Mambo 10 Unayoweza Kujifunza Kutoka kwa Lionel Messi - Fahamu Hili
Friday, September 29Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 Unayoweza Kujifunza Kutoka kwa Lionel Messi

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Lionel Messi akiwa amebeba kombe

Lionel Messi alizaliwa tarehe 24 Juni 1987 huko Rosario, Jimbo la Santa Fe huko Argentina. Akiwa na miaka mitano Messi alianza kucheza mpira wa miguu kwenye klabu ya Grandol iliyokuwa ikifundishwa na baba yake.

Wakati Messi akiwa mdogo, alibainika kuwa na tatizo au maradhi ya kuwa na upungufu wa seli za ukuaji. Akiwa na umri wa miaka 13 alihamia Uhispania na kujiunga na klabu ya Barcelona ambayo ilikubali kugharamia matibabu yake.

Pamoja na changamoto alizokuwa nazo Messi amefanikiwa kupata mafanikio makubwa sana. Messi anachukuliwa kama mchezaji bora zaidi duniani na mmoja kati ya wachezaji bora waliowahi kuwepo.

Messi ni mchezaji pekee aliyeshinda tuzo ya FIFA ya Ballon d’Or  mara tano, zikiwemo nne mfulilizo. Pia ni mchezaji pekee aliyeshinda tuzo ya kiatu cha dhahabu (European Golden Shoes) mara nne.

Natumaini unafahamu umuhimu wa kujifunza kwa waliofanikiwa; hivyo soma mambo 10 unayoweza kujifunza kutoka kwa Messi.

1. Pigania ndoto zako

“Unatakiwa kupambana kufikia malengo yako. Unatakiwa kujitoa na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya mfanikio yako”

Lionel Messi

Messi anatukumbusha kuwa kama una ndoto, unatakiwa ufanye kazi kwa bidii kuzifikia. Mafanikio hayaji kwa urahisi. Kuna gharama ambayo ni lazima uilipe na uwe tayari kuilipa.

Watu wengi hawafanikiwi kwa sababu hawataki kufanya vitu ambavyo vitawafanya wazalishe matokeo yasiyo ya kawaida.

Ni lazima uende zaidi, maili moja zaidi, uweke jitihada zaidi, uamke mapema na kuchelewa kulala kwa kuhakikisha tu unafikia ndoto zako.

2. Mafanikio huchukua muda

“Ilinichukua miaka 17 na siku 114 kuwa na mafanikio yanayojulikana kama ya usiku mmoja”

Lionel Messi

Hii ni nukuu ninayoipenda kutoka kwa Lionel Messi. Inanikumbusha kuwa mafanikio ni mchakato wa muda mrefu na sio jambo la usiku mmoja.

Acha kutafuta njia ya mkato, au mfumo wa kupata utajiri wa haraka. Rumi haikujengwa kwa siku moja, wala Steve Jobs hakuanza kampuni ya Apple kwa usiku mmoja.

Kwa hiyo, jikite kufanyia kazi ndoto zako bila kuchoka, safari haitakuwa rahisi, lakini matokeo yake yatakuwa ya kushangaza.

3. Fanya unachokipenda

“Ninachokifanya ni kucheza mpira wa miguu, ambacho ndicho kitu ninachokipenda”

Lionel Messi

Je umesikia hilo? Watu mashuhuri wanazalisha matokeo yakushangaza kwa sababu wanafanya kile wanachokipenda. Unapopenda kile unachokifanya, ni wazi kuwa utafanya kazi nzuri. Michael Jordan asingefanikiwa kwenye mpira wa kikapu kama asingekuwa anapenda mchezo huo.

Warren Buffett ametengeneza mabilioni ya dola kutokana na uwekezaji, kwa kuwa anapenda sana kazi hiyo.

Unatakiwa nawe uwe hivyo kama unataka kutengeneza matokeo ya kustaajabisha kwenye maisha yako.

4. Maboresho yanawezekana

“Siku unayofikiri kuwa hakuna mabadiliko yanayoweza kufanyika, ni siku ya huzuni kwa kila mchezaji”

Lionel Messi

Ni lazima ujikite kwenye maboresho kila siku. Kama wewe ni mjasiriamali, unahitaji kuboresha maarifa na ujuzi wako wa ujasiriamali. Njia pekee ya kuwa bora katika kile unachokifanya, ni kufanya maboresho kila siku.

Fanya kitu kitakachokufanya kuwa bora zaidi kila siku. Soma vitabu na makala (kama hii unayosoma), pia sikiliza watu watakaokujenga na kukupa hamasa kila siku.

5. Usiendeshwe na pesa

“Pesa siyo chanzo cha hamasa. Pesa hazinizuzui wala kunifanya nicheze vizuri kwa sababu kuna manufaa ya kuwa tajiri. Ninafurahi ninapokuwa na mpira mguuni mwangu. Hamasa yangu inatokana na kucheza mchezo ninaoupenda. Kama nisingekuwa nalipwa kwa kucheza kama mchezaji mashuhuri, ningekuwa tayari kucheza bila kulipwa chochote”

Lionel Messi

Messi anafahamu hasara za kuendeshwa na pesa. Ni wazi kuwa pesa ni alama zinazopatikana kutokana na kuishi ndoto zako.

Watu wengi hawafanikiwi kwa sababu wanatazama tu pesa; wanasahau kuwa pesa ni matokeo ya kuzifanya ndoto zako ziuzike kwa watu wengine.

