Mambo 12 ya Kufanya kwa Ajili ya Kesho Yako - Fahamu Hili
Friday, September 29Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 12 ya Kufanya kwa Ajili ya Kesho Yako

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Fikiri kuhusu Muda ujao(kesho)

Ni mara ngapi umejiambia kuwa kesho itakuwa siku nzuri na unatamani kuiona na kuiishi? Ni mara chache sana. Hofu na mashaka vimetawala na kuchukua nafasi katika kesho za watu wengi. Jambo zuri kwenye maisha ni kuwa una nafasi ya kutawala mambo mengi yanayotokea katika maisha yako. Kama kesho inafanana na leo hakuna maana; ikiwa leo ulikuwa na huzuni basi angalau kesho iwe na furaha.

Hivyo kuna mambo ambayo unaweza kuyafanya leo na kuhakikisha kuwa kesho inakuwa nzuri. Hapa kuna mambo 12 ambayo unayoweza kuyafanya na kuifanya kesho yako kuwa nzuri na yenye tija.

1. Panga kwa ajili ya kesho.

Mpango mzuri leo ni bora kuliko mpango mkamilifu kesho.

George S. Patton

George anatukumbusha  kuwa maandalizi bora ya kesho hufanywa leo. Kuwa na mpango wa kesho leo kutakuwezesha kufanya mambo kwa kutegemea mwongozo na mpangilio uliopo badala ya kuamka na kufanya chochote kinachokuja mbele yako. Panga mambo ambayo unatakiwa kuyakamilisha kesho kwa kutegemea umuhimu wake.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda.

2. Fikiri kwa mawazo mapana

Ni vyema ukafahamu kuwa ni wapi ulipo leo na ni wapi unapotaka kwenda. Ni vyema ukatenga muda ukabainisha lengo lako la mbeleni; kama unataka kuwa msanii mkubwa, mwandishi, rubani, daktari au mwanasiasa basi bainisha. Hili litakusaidia kukuongoza kurudi kwenye lengo pale unapokuwa umeliacha. Ni vyema kila siku ukahakikisha unafanya kitu kwa ajili ya kulikaribia au kufikia lengo lako.

3. Tengeneza mpango wa pili (Plan B)

Maisha ni kama fumbo, yale uliyoyapanga leo yanaweza kesho yasiwe kama ulivyoyapanga. Hivyo ni vyema ukawa na mpango wa pili au mbadala pale ambapo mpango wa awali utakwama. Hili ni jambo ambalo watu waliofanikiwa na werevu (smart) hulizingatia sana kwani wanajua mpango mmoja ukikwama watatumia mpango wa pili.

Soma pia: Vitu 15 Vinavyofanywa na Watu Werevu (Smart).

4. Tambua mafanikio yako

Ni vyema ukatenga muda kutambua mafanikio uliyoyapata hata kama ni kidogo. Ni kweli kuwa hakuna mtu anayesema nimeridhika na mafanikio hivyo sitaki kufanikiwa tena, lakini ni vyema ukatambua mafanikio unayoyapata. Kutambua mafanikio ambayo umebarikiwa kuyapata kutakupa hamasa ya kufanya bidii zaidi ili kuyafikia mengine makubwa na mazuri zaidi.

5. Tambua vinavyokausha nguvu yako

Mara nyingi tumezungukwa na upinzani kutoka kwa watu na mazingira yanayotuzunguka. Inawezekana hakuna anayekuthamini, kukuunga mkono au hata kukutia moyo. Jifunze kuepuka watu na mazingira haya ili kulinda nguvu yako ambayo ungeweza kuitumia kufanya vitu vyenye tija zaidi kwa jili ya leo na kesho. Kama wanakusema, acha waseme; kama wanakudharau, waache wakudharau; wewe tazama malengo yako tu, ipo siku watakuelewa.

Soma pia: Aina 8 za Watu Ambazo ni Sumu za Kuepuka Maishani Mwako.

6. Ione kesho kwa mafanikio

Mara nyingi watu huona magumu kiasi cha kutoamini kuwa kunaweza kukatokea nuru kesho. Jifunze na jizoeze kuiona kesho kwa jicho au mtazamo wa mafanikio. Ikiwa utaona kesho njema kwa ajili yako basi ndivyo itakavyokuwa kwani kila kitu kinaanza kwanza kwenye fikra zako. Epuka kauli kama vile mimi ni maskini, mimi ni wa kuachwa, mimi ni wakufa tu n.k

7. Kuwa na shukurani kwenye maisha

Ni vyema ukawa mtu mwenye shukurani kwa ajili ya watu na maisha. Kuwa na shukurani kutakuwezesha kupokea mengi zaidi kesho kuliko ungekuwa mtu wa kulalamika na kulaumu. Ni vyema ukajifunza kushukuru hata kwa mambo madogo kwenye maisha yako. Kuna mtu anatamani kupata hata vile ulivyo navyo au kuwa kama wewe lakini hawezi. Ni vyema kushukuru hata kwa kuwa na uhai na afya njema.

