
Chanzo cha picha: https://i.eurosport.com
Mchezo wa mpira wa miguu ulianza takriban kati ya karne ya 2 na ya 3 KB huko China. Mchezo huu umejizolea umaarufu mkubwa na kuwa chanzo cha kipato kwa watu wengi.
Mpira wa miguu ni mchezo unaopendwa na watu wengi duniani, inakadiriwa kuwa mchezo huu una mamilioni ya mashabiki kote duniani.
Kumeshuhudiwa mashabiki wa mpira wa miguu wakijitoa kwa dhati kushabikia timu zao; jambo hili limewagharimu pesa, muda au hata uhai wao.
Kwa mtu yoyote mwenye shauku ya kupata maarifa, anaweza kujifunza kitu kutoka kwa mashabiki wa mpira wa miguu; Ikiwa unapenda maarifa, basi karibu nikufahamishe mambo 6 unayoweza kujifunza kutoka kwa mashabiki wa mpira wa miguu.
1. Mapenzi ya dhati
Huwezi ukakosa swala la mapenzi ya dhati kwa timu pamoja na mchezo wenyewe kwa shabiki yeyote yule wa mpira wa miguu.
Mashabiki wa mpira wa miguu wameonyesha mapenzi makubwa kwa ajili ya timu zao kiasi cha kuzitaja na kuzielezea hadharani, kuzichangia, kumiliki vitu vinavyotangaza timu husika, kutoa muda wao, n.k.
Kwa hakika unaweza kujifunza kupenda na kufanya kwa moyo kitu chochote unachokifanya ili kifanikiwe.
2. Kukosa aibu
Shabiki halisi wa mpira wa miguu kuvua nguo uwanjani au kupiga kelele za kushangilia siyo jambo la aibu. Kila shabiki halisi hufanya kila analoweza bila kujali aibu ili tu ahamasishe timu yake kushinda kwa njia ya kuishangilia.
Kwa hakika katika maisha ya kawaida pia ni muhimu kutokuona aibu katika kutekeleza mambo mbalimbali ili tufanikiwe.
Kumbuka kuwa wapo watu walioanza kufanya kazi za aibu lakini sasa wana kazi na maisha mazuri kwa sababu hawakuona aibu kufanya kazi zinazoonekana kuwa ni za aibu.
3. Kuwa mtafiti
Kila mara utawakuta mashabiki wa mpira wa miguu wakiwa karibu na redio, televisheni au intaneti ili kuchunguza na kupata taarifa mbalimbali zinazohusu timu mbalimbali, wachezaji, uchambuzi, utabiri wa matokeo, n.k.
Kuna mtu anaweza kukuelezea mambo ya timu za Ulaya hadi ukafikiri naye yuko huko au ametoka huko hivi karibuni; lakini hii ni kutokana na kutafiti bila kuchoka juu ya maswala ya mpira wa miguu.
Pasipo shaka unaweza kujifunza juu ya kuwa mtafiti kutoka kwa mashabiki wa mpira wa miguu ili uongeze maarifa yako.
Kumbuka kadri unavyokuwa na maarifa ya kutosha katika kile unachokifanya ndivyo unavyoongeza nafasi ya kufanikiwa zaidi.
4. Imani ya kushinda
“Kwa kawaida tunakuwa kile tunachoamini au kufikiri.”
Haijalishi timu imeshindwa mara ngapi au imekosa viungo muhimu wangapi, bado mashabiki wataamini kuwa timu yao itashinda.
Ni muhimu kuwa na imani ya kufanikiwa au kushinda katika jambo lolote tunalolifanya ili lifanikiwe hatakama kuna changamoto nyingi.
Soma pia: Hatua 7 za Maumivu Zisizoepukika Kabla ya Kufanikiwa
5. Juhudi na kujitoa
Mashabiki wa mpira wa miguu hukesha, hulipa pesa au hata kusafiri umbali mrefu ili kushuhudia timu yao ikicheza. Hawajali gharama wala maumivu, wao hujitoa kwa moyo na kwa juhudi nyingi ili kuishuhudia na kuiwezesha timu yao kushinda.
Hakuna jambo lolote linaloweza kufanikiwa bila juhudi na kujitoa. Ni muhimu kujifunza jambo hili na kuliweka katika matendo kwenye yale unayoyafanya. Fanya kazi kwa bidii usiku na mchana hadi uone malengo yako yakitimia.
Soma pia: Faida 8 za Kufanya Kazi Kwa Bidii Unazotakiwa Kuzifahamu
6. Kujali muda
Hakuna shabiki wa mpira wa miguu anayetaka kuchelewa kwenye mpira. Nakumbuka wakati nikiwa chuoni watu walikuwa wakiwahi viti kwenye ukumbi wa mpira saa mbili kabla ya mpira kuanza.
Mashabiki wa mpira wa miguu hufanya kazi zao mapema na kwa juhudi ili wasije wakachelewa au kazi hizo zikawazuia kutazama mchezo wa timu zao.
Kwa kuwa kila jambo limefungwa kwenye muda; ni muhimu kuhakikisha unazingatia matumizi mazuri ya muda ili ukamilishe malengo yako. Usipoteze muda kwenye mambo yasiyokuwa na msingi wowote.
Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda
Hitimisho
Naamini umejifunza mengi kutoka kwa mashabiki wa mpira wa miguu kupitia makala hii. Kwa hakika ili tufanikiwe na tufikie malengo yetu, ni muhimu kuhakikisha tunafanya kazi kwa bidii, hatukati tamaa, pia tunatumia muda vyema.
Je wewe ni mshabiki wa mpira wa miguu? Je unanufaika vipi na mchezo huo katika kufikia malengo yako? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.