Fahamu Njia 8 Unazoweza Kuzitumia ili Kupata Mtaji - Fahamu Hili
Tuesday, March 19Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Fahamu Njia 8 Unazoweza Kuzitumia ili Kupata Mtaji

Washirikishe Wengine Makala Hii:
Mtaji

Nifanyeje nipate mtaji? Nina wazo zuri lakini sina mtaji? Haya ni maswali ambayo nimekuwa nikiulizwa sana na wasomaji wa Fahamuhili.com, pamoja na watu wengi ninaokutana nao kwenye maisha ya kila siku.

Kutokana na sababu hii, nimeona ni vyema niandae makala ambayo itajibu maswali ya wasomaji wangu pamoja na wale wote wenye maswali kama haya.

Ingawa mtaji siyo kigezo pekee cha kufanikiwa kwenye biashara au mradi unaoufanya, mtaji unabaki kuwa kiungo muhimu sana katika kutekeleza wazo fulani au mradi kwa ufanisi. Kwa kuwa watu wengi huanzisha miradi au biashara kwa lengo la kupata pesa, huwa vigumu sana kuwa na pesa za kutosha kuanza utekelezaji wa wazo hilo.

Karibu ufuatilie makala hii kwa karibu nikushirikishe njia 8 unazoweza kuzitumia ili kupata mtaji wa kutekeleza wazo lako.

1. Akiba binafsi

“Mtu anayeweka akiba, ni mtu anayewaza kuhusu kesho.”

Mara kadhaa nimekuwa nikieleza kuwa kuweka akiba kuna manufaa kemkem, ikiwemo kupata uwezo wa kuwahi fursa mbalimbali na kuzifanyia kazi kwa wakati.

Hivyo basi, unaweza kutunza kiasi fulani cha pesa katika kipato chako hatakama ni kidogo, ili uweze kupata mtaji wa kuanzisha biashara au mradi wako.

Kumbuka! Usitake kuanza biashara na mtaji mkubwa sana kwani kuna hatari ya kuupoteza, jega mtaji wako kidogokidogo; unaweza kuanza na mtaji wa shilingi 10,000 lakini baadaye ukakua na kuwa mamilioni ya pesa. 

Soma pia: Faida 8 za Kuweka Akiba Unazopaswa Kuzifahamu

2. Kubadilisha mali na vitu binafsi

Nimewahi kukutana na watu kadhaa wakilalamika kuwa hawana mtaji, lakini ukiwachunguza sana utagundua kuwa wamezungukwa na mitaji mikubwa wasiyoitambua.

Hakuna haja yoyote ya kuwa na simu, televisheni, Kompyuta, na nguo za thamani kubwa wakati hauna mtaji wa kutekeleza mradi wako.

Unaweza kuuza vitu vyote ambavyo ukivikosa hutokufa ili uweze kupata mtaji; kumbuka uwekezaji ni muhimu kuliko maisha ya kifahari na anasa.

Ikumbukwe kuwa ukiwekeza utaweza kutengeneza pesa nyingi zaidi na kumudu kununua vitu vingine bora zaidi huko mbeleni.

3. Ndugu na marafiki

Ikiwa una mahusiano mazuri na ndugu zako, wanafamilia au marafiki, kwanini unaona shida kuwaomba wakuwezeshe kupata mtaji?

Andaa wazo vizuri, tafuta watu au marafiki wakaribu watakaokuamini, waombe wakuwezeshe kupata mtaji na uwaahidi utaurejesha mapema kadri uwezavyo ili wakuamini.

Faida za mtaji au mkopo kutoka kwa marafiki na ndugu:

  • Mara nyingi hakuna riba.
  • Hakuna masharti na vigezo vigumu.
  • Upatapo shida katika biashara au mradi wako ni rahisi ndugu kukuelewa.

Kumbuka! Usicheze na mtaji wa biashara au mradi kwa kuwa umeupata kutoka kwa ndugu au marafiki; pia kumbuka kuwa mwaminifu kutimiza mapatano ili wakati mwingine usaidike.

4. Taasisi za kuwezesha wajasiriamali

Hivi leo kuna taasisi na mashirika mbalimbali yanayotoa mitaji ya fedha na vifaa kwa wajasiriamali mbalimbali ili waweze kutekeleza mawazo yao. 

Baadhi ya taasisi hizo ni:

Hivi leo kuna taasisi na mashirika mbalimbali yanayotoa mitaji ya fedha na vifaa kwa wajasiriamali mbalimbali ili waweze kutekeleza mawazo yao. 

