Sababu 7 za Kwa nini Hutakiwi Kutafuta Mpenzi Kwenye Mtandao wa Intaneti - Fahamu Hili
Friday, May 24Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Sababu 7 za Kwa nini Hutakiwi Kutafuta Mpenzi Kwenye Mtandao wa Intaneti

Washirikishe Wengine Makala Hii:
Wapenzi kwenye mtandao
Chanzo cha picha: http://www.paycron.com/

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia hasa katika sekta ya mawasiliano yamebadili mambo mengi. Hili ni tofauti na hapo awali ambapo watu walitegemea njia duni za mawasiliano kama vile posta.

Kutokana na maendeleo haya katika teknolojia ya mawasiliano, suala la mahusiano pia limebadilika kwa kiasi kikubwa. Hivi leo watu wanaweza kutafuta wapenzi kwenye mtandao wa intaneti bila kizuizi chochote.

Kwa hakika bila shaka kila jambo lina uzuri na ubaya  wake; hivyo suala la kutafuta wapenzi kwenye mtandao linatakiwa kutazamwa kwa jicho la pili.

Ikiwa umejiunga au unataka kujiunga na mitandao ya kutafuta wapenzi, basi fahamu sababu 7 za kwanini hutakiwi kutafuta mpenzi kwenye mtandao wa intaneti.

1. Watu wanaigiza uhalisia

Katika eneo ambalo watu wanaigiza uhalisia wa maisha kwa kiasi kikubwa ni kwenye mitandao ya kutafuta wapenzi pamoja na mitandao ya kijamii.

Watu huweka picha ambazo siyo zao, majina ya uongo, maelezo binafsi ya uongo, hali za mahusiano za uongo, eneo la makazi la uongo, n.k.

Ni muhimu kuwa makini kwani nimewahi kuona watu wakikimbia baada ya kukutana na wapenzi wao wa kwenye mtandao na kubaini kuwa hawako kama walivyowafahamu au kuwatarajia.

Hivyo kutafuta mpenzi kupitia mitandao ya kutafuta wapenzi ni rahisi kutapeliwa au kudanganywa kwani watu wanaigiza uhalisia.

2. Ni biashara

Mitandao mingi ya kutafuta wapenzi imeanzishwa kwa lengo la kibiashara. Hivyo uhalisia wa kupata mpenzi sahihi ni mdogo kwani suala la kutafuta wapenzi hutumiwa kama njia ya kupata pesa.

Kwa mfano unaweza kuanza mahusiano na mtu kumbe analipwa pesa afanye hivyo ili mfumo uzidi kupata wanachama au watembeleaji zaidi na hatimae kuzalisha pesa zaidi.

Kumbuka pia baadhi ya mitandao ya kutafuta wapenzi hutoza ada ya uwanachama ili kujipatia pesa.

3. Umbali

Lengo mojawapo la mahusiano ni watu wawili kukaa pamoja kwa karibu zaidi ili washirikishane hisia zao. Hivyo kwa kiasi kikubwa umbali unaweza kuathiri mahusiano.

Pamoja na teknolojia kuwaleta watu karibu, bado kiuhalisia kuna umbali ambao hauwezi kumalizwa kwa simu au kompyuta.

Hebu fikiri haya; je unaweza kumlisha mtu kitu kwa mtandao? Je unaweza kumkumbatia mtu kwa mtandao? Je unaweza kumbusu mtu kiuhalisia kwenye mtandao? Je unaweza kumbeba mtu kwa mtandao?

Naamini umeona jisi ambavyo mtandao unafanya mahusiano yawe duni, dhaifu, yasiyo na ladha na yanayoweza kuvunjika wakati wowote.

4. Hakuna mapenzi ya kweli

Mara nyingi watu wengi wanaojiunga na mitandao ya kutafuta wapenzi ni watu wanaojaribu mifumo hiyo au watoto.

Hivyo ni vigumu sana kupata mtu mwenye nia ya dhati ya kujenga mahusiano bora ambayo hatimaye yanaweza kufikia ndoa.

Kumbuka pia kwa kuwa tovuti za kutafuta wapenzi ni nyingi, ni rahisi mtu kuvunja mahusiano kwani atapata mpenzi mwingine ndani ya muda mfupi.

Soma pia: Sifa 17 za Kuzingatia Kwa Mtu Unayetaka Kuoa au Kuolewa Naye

5. Watu wengi wamejeruhiwa

Majeraha ya mahusiano huharibu mahusiano ya watu wengi. Tafiti mbalimbali zilibaini kuwa watu wengi wanapojeruhiwa au kukosana na wapenzi wao hukimbilia kwenye mitandao ya kutafuta wapenzi.

Hebu fikiri unaanza mahusiano na mtu mwenye majeraha na uchungu wa mahusiano yaliyopita; ni wazi hamtoweza kujenga mahusiano yatakayodumu.

6. Kudanganyana ni rahisi zaidi

Je umewahi kusikia mtu akipiga simu akiwa kwenye daladala Dar es Salaam lakini anasema yuko Mwanza? Haya ndiyo mambo yanayotawala mitandao ya kutafuta wapenzi.

Kwa kuwa humwoni mtu unayewasiliana naye, ni rahisi kukudanganya kwenye mambo mengi. Anaweza kuwa anawasiliana na wapenzi sita kwa wakati mmoja lakini hutoweza kubaini.

Hivyo mahusiano ya kawaida yaani ya ana kwa ana bado yanazidi kuwa na nguvu zaidi kuliko yale ya kwenye mtandao.

7. Unaweza kufanyiwa uhalifu

Unapoingia kwenye mahusiano na mtu kwa kupitia mitandao ya kutafuta wapenzi mnaweza kubadilishana taarifa kadhaa. Ikiwa utatoa taarifa zako muhimu kama vile pasi ya kusafiria, kadi za benki, n.k. taarifa hizo zinaweza kutumiwa na wahalifu kukufanyia uhalifu.

Kumbuka mtu anaweza kuvaa kofia ya kutafuta mpenzi kumbe ndani yake ni mwizi hatari anayetafuta kuwaibia watu; hivyo kuwa makini na mitandao hii.

Soma pia: Njia 4 za Kujilinda Unapofanya Miamala au Manunuzi Kwenye Mtandao

Neno la mwisho

Kwa hakika wahenga waliposema si kila king’aacho ni dhahabu hawakukosea kitu. Ni muhimu sana kuchunguza vitu vinavyoletwa na wimbi la teknolojia ili kuona ubora, usalama na uhalisia wake.

Unaweza kujitumbukiza kwenye matatizo makubwa yanayoweza hata kugharimu uhai wako kwa kuingia kwenye mahusiano na mtu usiyemfahamu vizuri kwenye mtandao. Hivyo kuwa makini na chukua tahadhari mapema.

Je wewe huwa unatumia mitandao ya kutafuta wapenzi? Je ni nini uzoefu wako juu ya matumizi ya mitandao hii?

Tafadhali unaweza kuandika maoni yako hapo chini kisha ukawashirikisha wengine makala hii.

0 0 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x