Madhara 6 ya Kutumia Dawa Bila Ushauri wa Kitaalamu - Fahamu Hili
Friday, May 24Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Madhara 6 ya Kutumia Dawa Bila Ushauri wa Kitaalamu

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Dawa

Mara nyingi watu wanaugua maradhi mbalimbali, lakini wengi wao hawapendi kwenda hospitali kufanya vipimo au kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa daktari.

Kutokana na uwepo wa maduka ya dawa baridi, watu wengi wanapojisikia kuwa wagonjwa, hununua dawa kwenye maduka hayo na kuanza kuzitumia.

Ni ukweli usiopingika kuwa dawa zimetengenezwa ili kutibu maradhi fulani ambayo yatabainika kwa mgonjwa baada ya uchunguzi wa kitaalamu.

Hivyo matumizi ya dawa bila kufanya uchunguzi wa kitaalamu yanaweza kuwa na madhara makubwa kwenye afya yako. Fahamu madhara 6 ya kutumia dawa bila ushauri au uchunguzi wa kitaalamu.

1. Huongeza sumu mwilini

Dawa zimetengenezwa kwa kutumia kemikali mbalimbali ambazo kimsingi ni sumu zinazoua vimelea vya magonjwa.

Hivyo kutumia dawa bila vipimo kunakusababishia kuongeza sumu za dawa hizo mwilini mwako kwani umetumia dawa ambazo mwili hauzihitaji kukabili ugonjwa husika.

Sumu hizi zinapokusanyika mwilini mwako zinaweza kukuletea athari mbalimbali za muda mfupi au hata mrefu.

Soma pia: Njia 12 za Kuondoa Sumu Mwilini.

2. Hutengeneza usugu wa maradhi

Mtaalamu wa afya hukupa kiwango (dosage) cha dawa kulingana na vipimo alivyovifanya; hivyo kutumia dawa bila vipimo vya kitaalamu kunaweza kusababisha vimelea vya ugonjwa vizoee dawa husika na kusababisha ugonjwa huo usitibike tena.

Hili ndilo linalosababisha maradhi kama vile malaria sugu au UTI sugu. Hivyo kabla ya kutumia dawa ni vyema ukafanya uchunguzi wa kitaalamu

3. Huweza kusababisha saratani

Dawa zinapoingia mwilini mwako kimakosa na kushindwa kufanya kazi yake, zinaweza kuharibu baadhi ya seli za mwili na kuzifanya kugeuka seli za saratani. Hivyo hakikisha dawa unayoitumia ni sahihi na inalenga ugonjwa husika.

4. Huweza kusababisha kifo

Kama nilivyoeleza kwenye hoja zilizotangulia, dawa ni sumu zinazokabili vimelea vya magonjwa. Hivyo kutumia dawa vibaya kunaweza kusababisha kifo.

Ikumbukwe pia watu wenye matatizo maalumu kama vile maradhi ya moyo pamoja na shinikizo la damu, wanapaswa kuwa makini na dawa wanazozitumia kwani zinaweza kuchochea matatizo yao na hatimaye kifo.

5. Kuibua tatizo la mzio (allergy)

Kuna watu wenye tatizo la mzio au wengi huita “aleji” kwa lugha isiyo sanifu, watu hawa wanapaswa kuwa makini na kuepuka kutumia dawa bila ushauri wa kitaalamu.

Hili ni kutokana na baadhi ya dawa kutokuendana na afya zao, hivyo kusababisha tatizo lao la mzio kuibuka. Ni vyema ukamwona mtaalamu wa afya na umweleze aina ya mzio uliyo nayo ili akupe dawa stahiki.

6. Huweza kuathiri afya ya mama na mtoto

Mama mjamzito anatakiwa kuwa makini sana katika swala la matumizi ya dawa. Dawa anazozitumia mama zinaweza kumuathiri yeye pamoja na mtoto aliyeko tumboni.

Hivyo ni muhimu sana kwa mama mjamzito anapohisi dalili za maradhi fulani akamwona mtaalamu wa afya ili amfanyie uchunguzi na kumpa tiba sahihi.

Hitimisho

Ni muhimu ukumbuke kuwa dalili za ugonjwa mmoja zinaweza kuwa dalili za ugonjwa mwingine pia. Hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi pamoja na kutafuta ushauri wa kitabibu kabla ya kutumia dawa zozote kutibu maradhi yanayokukabili.

Je wewe huwa unatumia dawa baada ya ushauri wa kitaalamu? Je ulishawahi kupata tatizo kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa?

Tafadhali tuandikie maoni yako kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kujiunga nasi kwa barua pepe hapo chini au kulike ukurasa wetu wa Facebook ili ufahamu mengi zaidi.

5 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x