Fuatilia vyombo mbalimbali vya habari pia jiunge na vikundi vya wajasiriamali wengine ili zitokeapo fursa za mitaji uweze kuzifahamu na kuzitumia.

5. Mikopo ya taasisi za kifedha

Hivi leo ziko taasisi kedekede zinazotoa mikopo kwa ajili ya watu mbalibali; hivyo, mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha inaweza kutumiwa kama mtaji mzuri sana wa biashara. 

Hata hivyo nimekuwa nikiwashauri wajasiriamali wengi hasa wachanga kutokupendelea njia hii, ikiwa hawajaweka mikakati sahihi ya kutumia na kurejesha mkopo husika.

Hakikisha kama unataka kutumia njia hii kupata mtaji wa biashara au mradi wako, umejipanga vyema na unafahamu wazi njia na mbinu utakazozitumia kurejesha mkopo wa taasisi husika hata kama mambo yatakwenda mrama.

Soma pia: Mambo Matano Muhimu ya Kuzingatia Kabla ya Kuomba Mkopo

6. Ubia au uwanahisa

Katika dunia yetu ya leo, wapo watu wengi wenye fedha lakini hawajapata mahali pa kuwekeza fedha zao; wengi huwa na pesa nyingi lakini hawana muda wa kuanzisha na kusimamia biashara au mradi.

Unaweza kutumia mbinu hii kupata mtaji, kwa njia ya kuingia ubia au uanahisa na mtu au watu wengine wenye mitaji wanaotafuta mahali pakuiwekeza.

Kwa mfano unaweza kumfuata mtu mwenye pesa na ukamwomba akufungulie biashara au mradi; kisha utampa asilimia fulani ya faida ya biashara au mradi huo kwa kipindi fulani hadi utakapokuwa umereejesha mtaji wake na kiasi fulani cha asante au riba.

7. Mali kauli

Najua umeshajiuliza ‘mali kauli’? Ndiyo, mali kauli ni njia nyingine bora kabisa unayoweza kuitumia kupata mtaji wa biashara kwa kutegemea uaminifu wako.

Zipo biashara kubwa zenye mali nyingi lakini zina mzunguko mdogo katika eneo husika; lakini inawezekana wewe unafahamu mahali ambapo mali hizo zikiuzwa zitauzika vizuri. Unachopaswa kufanya ni kuchukua mali kwenye biashara husika na kwenda kuziuza kisha unarejesha fedha ya mauzo ya bidhaa husika na yule mwenye biashara atakupa gawio fulani kwa kazi hiyo.

Ikiwa utakuwa mwaminifu na kufanya kazi hii kwa bidii, ndani ya muda mfupi utapata mtaji wa kuanzisha biashara yako mwenyewe ambayo imetokana na kuuza mali za biashara nyingine kubwa kwa kuaminika tu (mali kauli).

8. Mashindano

Je, unajua kuna watu wametoka kimaisha kutokana na mitaji waliyoipata kutokana na mashindano mbalimbali? 

Hivi leo, yanaendeshwa mashindano mbalimbali hasa yale yenye lengo la kuibua wajasiriamali wenye mawazo mazuri lakini hawana mtaji. Mfano Mzuri ni Shindano la 3N lililokuwa likiendeshwa na hayati Regnald Mengi lenye lengo la kuwaibua vijana wajasiriamali.

Soma pia: Mambo 5 ya Kujifunza Kutoka kwa Reginald Mengi

Hivyo basi, unaweza kushiriki mashindano haya, na ukaibuka mshindi na ukajipatia mtaji wa kutosha kutekeleza wazo lako. Kumbuka kuweka nidhamu kwenye pesa unayoipata kwenye mashindano; kwani kutokana na kupatikana kwake bila kutarajia; inaweza kutumiwa vibaya na ikapotea.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema

Hitimisho

Naamini hadi kufikia hapa umepata mwanga wa ni njia gani unaweza kuitumia ili kupata mtaji kwa ajili ya kutekeleza wazo au mradi wako.

Napenda kukukumbusha kuwa mtaji siyo kila kitu na wala siyo kiasi cha pesa; bali usimamizi na mikakati sahihi kwenye kile unachaokifanya vitakuwezesha kukuza mtaji wako na kufikia malengo yako.

Je wewe unafahamu njia nyingine ya kupata mtaji? Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali andika maoni yako hapo chini, kisha washirikishe wengine makala hii.

3.4 10 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Richard
Richard
2 years ago

nimependa Sana makala yenu na Kuna kitu najifunza, pia nawafuatilia Sana
Swali: je nikihitaji kuwa napata makala zenu au taarifa ya makala mpya kwa njia ya email nifanyaje

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x