Sifa 17 za Kuzingatia Kwa Mtu Unayetaka Kuoa au Kuolewa Naye - Fahamu Hili
Tuesday, March 19Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Sifa 17 za Kuzingatia Kwa Mtu Unayetaka Kuoa au Kuolewa Naye

Washirikishe Wengine Makala Hii:
maharusi
Chanzo cha picha: http://ichretien.com

Swala la mtu wa kuoa au kuolewa naye ni swala nyeti linalohitaji maamuzi yanayohusisha hekima, utulivu, kumwomba Mungu pamoja na uchunguzi wa kutosha. Maisha ya watu wengi yamekuwa na matatizo makubwa kutokana na kufanya makosa katika kuchagua mtu wa kuoa au kuolewa naye.

Kwa hakika hakuna mtu au mwenzi mkamilifu, lakini kuna sifa za msingi ambazo kila mtu unayetarajia kuoa au kuolewa anapaswa kuzizingatia na kuzitilia maanani.

Naamini unapenda kuoa au kuolewa na mtu sahihi. Karibu nikushirikishe sifa 17 za kuzingatia kwa mtu unayetaka kuoa au kuolewa naye.

1. Ana malengo na maono

Hakikisha mtu unayetaka kuoana naye ni mtu mwenye malengo katika maisha yake. Mtu mwenye malengo hujishughulisha kila mara kuhakikisha anaandaa baadaye yake.

Mtu asiyekuwa na malengo huwaza matumizi na anasa kuliko kuzalisha; hafanyi kazi wala hajali kuhusu kesho. Hakika mtu kama huyu hawezi kuingia kwenye ndoa ikadumu au akaweza kulea familia yenye ustawi mzuri.

2. Anakuheshimu na kukuthamini

Heshima na kuthaminiana ni msingi muhimu katika ndoa. Nimeshuhudia mwanandoa akimzarau au hata kumbeza mwenzi wake mbele ya wageni au watoto; ni wazi kuwa tabia hii ilianza siku nyingi.

Ni muhimu kuhakikisha mtu unayetaka kuoana naye anathamini utu wako kuliko hata vitu vingine. Hakikisha anakusikiliza na kujali pia hisia zako.

3. Anajali na kuheshimu ndugu na familia yako

Ndoa ni kitu kinachounganisha watu wengi, watu wanapoingia kwenye ndoa familia mbili huungana kupitia ndoa hiyo.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha mtu unayetaka kuoana nae anathamini na kuheshimu familia yako. Naamini usingependa mama, baba, shangazi, mjomba au ndugu yako wa damu adharauliwe na mwenzi wako.

Hivyo chunguza msimamo na tabia ya yule unayetaka kuoana naye ukoje juu ya familia yako kabla hamjaoana.

4. Anakuamini

Migogoro mingi kwenye ndoa inatokana na wanandoa kutokuaminiana. Kamwe usikubali kuoana na mtu ambaye hakuamini vyema.

Nimeshuhudia watu wakiwekewa watu wa kuwafuatilia, simu zao zikifuatiliwa na hata kuwekewa sheria kali kutokana na mwenzi mmoja kutokumwamini vyema mwenzake.

Kumbuka! Kama anakupenda kweli atakuamini na kuwa mwaminifu kwako.

5. Hakutamani bali anakupenda

Watu wengi hutamaniana badala ya kupendana. Tamaa huongozwa na vitu au mwonekano wa nje tu.

Hakikisha unaoana na mtu ambaye hata ukiwa mgonjwa, mzee, maskini au dhaifu bado atakupenda tu jinsi ulivyo. Kumbuka pia upendo wa kweli hautaki malipo wala hauulizi kwanini. Tamaa huhusisha hisia kali  na baada ya muda hisia hizi hutoweka na kuisha kabisa ila upendo huhusisha bidii, kujitoa, kuvumilia na akili nyingi.

6. Anamheshimu Mungu

Watu wengi hupuuza nafasi ya Mungu katika mahusiano na maisha yao kwa ujumla. Ni muhimu ukakumbuka kuwa kwa asili binadamu hakuumbwa kukaa bila imani ya kitu chochote.

Mwenzi mwenye hofu ya Mungu atakujali, atakuheshimu, atakuthamini, atakutia moyo, atakuombea na hata kulea familia katika maadili mema.

7. Anakufanya ufurahi

Kuna watu wanakaa kwenye mahusiano na watu ambao hawawapi furaha lakini bado wanaendelea kung’ang’ania hadi ndoa. Inawezekana hiii ni kutokana na upendo kujengwa kwenye vitu kama vile pesa n.k.

Kumbuka kuwa hakuna mbadala wa ndoa, ukishaingia umeingia; hivyo hakikisha mtu unayeoana nae anakufanya ufarahi kila mara na si uhuzunike maana utahuzunika maisha yako yote.

8. Anakusaidia kuwa bora zaidi

Je ulikua hujui kuvaa akakufundisha kuvaa? Ulikuwa hujui kupika akakufundisha kupika? Au umejifunza vitu vipya kutoka kwake?

Ni muhimu ukajiuliza maswali kama haya ili uweze kupata mwenzi wa maisha ambaye anaweza kukufanya kuwa bora zaidi na si kukurudisha nyuma au kukuacha ulivyo.

9. Ni msikivu

Usikivu ni tabia muhimu sana kwenye ndoa. Hakikisha yule unayetaka kuoana naye ana usikivu mzuri. Uwekaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali katika familia unategemea kusikilizana.

Hebu fikiri baba anataka kujenga wakati mama anataka kununua gari, baba anataka mama asimamie miradi wakati mama anataka kwenda kusoma; ni wazi kuwa hapa kutakuwa na sitofahamu kubwa.

