Faida 8 za Kufanya Kazi Kwa Bidii Unazotakiwa Kuzifahamu - Fahamu Hili
Tuesday, June 6Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Faida 8 za Kufanya Kazi Kwa Bidii Unazotakiwa Kuzifahamu

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Bidii

Kuna fikra potofu zimejengeka miongoni mwa watu wakidhani kuwa kufanya kazi kwa bidii ni utumwa. Hii ni kutokana na dunia ya sasa kujaa watu wasiopenda kazi na wavivu.

Kwa hakika kufanya kazi kwa bidii kuna manufaa mengi sana ambayo watu wengi hawayajui. Huu ni wakati wa kubadili mtazamo wako juu ya kufanya kazi kwa bidii kwa kufahamu faida 8 za kufanya kazi kwa bidii.

1. Utaweza kutumia muda vyema

Huwezi kutumia muda vyema kama hutofanya kazi kwa bidii. Ukiwa na bidii katika kufanya kazi, unaweza kufanya kazi za siku nzima ndani ya saa moja au kazi za siku mbili ndani ya siku moja.

Hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa bila kutumia muda vyema; muda ni mali, hivyo yakupasa uutumie vyema kwa kufanya kazi kwa bidii.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda

2. Kufikia malengo yako

Kanuni moja wapo ya kufikia malengo ni kufanya kazi kwa bidii. Safari ya mafanikio siyo ya mteremko, inahitaji juhudi nyingi ili tuweze kuona matokeo.

Hakuna mtu aliyewahi kufanikiwa kwa kufanya kazi kivivu; fuatilia watu waliofanikiwa watakueleza jinsi wanavyofanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ndoto zao.

Soma pia: Tabia 10 Unazotakiwa Kijifunza Kutoka kwa Watu Waliofanikiwa

3. Kuheshimika

Nani atamheshimu mvivu? Kwa hakika hakuna. Mtu anapokuwa mwenye bidii utasikia kauli kama vile huyo hapendi mchezo, akishaingia kwenye kazi zake humpati, hageukagi nyuma kwenye kazi huyo, kama huyo yupo hiyo kazi lazima iishe, n.k.

Hizi ni baadhi ya kauli zinazoonyesha kuheshimiwa kwa mtu husika kutokana na kufanya kazi kwa bidii. Ikiwa unataka kuheshimika ni lazima ufanye kazi kwa bidii.

4. Kutambulika

Ikiwa unafanya kazi kwa bidii huna haja ya kujikombakomba kwa wakubwa au mbele za watu ili utambulike; bidii yako ya kazi itakutambulisha.

Naamini umewahi kusikia watu wakipewa tuzo kwenye sherehe za kitaifa kutokana na kufanya kazi kwa bidii; hili linatupa picha ya kipekee ya faida ya kufanya kazi kwabidii.

Usijali hata kama wanakudharau au wanakuona duni, wewe fanya kazi kwa bidii watakutambua ukiwepo au hata wakati utakapoondoka wataona pengo lako.

5. Kuondoa lawama na manung’uniko

Mara nyingi idara au ofisi zenye malalamiko mengi ni zile zenye wafanyakazi wavivu. Pia wafanyakazi wengi wanaolaumiwa na kunyoshewa vidole na waajiri wao, wengi ni wale wavivu.

Ili kuepuka lawama au manung’uniko, ni vyema ukafanya kile unachokifanya kwa bidii kwani kwa njia hii utaongeza ufanisi wako.

6. Kupata matokeo makubwa

“Kazi kubwa = Matokeo makubwa.”

Hakuna matokeo makubwa bila kazi kubwa, yaani kazi iliyofanywa kwa bidii. Kwa mtu yeyote anayetaka kuona matokeo makubwa katika kile anachokifanya ni lazima kwanza afanye bidii.

Kumbuka hata mkulima anayefanya bidii katika kilimo ndiye huvuna zaidi ya wakulima wengine. Hivyo kufanya kazi kwa bidii hakuepukiki kwenye maisha.

7. Huleta fursa mpya

Mtu mwenye bidii kila mara hufungua milango ya kupata fursa mpya, kazi zake na bidii yake humtangaza na kumfungulia fursa zaidi. Hakuna mtu atakayempa mtu mvivu kazi au fursa zenye manufaa.

Hapa nakumbuka mfano wangu binafsi kwenye kazi ya mwezi mzima niliyoifanya usiku na mchana bila kuchoka kwa wiki mbili pekee. Kazii hii ilinipa sifa njema na kuniwezesha kupata kazi nyingine lukuki.

uprev
Mrejesho niliopata kutoka kwa mwajiri kwenye kazi husika.

8. Kuboresha afya

Kukaa bila kufanya kazi ni kujiletea matatizo ya kiafya; kazi ni sehemu ya mazoezi. Hivyo kufanya kazi kwa bidii kutakufanya uwe mwenye afya njema kila wakati.

Unalotakiwa kukumbuka hapa ni kuwa na kiasi, fanya kazi kwa bidii lakini usipitilize hadi uathiri afya yako.

Soma pia: Faida 10 za Kupumzika

Neno la mwisho

Kwa hakika mkono wa mtu mwenye bidii hauwi mtupu. Mtu mwenye bidii hujitesa kwa muda mfupi lakini matokeo yake huwa ni mazuri na ya muda mrefu.

Haipingiki kuwa bidii ndiyo kanuni mojawapo ya mafanikio.

Kumbuka hakuna mkato kwenye mafanikio; mtangulize Mungu, weka malengo, fanya bidii na matokeo ni hakika.

Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali andika maoni na maswali yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

4.3 13 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
guest

6 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mohammed
Mohammed
3 years ago

Wafanya kazi kwa bidii lakin pesa unayolipwa ni kidogo

Wilondja shindano Willys.
Wilondja shindano Willys.
3 years ago

Tunakushukuru sana kwa maelezo yenye elimu nzuri. Tuandalie jinsi ya kuwasaidia vijana wenye kuathirika dhidi ya madawa ya kulevya.

Bkk
Bkk
2 years ago

Poa poa sana

6
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x