Mbinu 7 za Kulinda Biashara Yako Dhidi ya Athari za Corona (COVID 19) - Fahamu Hili
Tuesday, March 19Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mbinu 7 za Kulinda Biashara Yako Dhidi ya Athari za Corona (COVID 19)

Washirikishe Wengine Makala Hii:
COVID 19

Ni wazi kuwa dunia nzima inapitia msimu mpya baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa homa ya mapafu wa Corona ulioibuka mnamo mwaka 2019 (COVID 19). Pasipo shaka sekta na taasisi mbalimbali zimeshuhudia mabadiliko makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa hayakutegemewa wala hazikujiandaa kwa mabadiliko hayo.

Moja ya sekta iliyoathiriwa na inaendelea kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko yaliyoletwa na Corona ni biashara; biashara nyingi zimeporomoka, nyingine zimekufa na wakati nyingine zikijikuta katika wakati mgumu wa kujiendesha kwa utamaduni wake uliozoeleka.

Karibu nikushirikishe mbinu 7 ambazo ikiwa utazitekeleza kikamilifu basi kwa kiasi kikubwa utaweza kukabili athari zitokanazo na ugonjwa wa Corona  (COVID 19) kwenye biashara.

1. Punguza matumizi yasiyo ya lazima

Kutokana na athari za corona kwenye mapato ya biashara nyingi ni vyema kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwenye biashara yako ili kuilinda dhidi ya athari mbaya zaidi za kifedha zinazoweza kutokea kutokana na Corona.

Hakikisha rasilimali zote za biashara zinatumika vyema na kwa weledi mkubwa. Epuka matumizi ya anasa, usimamizi duni wa rasilimali za biashara kama vile umeme, maji na intaneti au matangazo ya gharama kubwa ambayo hayana ulazima sana kwa sasa.

Soma pia: Njia 8 Rahisi za Kupunguza Matumizi ya Umeme

2. Weka akiba

Huu siyo wakati wa kufagia kila kitu kwenye mifuko ya biashara yako; leo unauza kesho unaweza usiwe unauza. Hakikisha unaweka akiba kwa ajili ya biashara yako ili uweze kukabili changamoto mbalimbali za kifedha zinazoweza kukumba biashara yako huko mbeleni.

Kumbuka kuwa ugonjwa wa Corona umefanya upatikanaji wa fedha kuwa mgumu hata zinapopatikana mathalan kutoka kwenye taasisi za kifedha zinatolewa kwa masharti magumu ambayo ni vigumu kutekelezeka.

Lakini ikiwa umejiwekea akiba itakusaidia kwenye biashara yako mara upatapo changamoto ya kifedha.

Kumbuka! “Mtu anayeweka akiba ni mtu anayewaza kuhusu kesho.”

Soma pia: Faida 8 za Kuweka Akiba Unazopaswa Kuzifahamu

3. Kuwa makini juu ya kuajiri na kupandisha vyeo

Kama nilivyotangulia kueleza kuwa msimu huu mpya baada ya Corona siyo msimu wa kutumia pesa hovyo; ikumbukwe kuwa kuajiri na kupandisha vyeo ni suala linaloongeza gharama za uendeshaji.

Hivyo, ni muhimu kuwa makini juu ya suala hili ili kuhakikisha biashara yako haiingii kwenye matumizi na gharama kubwa zisizokuwa na ulazima.

Kwa mfano kama unaajiri mtu wa mauzo ajiri mtu mwenye uwezo wa kuendesha gari pia badala ya kuajiri dereva na mtu wa mauzo ambao wote wangefanya kazi kwa pamoja.

4. Panga bei vizuri

Huu siyo msimu wa kukomoa wateja kwa bei, hali ya uchumi imebadilika sana kutokana na Corona, watu wengi wamepoteza kazi na wengine vipato vyao vimepungua. Hivyo, hakikisha unapanga bei zako vizuri ili usiwapoteze wateja wako na mwishoe kupoteza mapato ya biashara yako.

Chukua muda kujifunza juu ya bei za washindani wako ili uweze kupanga bei ambayo ni rafiki kwa wateja wako na ambayo itaweza kumudu ushindani ulioko kwenye soko kwa sasa.

Soma pia: Kanuni 15 za Ujasiriamali Ambazo ni Lazima Uzifahamu

5. Tafuta na tumia mbinu mpya za masoko

Zama za kupanga bidhaa kwenye biashara yako na kusubiri wateja zimepitwa na wakati. Huu ni msimu mpya wa kubuni njia tofauti za kuuza bidhaa zako ili kumudu ushindani na kujitofautisha na wafanya biashara wengine walioko katika ushindani.

Tumia mbinu kama vile kutembeza bidhaa, kuwapelekea wateja moja kwa moja kule waliko, ununuzi wa bidhaa kwa kuwekeza, kuuza bidhaa kwa mtandao n.k.

6. Tumia nafasi ya teknolojia

Kwa hakika hakuna mtu ambaye aliwahi kufikiri kuwa kuna siku watu wangehimizwa kujitenga (social distancing) au watu kuacha kufika kazini badala yake wafanyie kazi zao nyumbani. Hiki ni kiashiria kikubwa kuwa kuna mabadiliko makubwa katika mfumo wa maisha na shughuli za kila siku ambayo hayawezi kukabiliwa pasipo matumizi makubwa na stahiki ya teknolojia.

Takwimu zinaonyesha kuwa biashara kwa njia ya mtandao imeongezeka kwa takriban asilimia 6 hadi 10 (UNCTAD) tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Corona.

Hivyo basi, itakuwa jambo la kusikitisha kama mfanyabiashara anataka kujikinga na athari za Corona kwenye biashara yake kisha akabaki katika mifumo ya zamani ya biashara na kupuuza nafasi ya teknolojia.

Soma pia: Makosa 8 ya Kuepuka Unapofanya Biashara Kwenye Mtandao

7. Tekeleza mipango kwa kujaribisha

Kwa kuwa hakuna anayejua kesho ni hali gani au jambo gani litatokea kutokana na kuibuka kwa msimu mpya ulioletwa na ugonjwa wa Corona, basi ni muhimu kwako mfanyabiashara kufanya maamuzi kwa kujaribisha kabla ya kutekeleza mpango kamili.

Hakikisha unajaribisha na kufanya utafiti vya kutosha juu ya mpango mkubwa unaotaka kuufanya katika biashara yako ili kuepusha hasara au matatizo mengine yanayoweza kutokea huko mbeleni.

Kwa mfano kama unataka kufungua ofisi mpya, ifanyie majaribio kwanza, kama unataka kununua bidhaa fulani kwa wingi au mpya fanya majaribio kuona ufanisi wake kwanza kabla ya kufanya mamuzi kamili. Kwa njiaa hii unaweza kujipa muda wa kufanya maamuzi ambayo siyo sahihi yanayoweza kugharimu biashara yako kwa kiasi kikubwa.

Hitimisho

Naamini kupitia mbinu hizi saba zilizoelezwa hapa wewe kama mfanyabiasha utakapozizingatia utaweza kwa kiasi kikubwa kukabili athari nyingi zinazotokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona. Jambo kubwa la msingi ni kuhakikisha kila mara unajifunza na unafanya maamuzi sahihi na kwa uangalifu mkubwa katika biashara yako ili iwe salama.

Je umeshaona athari za Corona kwenye biashara? Je unazikabili kwa mbinu gani au una mawazo gani juu ya haya yaliyojadiliwa hapa? Tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii kwa kubofya kitufe cha mtandao wako wa kijamii.

3 3 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x