10. Anayesamehe

Watu wanapokaa pamoja, kukoseana hakuepukiki. Hivyo ni muhimu kumchagua mwenzi wa maisha ambaye anajua umumu wa kusamehe.

Epuka kuoana na mtu mwenye tabia za kubeba vinyongo na chuki kwani mtashindwana mapema kwenye ndoa.

Soma pia: Sababu 9 za Kwanini Umsamehe Aliyekukosea.

11. Upendo wake haujajengwa kwenye vitu

Mapenzi ya leo kwa kiasi kikubwa hujengwa kwenye vitu na mali. Wengi hupendana kutokana na pesa au mionekano ya nje tu; hili limesababisha wengi kutengana pale vitu hivyo vinapokosekana.

Hakikisha kama unataka kuoana na mtu sahihi unatafuta mtu ambaye upendo wake haujajengwa kwenye vitu vya muda vinavyopita.

“Vitu hutumiwa na watu hupendwa, usitumie watu na kupenda vitu.”

12. Anashukurani

Mtu asiye na shukurani ni mtu asiyefaa kuwepo kwenye ndoa. Watu hawa huwa hawaoni jema wala zuri lolote, wao ni kulalamika na kulaumu tu.

Hakikisha unaoana na mtu mwenye shukurani hata kwa mambo madogo, kwani kwa kufanya hivi mtakuwa na ndoa yenye upendo na kuthaminiana kila mmoja.

13. Tendo la ndoa siyo kipaumbele cha kwanza katika mahusiano

Hili ni tatizo kubwa sana ambalo kwa kiasi kikubwa huharibu mahusiano na ndoa za leo.

Watu wengi hujenga mahusiano yao kwenye tendo la ndoa, jambo linalowafanya wengi kuishia kuzaa nje ya ndoa au hata kutokuwa tayari kuingia kwenye ndoa kwani mambo yote ya ndoa tayari yameshafanywa.

Mtu anayekuthamini hatakutaka kimwili bali atauthamini mwili na utu wako hadi mtakapokuwa kwenye ndoa kamili. Wakati fulani nilisoma mtandaoni kuwa “Vijana wengi wa kiume hawafanyi maamuzi ya kuoa kwa kuwa ngono inapatikana kirahisi”

Kumbuka! Kukutana kimwili siyo tiketi ya kuolewa na mtu; mnaweza kukutana kimwili na bado akakuacha, hivyo kuwa makini.

14. Mkarimu

Mwenzi mkarimu ni bora kwani atakuwa mkarimu kwako, familia yako pamoja na wageni watakaofika nyumbani kwenu.

Unapooana na mwenzi mchoyo ni wazi kuwa ataharibu mahusiano yako na watu; wala hatakuwa tayari kukuhudumia wewe au mtu mwingine kupitia vitu mlivyonavyo.

15. Anakutia moyo

Moja ya jukumu muhimu la mwenzi wa maisha ni kukutia moyo hasa pale unapokutana na changamoto. Hakikisha unaoana na mtu anayeweza kubeba raha na mamumivu yako. Kuna msemo maarufu usemao kuwa “mwanaume anaweza kushinda vita zote ila si ya nyumbani mwake” Jaribu kukumbuka kisa cha Samson na Delila, pamoja na umahiri wa ajabu wa Samson katika vita hakuweza kuishinda vita ya nyumbani mwake  iliyoongozwa na mkewe Delila.

16. Anatumia pesa na muda vyema

Mwenzi asiyejua kutumia muda na pesa vyema ni mzigo na hasara kubwa. Ili mtu afanikiwe ni lazima ajifunze umuhimu wa kujali muda pamoja na matumizi mazuri ya pesa.

Hebu fikiri mke anayekaa kwenye televisheni siku nzima au mume anayeshinda kijiweni; niwazi hawa watakuwa masikini na hawataweza kulea familia zao katika malezi bora.

Hakikisha unaoana na mtu anayetunza pesa na muda vyema.

Soma pia: Tabia 10 zitakazobadili maisha yako.

17. Ana ukomavu wa akili

Siyo kila mtu ana akili iliyokomaa kuingia kwenye ndoa. Watu wengine bado ni watoto wadogo ambao hata maaumuzi na matendo yao bado ni ya kitoto.

Ndoa ni swala linalohitaji akili iliyokomaa vyema inayoweza kufanya maamuzi sahihi pamoja na kupambanua jema na baya. Hivyo hakikisha unaoana na mtu mwenye upeo mzuri wa kufikiri.

Neno la mwisho

Kila mtu anaweza kujifunza sifa hizo anuwai hapo juu na akawa mahiri kwazo. Pia ni muhimu sana sana uweke akilini mwako kuwa sifa hizi hazitoendelea kuwepo kwa mwenzi wako ikiwa hautazithamini na kufanya bidii kuzitunza. Kila chenye thamani hulindwa kwa gharama kubwa.

Kwa hakika kuna sifa lukuki ambazo inapaswa kuzizingatia katika swala la kuchagua mwenzi wa maisha. Lakini naamini kwa sifa hizi za msingi nilizozijadili hapa zitakupa msingi mzuri wa kuchagua mwenzi atakayekufaa maishani.Je unaye mwenzi mwenye sifa hizi? Je kuna sifa nyingine muhimu unazozizingatia?

Tafadhali tuandikie maoni yako kisha washirikishe wengine makala hii. Karibu pia ufuatilie ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

3.4 14 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Bernard Deus
Bernard Deus
3 years ago

Shukrani sana nimejifunza kitu

Kornelio Maanga
Reply to  Bernard Deus
3 years ago

Asante sana kwa maoni yako ya thamani kwetu; karibu sana Fahamuhili.com

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x