Soma pia: Mambo 20 Yakushukuru Kwa Ajili Yake Kwenye Maisha.

8. Fanya yaliyo ya muhimu kwako

Ni rahisi kupelekwa huku na huko na mambo mengi kwenye maisha. Hivyo ni vyema ukatambua maisha ni zaidi ya mambo kama vile kupata hela nyingi au umaarufu. Ni lazima ufanye yale ambayo yana kuwezesha kufikia malengo na ndoto zako. Kama ni elimu basi tafuta elimu, kama ni maandalizi ya mazingira mengine basi yafanye. Kama unataka kuboresha kesho yako basi epuka kufanya mambo kwa sababu mwingine anafanya; ni lazima ukumbuke kuwa kuleta mabadiliko ni kufikiri na kuwa tofauti.

9. Usihamishie ofisi nyumbani

Hapa simaanishi kuwa usifanye chochote kiachohusiana na kazi yako nyumani, bali ujifunze kutenganisha ofisi na familia. Kama unataka kuwa na kesho nzuri ni lazima ujifunze namna bora ya kuweka vipaumbele. Watu wengi wameshindwa kutofautisha nafasi ya kazi/ofisi na familia. Wengi wamekuwa wakitumia muda wa familia kwa ajili ya kazi au wakitumia muda wa kazi kwa jili ya familia. Nimeshuhudia watu wakikosa hata muda wa malezi ya watoto kwa kigezo tu kuwa wana kazi nyingi. Ni wazi kuwa ni lazima kila kimoja kiwe na nafasi yake ili uweze kujenga kesho njema yenye mpangilio na utulivu.

10. Jifunze kusamehe

Katika jambo ambalo limekuwa gumu kwa watu wengi ni kusamehe na kusahau wale waliowakosea. Kumbuka kuwa kubeba maumivu na uchungu moyoni mwako hakutakuwezesha kuwa na kesho njema bali mbaya. Ni lazima ujaze nafsi na moyo wako furaha inayopatikana baada ya kusamehe; kwani kutosamehe kunaweza kusimuathiri aliyekukosea bali kukakuathiri wewe mwenyewe.

Soma pia: Sababu 9 za Kwanini Umsamehe Aliyekukosea.

11. Pumzika na burudika

Ni vyema ukafahamu kuwa kesho yako inategemea afya njema ya mwili na akili. Hivyo ni vyema ukatenga muda wa kutosha kwa ajili ya kupumzika na kuburudika. Kwa kufanya hivi mwili wako na akili vitajijenga na kujisafi kwa ajili ya kuanza kesho nzuri yenye tija na furaha.

Soma pia: Tabia 10 zitakazobadili maisha yako.

12. Sahau yaliyopita

Kuna usemi usemao “Yaliyopita si ndwele tugange yajayo”. Ni vyema ukajifunza kutoruhusu zamani yako kukushikilia kusonga mbele kuelekea kwenye kesho yako yenye mafanikio. Kumbuka kuwa huwezi kubadili jana wa juzi lakini unaweza kubadili kesho na kesho kutwa. Fanya yale yanayowezekana kubadili kesho yako na kamwe usiruhusu kurudishwa nyuma na kale yako.

Neno la Mwisho

Ni wazi kuwa matendo na maamuzi utakayoyafanya leo ndiyo yatakayo amua kesho yako. Ikiwa utafanya maamuzi na matendo sahihi leo basi ujue kuwa kesho yako pia itakuwa njema.

Je wewe una mipango gani kwa ajili ya kesho yako? Je umeshaanza kuchukua hatua leo? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine.

2.7 3 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

5 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Reginald
Reginald
3 years ago

12: sahau yaliyopita; kuhama na mawazo au matatizo ya Jana katika kuifikia kesho haswaaa hili husababisha kutofikia mafanikio Kwan tabia hii hulazimisha siku zifanane: NB THERE IS NO FUTURE IN THE PAST

Amani
Amani
7 months ago

Shukran

Abdallah
Abdallah
2 months ago

Thanks

5
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x