Vitu 15 Vinavyofanywa na Watu Werevu (Smart) - Fahamu Hili
Wednesday, February 28Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Vitu 15 Vinavyofanywa na Watu Werevu (Smart)

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Watu werevu (Smart)

Unaweza kujiuliza ni mambo gani yanayomfanya mtu kuwa mwerevu (smart). Je ni wingi wa maarifa anayoyafahamu? Au je ni kiwango cha wastani au cha juu cha kufikiri kwake? Ukweli ni kuwa ni werevu ni uwezo wa kufanya maamuzi yatakayofaa wakati wote; au ni kuweza kuibua kitu kizuri katika kitu kibaya au wakati mbaya. Watu werevu huweza kufanya maamuzi ambayo yanazingatia matokeo ya mbeleni ya maamuzi hayo.

Ni dhahiri kuwa watu werevu (smart) ni tofauti na watu wengine kutokana na yale wanayoyafanya au kutofanya. Fahamu mambo 10 ambayo watu werevu hawayafanyi.

1. Hawapuuzi uwekaji akiba

Katika maisha ya kiuchumi kuna vipindi viwili; kipindi cha mavuno(shibe) na kipindi cha ukame(njaa). Ni watu wachache sana ndio wanaoweza kuishi katika vipindi hivi viwili bila shida. Watu werevu hawapuuzi swala la kuweka akiba hata kidogo, kwani wanafahamu kuna kipindi watahitaji akiba hizo ziwasaidie kuishi maisha yao ya kawaida bila tatizo. Hivyo basi, unatakiwa kujifunza kuweka akiba ili uweze kuishi kipindi cha ukame bila shida.

2. Hawategemei tu watu wengine

Ni kweli kuwa duniani tumeumbwa kushirikiana na kutegemeana, lakini si kwa kila kitu. Ni wazi kuwa, watu werevu wanafahamu umuhimu wa kusimama wao kama wao na si kutegemea watu wengine kwa kila kitu. Unapotegemea watu wengine kwa kila kitu ni wazi kuwa hutoweza kufikia malengo yako kwani si wote watakaokuunga mkono ipasavyo.

Soma pia: Aina 8 za Watu Ambazo ni Sumu za Kuepuka Maishani Mwako.

3. Hawaishi kama wasio na cha kufanya

Mara nyingi watu hupenda kujishughulisha pale wanapopangiwa majukumu au wanaposimamiwa na mtu mwingine. Lakini hali ni tofauti kwa watu werevu kwani wao hujipangia majukumu yao na kujisimamia wenyewe. Mara nyingi utawaona watu werevu wakiandika, wakisoma vitabu na makala mbalilimbali, wakisikiliza hotuba, n.k. Ilimradi tu wawe na cha kufanya. Jifunze kuwa mtu mwenye tija kwa kuishi maisha ya watu werevu; usiishi kama huna kitu au kazi za kufanya.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda.

4. Hawabaki kwenye makosa yao

Ni kweli umefanya kosa fulani na pengine athari zake unaziona katika maisha yako. Lakini hebu jifunze kutokana na makosa na si kubaki katika hali mbaya ya kosa ukijilaumu, ukilalamika na hata ukijihukumu. Watu werevu hutumia makosa kama shule ya kuwafundisha kufanya mambo bora zaidi mbeleni na si kubaki katika makosa yao.

5. Hawaruhusu zamani zao ziwashikilie

Kama ilivyo katika hoja ya kutoruhusu kubaki kwenye makosa, ndivyo ilivyo pia katika kutoruhusu zamani yako kukushikilia. Tambua ya kale yamepita, na hauwezi kuibadilisha jana ila unaweza kuibadilisha kesho. Ulikuwa na msingi mbovu kiuchumi katika familia, hukusomeshwa vyema n.k ni baadhi tu ya hali za zamani ambazo haupaswi kuziruhusu kukuathiri. Watu werevu wanafahamu wazi athari za kuruhusu zamani zao kuwashikilia, hivyo wao hufanya kila jitihada kujinasua.

6. Hawategemei bahati kufanikiwa

Ni wazi kuwa wapo watu waliofanikiwa kibahati tu katika maisha, lakini hili si jambo la kutegemewa. Watu werevu hawaishi maisha ya kusubiri kushinda Bingo au bahati nyingine ili wafaulu kimaisha au watimize ndoto zao. Watu hawa hufanya kazi kwa bidii wakijua kuwa katika juhudi ndiko hutoka mafanikio. Hivyo nakuhamasisha kuacha fikra finyu za kungoja “dili” au “jiwe” ili ufanikiwe.

7. Hawapuuzi mambo ya muhimu kwenye biashara zao

Nimeshuhudia wafanyabiashara wengi wa Kiafrika wakibweteka na kupuuza mambo ya msingi kwenye biashara zao. Maswala kama vile kujali wateja, kutunza taarifa za kibiashara, kuboresha huduma n.k. ni mambo ambayo watu werevu huyapa kipaumbele. Hivyo ni vyema ukajifunza kutokupuuza mambo ya msingi katika kazi au biashara yako.

Soma pia: Makosa 15 Ambayo Kila Mjasiriamali Anatakiwa Kuyaepuka.

