Hubeba biashara haramu

Mtandao wa intaneti ni mfumo mkubwa sana ambao unahusisha maelfu kwa mamilioni ya kompyuta, watu, pamoja na shughuli mbalimbali.

Baadhi ya watu hutumia mtandao wa intaneti hasa sehemu ile inayojulikana kama Deep Web ili kutekeleza bishara zao haramu kama vile kuuza madawa ya kulevya, silaha, n.k.

Soma pia: Fahamu Kuhusu Sehemu ya Mtandao wa Intaneti Iliyofichwa (Deep web na Dark web)

8. Huathiri afya

Kutumia mtandao kwa muda mrefu siyo jambo zuri kwani kunaweza kuathiri afya ya macho yako pamoja na viungo vingine vya mwili.

Inakupasa kufanya shughuli nyingine au mazoezi badala ya kukaa kwenye mtandao wa intaneti siku nzima.

9. Ni chanzo cha kusambaa kwa virusi vya kompyuta

Virusi vya kopyuta husambaa kwa urahisi sana kupitia mtandao wa intaneti.

Mfano mzuri ni kirusi cha Code Red kilichoibuka mwaka 2001 na kusambaa kwa kasi sana kwa muda usiozidi wiki moja na kuweza kuathiri seva 400,000 na kompyuta milioni moja kote duniani.

Soma pia: Virusi 10 vya Kompyuta Hatari Zaidi Kuwahi Kutokea

10. Huongeza matumizi ya pesa

Ili uweze kutumia intaneti utatakiwa kuwa na kifaa kama vile simu au kopyuta pamoja na huduma ya mawasiliano ya intaneti — yaani data.

Hivi vyote kwa jumla vinahitaji pesa ili uweze kuvipata. Hivyo kutumia mtandao wa intaneti sana kutakuongezea gharama ya matumizi.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema

Hitimisho

Pamoja na mtandao wa intaneti kuwa na manufaa mbalimbali, naamini sasa umeona kuwa zipo athari au madhara mbalimbali yatokanayo na mtandao wa intaneti ambayo hayapaswi kupuuzwa.

Ni muhimu kutawala matumizi yako pamoja na kuzingatia kanuni za usalama kwenye mtandao ili usiathirike.

Je wewe huwa unatumia mtandao wa intaneti? Je unapata manufaa aa madhara gani? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

3.6 25 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

4 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
waler*
waler*
3 years ago

huathiri hulka za watu

Vo_stee
Vo_stee
3 years ago

Imenisaidia sana

4
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x