Kuweka akiba ni kanuni mojawapo ya matumizi mazuri ya pesa. Hata hivyo kutokana na watu wengi kutokuwa na matumizi mazuri ya pesa, bado wengi wanashindwa kuweka akiba.
Baadhi ya watu hufikiri kuwa ili uweze kuweka akiba ni lazima uwe na pesa nyingi, lakini ukweli ni kuwa kuweka akiba ni maamuzi tu na siyo kuwa na pesa nyingi.
Ikiwa umekuwa ukipuuza suala la kuweka akiba na kuliona kuwa halina maana, basi fahamu faida 8 za kuweka akiba.
1. Uhuru wa kifedha
Uhuru wa kifedha ni zaidi ya kuwa na pesa, uhuru wa kifedha ni kuwa mtu ambaye unatakiwa kuwa maishani na kuweza kufanya au kupata kile unachokihitaji maishani.
Hata hivyo pesa ni muhimu sana kwenye swala la uhuru wa kifedha, ingawa pesa hizi zinatakiwa ziambatane na fikra sahihi.
Kwa njia ya kujiwekea akiba utaweza kujijengea msingi mzuri wa kifedha ambao ukiambatanishwa na fikra sahihi utakuletea uhuru wa kifedha.
2. Matumizi mazuri ya pesa
Kama nilivyoeleza hapo mwanzo kuwa kuweka akiba siyo kuwa na pesa nyingi bali ni maamuzi na mipango stahiki pekee.
Hivyo kuweka akiba kutakufaidisha kwa kukuwezesha kutumia pesa vyema. Ikiwa unapata elfu kumi kwa siku, itakubidi uitumie vizuri ili uweze kutenga fedha ya akiba.
Kama huweki akiba huna haja ya kutumia pesa vyema kwani hakuna sehemu ya akiba inayotakiwa kutengwa.
Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema
3. Kujiaandaa kwa dharura
Watu wengi huingia kwenye madeni au kupata uhitaji mkubwa wa pesa mara wapatwapo na dharura. Hivyo kwa kuweka akiba utapata faida ya kukuepushia mahangaiko wakati wa dharura kama vile maradhi, msiba, majanga, n.k.
Soma pia: Njia 10 za Kuepuka Madeni
4. Kuweza kufanya manunuzi au miradi ya gharama kubwa
Kuna manunuzi au miradi ambayo inahitaji pesa nyingi ili kuitekeleza. Maswala kama vile ujenzi wa nyumba, ununuzi wa kiwanja, kununua gari, n.k. ni baadhi ya mambo yanayohitaji fedha nyingi.
Hivyo, kwa kuwa na akiba utaweza kutekeleza mambo haya kwa urahisi zaidi kuliko ungeyafanya bila akiba.
Soma pia: Makosa 8 ya Kuepuka Kabla na Wakati wa Kujenga Nyumba
5. Kuweza kumudu wanaokutegemea
Ikiwa kuna watu wanaokutegemea kama vile wazazi, ndugu au watoto; ni vyema kuweka akiba ili uweze kuwa na fedha ya kukidhi mahitaji yao mara wapatwapo na uhitaji.
Kutokuweka akiba kutakufanya uhangaike huku na huko ukitafuta fedha za kukidhi mahitaji ya wategemezi wako kama vile chakula, matibabu au hata ada za shule.
6. Utulivu wa akili
Unapokuwa huna akiba yoyote huwezi kuwa na utulivu wa akili. Kila wakati unahofu na wasiwasi juu ya maisha yako, unajiuliza likitokea tatizo itakuaje? Au hitaji fulani linalokuja hivi karibuni litakuwaje? n.k.
Unapokuwa na fungu fulani la akiba huna haja ya kuwa na wasiwasi kwani unajua hata ukikosa fedha akiba yako itakusaidia.
7. Hukuwezesha kuandaa kesho vyema
Maandalizi ya kesho yanafanywa leo. Kuweka akiba maana yake unajiandaa kwa mahitaji ya kifedha ya baadaye — yaani kesho. Mtu asiyeweka akiba mara nyingi hafikiri kuhusu kesho wala hana malengo kwa ajili ya baadaye yake.
Ili kujenga baadaye au kesho njema, ni muhimu pia kuimarisha msingi wako wa kiuchumi kwa njia ya kuweka akiba.
Soma pia: Mambo 12 ya Kufanya kwa Ajili ya Kesho Yako
8. Hukuwezesha kuwahi fursa
Ni mara ngapi umekuwa ukisema au ukisikia kauli kama vile “Ningekuwa na pesa ningenunua hiki kitu”, “Ningekuwa na pesa ningejiunga kwenye hii huduma”, “Ningekuwa na pesa ningejiunga na huu mradi”, n.k.
Hili linadhihirisha kuwa watu hukosa fursa mbalimbali kutokana na kukosa akiba ya fedha. Unapokuwa na akiba ya fedha ni rahisi kuwahi fursa mpya au bidhaa zenye manufaa mara zinapopatikana.
Hitimisho
Fedha ni jambo linalohitaji nidhamu na busara ya hali ya juu; vivyo hivyo kuweka akiba ni swala linalohitaji kufanya maamuzi sahihi ili uweze kulitekeleza.
Baada ya kusoma makala hii, naamini sasa hutopuuza tena swala la kuweka akiba. Hakikisha hutumii akiba yako pasipokuwa na sababu ya msingi; tambua itakusaidia sana mbeleni wakati wa uhitaji.
Je wewe huwa unaweka akiba? Je unanufaika vipi kwa akiba yako?
Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Usisahau kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
Hii ni moja ya mada bora kuhusu kuweka akiba. Ahsante mwandishi kwa mada hii.
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Nafurahi sana kama ungeingia kiundani zaidi kwenye kuelezea kuhusu hii mada ✌
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Najaribu kujiwekea hakiba lakini nashindwa naomba msaada tafathali
Tutakuja na makala yenye muongozo wa kuweka akiba. Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Ni vizur kuwa na msaada kwa wat hat ktk jamii unayo ishi nayo
Hakika; Asante sana kwa maoni yako ya thamani kwetu; karibu sana Fahamuhili.com