Tambua mambo ya msingi yatakayokuwezesha kufikia malengo yako. Acha kukimbilia vitu vinavyong’aa kwani wewe siyo kama wengine. Fanyia kazi mawazo uliyo nayo, tatua matatizo ya watu na pesa zitakujia bila shida.Lionel Messi pamoja na mwenzi wake Antonella Roccuzzo wakati wa harusi yao.

6. Usisahau vitu vya muhimu

“Kuna vitu vya muhimu zaidi maishani kuliko kushinda au kushindwa mchezo”

Lionel Messi

Ni dhahiri unaweza kujifunza kutoka kwa Messi kuwa kuna wakati kwenye maisha tunazingatia mambo fulani zaidi na kuyasahau yale ya msingi. Mambo kama vile kazi, miradi na pesa vina nafasi yake lakini havitakiwi kuchukua nafasi ya ndugu, jamaa, marafiki na familia.

Nimeshuhudia watu wanaojiita ni wajasiriamali wakiangamiza ndoa na familia zao kwa kukosa muda wa kuwa karibu au kuzihudumia. Ni lazima ubainishe mambo ya muhimu zaidi kwenye maisha yako ili uwe mwenye tija zaidi.

7. Kuacha ubinafsi

“Mwaka unapoanza lengo ni kushinda kama timu, rekodi binafsi ni swala la ziada”

Lionel Messi

Messi anafahamu madhara ya ubinafsi kwenye maisha na soka. Ni dhahiri kuwa watu wengi hawafanikiwi kwani hutazama mambo yao wenyewe. Nimeshuhudia biashara na miradi mingi ikifa kutokana na ubinafsi.

Kwa mfano watu wanapatana kuanzisha mradi au biashara kwa pamoja, baada ya kupata mafanikio kila mtu anakimbia kuanzisha ya kwake na hatimaye zote zinakufa. Ni wazi kuwa ni lazima kujikita kwenye malengo yenu kama kundi au timu ili muweze kufanikiwa.

Siku zote jiwekee kauli mbiu hii “Mwingine kwanza, mimi baadaye”.

8. Jifunze kukubali kushindwa

“Wakati mwingine ni lazima ukubali kuwa huwezi kushinda wakati wote”

Lionel Messi

Lionel anatukumbusha kuwa hakuna mtu au watu wanaoweza kushinda kila wakati. Wakati mwingine tunaendelea na kujifunza kutokana na kushindwa. Haupaswi kujisikia vibaya na kukata tamaa pale unaposhindwa. Hii ni sehemu ya mzunguko; jua haliwezi kuwaka siku zote, ni lazima mvua inyeshe pia.

Unaposhinda fanya bidii kuendelea mbele. Unaposhindwa pia, fanya bidii zaidi kuendelea mbele huku ukijifunza kutokana na makosa.Messi akicheza kwenye fainali za kombe la FIFA 2014

9. Uaminifu

Hivi leo uaminifu ni bidhaa adimu ambayo hauwezi kuipata kirahisi. Ni dhahiri kuwa kuna somo kubwa la kujifunza kutoka kwa Lionel Messi kuhusu uaminifu aliouonyesha kwa klabu yake ya Barcelona.

Messi amekuwa akichezea klabu ya Barcelona zaidi ya miaka 12 licha ya kuitwa na klabu nyingine kwa ahadi za fedha nyingi. Ni wazi kuwa Messi alifahamu kuwa uaminifu na upendo wa dhati kwa klabu yake ungemjenga zaidi kisoka kuliko kuhamahama.

Ni muhimu kujifunza na kujizoesha kuwa mwaminifu kwa mambo yote. Kama umekabidhiwa mali au biashara ya mtu mwingine ni vyema ukaisimamia kwa uaminifu ili nawe uweze kupata ya kwako.

10. Kuamini unaweza na inawezekana

“Hakuna shaka, kwa hakina nitafikia asilimia 100”

Lionel Messi

Bila shaka watu wenye malengo na maono wanaamini kuwa wanaweza kufikia asilimia 100 ya malengo na maono yao. Lionel Messi analifahamu hili vyema na anaamini kuwa kwa kiasi fulani anaweza kufikia asilimia 100 ya mafanikio yake.

Jitahidi kubadili kufikiri kwako na kuamini kuwa unaweza kufikia na kuishi ndoto zako

Soma pia: Dondoo 5 za Kuishi Ndoto Zako.

Hitimisho

Natumaini umejifunza mengi kutoka kwa mwanasoka mashuhuri ulimwenguni Lionel Messi. Ni matumaini yangu umefahamu pia ni kwa namna gani ni muhimu kubadili fikra na mtazamo wako. Ni wazi kuwa umeona pia umuhimu wa kujiwekea malengo na kuyafuata.

Anza leo, unaweza, kuna kufanikiwa kulikofichwa ndani yako. Usiogope changamoto kwani hata Lionel Messi alikuwa na maradhi ambayo yalihitaji matibabu ya zaidi ya dola 900 kwa mwezi lakini hayakumzuia.

Naamini kuna nukuu au jambo ambalo umelipenda zaidi katika makala hii. Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine.

2.3 4 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

6 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
James
James
3 years ago

Napenda sanaa makala yako

James
James
3 years ago

Naomb makala mengine juu sehemu mbalmbal

mtegwajnr
mtegwajnr
3 years ago

Nimezipenda sana Makala zako. Uko vizuri sana.

6
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x