
Kwa mujibu wa Forbes 2017, Bill Gates ndiye mtu tajiri zaidi duniani akiwa na utajiri unaokadiriwa kuwa dola za Marekani bilioni 86. Bill Gates ndiye mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya Microsoft.
Microsoft ni kampuni iliyotengeneza programu endeshi (operating system) maarufu na mashuhuri sana duniani ya Window. Kampuni hii pia inazalisha bidhaa nyingine kama vile vifaa vya michezo ya kielektroniki, pogramu mbalimbali pamoja na vifaa vingine vya kiteknolojia.
Kwa hakika Bill Gates ni mtu aliyefanikiwa sana ambaye kila mtu anayetaka kufanikiwa anaweza kujifunza mambo kadhaa kutoka kwake.
Kwa kutambua umuhimu wa kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, karibu nikushirikishe mambo 12 unayoweza kujifunza kutoka kwa Bill Gates.
1. Anza mapema kadri iwezekanavyo
Bill Gates alianza kujishughulisha na maswala ya kompyuta alipokuwa na umri wa miaka 13. Hili linatupa somo muhimu la kuanza mambo mapema.
Unapoanza jambo mapema unajijengea uwezo zaidi wa kukomaa kwenye jambo husika; pia kwa kuanza jambo muda mrefu unajijengea uzoefu ambao utakukinga dhidi ya kukata tamaa.
2. Hutakuwa tajiri mara baada ya kumaliza shule
Bill Gates alifahamu kuwa hawezi kupata pesa kwa kiwango kizuri mara baada ya kuhitimu elimu yake ndiyo maana akaamua kuacha Chuo.
Siku hizi haijalishi mtu ana cheti kizuri kiasi gani, hatoajiriwa kuwa mkurugenzi wa kampuni ya kimataifa au kupata kazi nyingine kubwa kabla ya kujenga uzoefu.
Hili ni somo zuri ambalo kila mhitimu au msomi anaweza kulitafakari ili limsaidie katika kufanya maamuzi.
3. Fanyia kazi ndoto zako
“Jenga ndoto zako wewe mwenyewe, la sivyo mtu mwingine atakuajiri kujenga zake.”
Bill Gates alianza kufanyia kazi ndoto zake yeye mwenyewe mapema bila kujali changamoto wala vikwazo.
Soma pia: Dondoo 5 za Kuishi Ndoto Zako.
4. Kujifunza kutokana na makosa
“Ukiharibu, siyo kosa la wazazi wako. Kwa hiyo usilie kutokana na makosa yako bali jifunze kutokana na makosa hayo.”
Makosa ni shule nzuri sana inayotuwezesha kuboresha maisha na ufanisi wa kile tunachokifanya. Bill Gates anatukumbusha umuhimu wa kujifunza kutokana na makosa.
Tunapokosea ni muhimu kujifunza kutokana na makosa hayo ili wakati mwingine yasitokee tena.
Soma pia: Mambo 25 Unayoweza Kujifunza Kutokana na Makosa.
5. Kujitoa na kuwa na subira
Ni wazi kuwa mafanikio ya Bill Gates hayakuwa ya usiku mmoja wala rahisi kuyapata. Ni ukweli usiopingika kuwa alifanya kazi kwa bidii kwa miaka mingi bila kukata tamaa wala kukosa uvumilivu.
Tunakosa vitu vingi kwenye maisha yetu kutokana na kutokujitoa pamoja na kukosa uvumilivu katika yale tunayoyafanya.
6. Televisheni siyo maisha halisi
Mara nyingi tumekuwa tukiona watu wakiishi maisha ya kifahari au anasa mbele ya kamera. Lakini uhalisia wa maisha hauko hivyo, maisha yana changamoto na inatupasa kuzikabili.
“Televisheni siyo maisha halisi. Kwenye maisha halisi watu wanatakiwa kuacha migahawa ya kahawa na kwenda kazini.”
7. Maisha hayana usawa
Haijalishi unafanya kazi kwa bidii kiasi gani, wakati mwingine mambo yanaweza yasiende kama unavyotarajia.
Bill Gates anatukumbusha kuwa hakuna watu walioandikiwa kufanikiwa au kupata kitu fulani. Hivyo wakati mwingine inabidi tukubaliane na hali halisi.
“Maisha hayana usawa. Kubaliana nayo.”
8. Kuwa tayari kukabili hatari
Kuanzisha biashara ni jambo lenye changamoto au hatari nyingi. Unaweza kuwa na pesa nyingi pamoja na wazo zuri la biashara, lakini ukaishia kupata hasara.
Bill Gates anatukumbusha kuwa biashara ni kuthubutu kuchukua au kukabili hatari au changamoto.
“Biashara ni mchezo wa pesa wenye kanuni chache na hatari nyingi.”
9. Hakuna njia ya mkato ya mafanikio
Watu wengi hujidanganya kuwa kuna njia ya mkato ya kufanikiwa au kupata pesa. Katika uhalisia, hakuna kitu cha namna hii katika mafanikio.
Bill Gates alianza Microsoft miaka mingi iliyopita pamoja na rafiki yake Paul Allen hadi leo hii alipokuwa tajiri wa kwanza duniani.
“Uvumilivu ni kipengele muhimu cha mafanikio.”
10. Jikubali ulivyo
Watu wengi wanakosa furaha pamoja na kushindwa kufikia malengo yao kutokana na kutokujikubali wao wenyewe. Bill Gates anatukumbusha kutokujilinganisha na watu wengine, kwani kwa kufanya hivo tunajifanya kuwa duni sisi wenyewe.
“Usijifananishe na mtu yeyote katika ulimwengu huu… ikiwa unafanya hivyo, unajidunisha mwenyewe.”
Soma pia: Njia 10 za Kukufanya Kuwa na Furaha.
11. Kuwa mnyenyekevu
Maisha ni kama gurudumu au foleni, maisha hayatabiriki, unaweza kuwa juu leo kesho ukawa chini. Ni muhimu kunyenyekea na kuwaheshimu watu hata kama una mafanikio makubwa.
“Mafanikio ni mwalimu dhaifu. Yanawapotosha watu werevu (smart) na kuwafanya kufikiri kuwa hawawezi kushindwa.”
12. Shiriki mafanikio yako na wengine
Dunia hii ya leo watu wamekuwa wabinafsi sana. Watu hawapendi kushirikisha mafanikio yao kwa watu wengine au hata kuwasaidia watu wengine wafanikiwe.
Bill Gates amekuwa ni mfano mzuri wa watu ambao wanawasaidia watu wengine kupitia mafanikio yao. Amekuwa akitoa maarifa kwa wajasiriamali wanaoanza pamoja na kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali.
“Tunapotazama karne mpya, viongozi watakuwa wale wanaowawezesha wengine.”
Neno la mwisho
Kwa hakika kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa watu waliofanikiwa ikiwa tunataka kufanikiwa. Kazi iliyobaki ni kuweka kwenye matendo mambo yaliyoelezwa kwenye makala hii ili tutimize ndoto zetu.
Soma pia: Nukuu (Quotes) 30 za Mafanikio Zitakazokuhamasisha.
Je una maoni yoyote? Tafadhali tuandikie hapo chini. Usisahau kuwashirikisha wengine makala hii pamoja na kujiunga nasi kwa barua pepe au kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.