Kwa miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa kuporomoka kwa maadili ya watoto kwa kiwango kikubwa. Hili limepelekea kuibuka kwa maswali mengi juu ya ni nini hasa chanzo cha tatizo hili.
Hivi leo watoto wengi hawaheshimu wazazi wala waliowazidi umri, wanatumia pombe na madawa, wanaiba, wana kiburi, wavivu, n.k.
Kwa hakika vipo vitu vinavyochangia katika kuporomoka kwa maadili ya watoto. Karibu nikushirikishe vitu 10 vinavyoharibu maadili ya watoto.
1. Wazazi kuwa mfano mbaya
Wazazi wa karne hii wengi wanawalaumu watoto kuwa wana maadili mabaya, lakini chanzo cha tatizo hili ni wao wenyewe.
Wazazi wamekuwa wakilewa, kutukanana, kupigana au hata kufanya mambo mengine machafu kama vile uzinzi mbele ya watoto. Kwa hakika tabia hizi zinapofanywa mbele ya watoto nao huziiga na kuzifanya.
Wazazi wengine pia wamekuwa wakiwadekeza au kutokusimamia vyema maadili kwa watoto wao na kuwafanya kukua bila malezi bora.
Soma pia: Makosa 15 ya Kuepuka Katika Malezi ya Watoto
2. Teknolojia
Teknolojia ina manufaa yake lakini pia ina hasara zake hasa kwenye malezi ya watoto. Hivi leo watoto wanatazama mambo maovu kwenye televisheni na mtandao wa intaneti na kuyaiga.
Jambo hili limepelekea watoto kujifunza tabia chafu kutoka kwenye tamaduni za kimagharibi zilizoporomoka.
3. Marafiki
Inawezekana mtoto amelelewa vizuri nyumbani lakini akajifunza mambo mabaya kutoka kwa marafiki zake.
Jambo hili limesababisha maadili ya watoto kuharibika kwani watoto wanaotoka katika familia au mazingira yenye kiwango kikubwa cha kuporomoka kwa maadili huwafundisha wengine tabia mbaya.
4. Mazingira mabaya ya kuishi
Siyo kila mazingira ya kuishi ni mazuri kwa malezi ya watoto. Mazingira mengine huwaharibu watoto kisaikolojia na kuwafanya wawe na tabia mbaya.
Hebu fikiri mtoto anayekaa kwenye mazingira yanayouziwa au yanayofanyika biashara za madawa ya kulevya au ukahaba; ni wazi kuwa mtoto ataiga tabia chafu kutokana na mazingira haya yanayomzunguka.
5. Maadili duni kwa wanafamilia
Inawezekana wazazi wamekuwa na maadili mema, lakini wanafamilia wengine hawana maadili mema. Hili bado kwa kiasi kikubwa litaharibu maadili ya watoto.
Ikumbukwe kuwa mtoto huiga tabia na matendo anayoyaona kwa wale wanaomzunguka mara kwa mara.
6. Unyanyasaji
Vitendo vya unyanyasaji vimeshamiri sana hivi leo. Watoto huchomwa, hupigwa sana, hubakwa, hulawitiwa na hata kufanyiwa unyanyasaji mwingine.
Matendo haya humharibu mtoto kisaikolojia na kumfanya akue akiwa na majeraha ya nafsi na akili ambayo humfanya awe na tabia mbaya.
Mara nyingi watoto waliofanyiwa unyanyasaji hutaka kulipa kisasi au hukata tamaa na kuishi maisha ya hovyo.
7. Malezi ya upande mmoja
Malezi ya upande mmoja ni changamoto kubwa sana iliyoshamiri hivi leo. Hili linatokana na kuwepo kwa watu wengi wanaozaa nje ya ndoa au kuvunjika kwa ndoa nyingi.
Kuna umuhimu mkubwa wa mtoto kulelewa na pande zote, yaani baba na mama. Watoto wengi waliolelewa na mzazi mmoja huwa na maadili mabaya, hasa kama chanzo cha malezi hayo ni kuvunjika kwa ndoa.
8. Kutokusikilizwa
Watoto nao wana haki ya kusikilizwa. Wazazi wengi wana shughuli nyingi hasa za kutafuta pesa, hivyo hawana muda wa kukaa kutulia na kuwasikiliza watoto wao.
Mtoto asiposikilizwa huwa mkatili na mwenye majeraha mengi ya nafsi na akili.
9. Kutokupata huduma stahiki
Mtoto anahitaji huduma stahiki kama vile chakula, malazi, mavazi, matibabu, elimu, burudani, n.k. Kwa kutokumpa mtoto huduma anazohitaji, humfanya athirike kisaikolojia au hata awe na tabia kama vile udokozi na wizi ili apate mahitaji yake.
10. Utamaduni wa kimagharibi
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kumekuwa na mwingiliano mkubwa wa tamaduni. Watu wengi huona tamaduni zao za Kiafrika hazina maana na kutaka kufuata tamaduni za kimagharibi.
Hili limesababisha watoto kuwa na maadili mabaya kwani huiga tabia mbaya za kimagharibi. Watoto hujifunza kudeka, kulilia vitu vya anasa au hata kutaka kuishi kama watoto wa kimagharibi.
Kutokana na hili, siku hizi watoto wanataka kwenda disko, kuvaa kimagharibi, kuwa na wapenzi, kutokupangiwa kazi na wazazi, n.k.
Hitimisho
Kwa hakika kuharibika au kuporomoka kwa maadili ya watoto hivi leo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na vitu vilivyoelezwa hapa juu. Ikiwa wazazi na walezi wanataka kunusuru vizazi vijavyo, ni vyema wahakikishe wanakabili vitu tajwa hapo juu ili kulinda maadili ya watoto yasiharibike.
Je una maoni au swali lolote? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
Hongera nimeipenda kwa kufuata hayo hakika tutakuwa na kizazi chenye maadili mema na mazuri ahsantee
Tunashukuru sana kwa kuwa msomaji wetu; pia tunashukuru kwa maoni yako ya thamani; tunakutakia kila la heri katika malezi…karibu sana Fahamuhili.