8. Hawasiti kusema hapana

Watu werevu wanajua nguvu iliyoko katika jibu la “Hapana”. Je, wajua kuwa hapana ni jibu rahisi au dogo sana lakini lina nguvu kubwa? Usikubali kuwa mtu anayepokea na kukubaliana na kila kitu. Kwa mfano twende sokoni, unaenda; twende disko, unaenda; kunywa pombe, unakunywa; nakupenda, unakubali; twende tukatembee unaenda; vuta bangi, unavuta n.k. Jifunze kusema hapana hata kama hutamfurahisha unayempa jibu hilo. Watu werevu wanajua kuwa jibu la hapana litawatenga na watu na mipango isiyo sahihi kwenye maisha yao.

Soma pia: Tabia 10 zitakazobadili maisha yako.

9. Hawaachi mawazo yao kwa kuwa hayakubaliwi na wengine

Mara nyingi tunapokuwa na wazo au mpango si rahisi kukubaliwa na kila mtu. Wengine watakupinga kwa ajili ya wivu, chuki au kutokana na uwezo wao mdogo wa kufikiri. Kwa kulifahamu hili watu werevu hawaachi mawazo yao kwa kuwa tu yamepingwa na watu wengine. Wao huyafanyia kazi mawazo yao kwa kutazama malengo yao na hatimaye hufanikiwa.

10. Hawapuuzi vifaa vyao vya kielektroniki

Hivi leo watu wengi wanamiliki simu za kisasa au kompyuta. Vifaa hivi vina matumizi mbalimbali, yenye tija na na yasiyo na tija. Watu werevu hawaachi kutumia vifaa vyao katika mambo yenye manufaa kwao. Watu hawa huvitumia kujifunza, kufanya kazi mtandaoni na hata kuwasiliana kwa maswala ya msingi. Kwa hiyo hata wewe unaweza kutopuuzia manufaa yaliyoko katika vifaa vyako vya kielektroniki kama ilivyo kwa watu werevu.

11. Hawatengenezi maadui wasiokuwa na sababu

Watu werevu wanajua si wote hupenda mafanikio; wengine hujenga uadui ili kukurudisha nyuma. Mara nyingi maadui hujitokeza katika maisha, hasa pale unapofanya mambo ya maendeleo yenye kukinzana nao. Lakini kuna maadui ambao unaweza kuwazuia; jitaidi kuondoka au kuachana na wale watu wanaotaka kutengeneza shari bila sababu. Pia unaweza kubadili jambo au kuliacha kwa muda ili kuepuka kutengeneza maadui wasiokuwa na ulazima. Zingatia pia kusamehe na kuwafanyia mambo mema wale waliokufanyia mabaya.

Soma pia: Sababu 9 za Kwanini Umsamehe Aliyekukosea.

12. Hawajikwezi

Unyenyekevu na hekima ni karama adimu hasa kwa watu wanaoibukia katika mafanikio. Lakini watu werevu wanajua umuhimu wa kunyenyekea na kutojikweza. Unyenyekevu hukupa nafasi ya kufanya bidii zaidi kwani hujioni kuwa umefika. Pia unyenyekevu hukuweka karibu na watu wote; kwani hutomdharau au kumpuuza mtu yeyote.

13. Hawategemei kitu kimoja

Kuna usemi usemao “usiweke mayai yote kwenye kikapu kimoja” usemi huu unafahamika vyema sana na watu werevu. Watu werevu huwa hawategemei kitu kimoja pekee; yaani kitu kimoja kikishindwa wao nao wameshindwa. Jifunze kuwekeza katika mambo mbalimbali ili moja likikwama basi lingine liendelee.

14. Hawajidanganyi kuwa mambo ni rahisi

Safari ya mafanikio ina milima na mabonde. Kujidanganya kuwa mambo ni rahisi na hakuna changamoto zozote ni tatizo kubwa. Watu werevu wanajua mambo siyo rahisi, wanafahamu kuwa watakutana na changamoto hivyo hujiandaa kuyakabili.

Soma pia: Hatua 7 za Maumivu Zisizoepukika Kabla ya Kufanikiwa.

15. Hawatengenezi mathara au hatari zisizokuwa na sababu

Inawezekana una fedha fulani za ziada, kila unachosikia na kuona unataka kuweka pesa zako. Huku ni kujitengenezea hatari zisizokuwa na sababu. Siyo muhimu pia, kuhusiana na kila mtu kwani siyo wote wanakufaa; wengine ni kujitengenezea hatari au madhara yasiyokuwa ya lazima. Jambo hili linafahamika vyema kwa watu werevu; hivyo hawajitengenezei hatari zisizokuwa za ulazima ili kuhakikisha kuwa wanafikia malengo yao.

Hitimisho

Naamini umebaini kuwa maisha ya watu werevu (smart) ni tofauti sana na watu wa kawaida. Pia umebaini kuwa wamedhubutu kufanya mambo ambayo hayajazoeleka kwa watu. Hivyo, na wewe unaweza kufanya uamuzi leo wa kubadili tabia na mwenendo wako ili uwe mtu mwenye tija zaidi. Jiwekee maleko, tunza muda na fanyia kazi maono na ndoto zako.

Je wewe ni mtu mwerevu? Au je, ungependa kuwa mtu mwerevu? Tuandikie maoni yako kisha washirikishe wengine.

3.7 3 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

4 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Faustin magome
Faustin magome
4 years ago

Mnaelimisha vizuri sana

Green
Green
4 years ago

Nakuelewa Sana Kornelio

4
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x