Kuanza biashara kutoka kiwango cha sifuri siyo kazi rahisi. Kama mjasiriamali utakutana na changamoto nyingi. Hili haliwezi kuwa tatizo ikiwa uko tayari kujifunza kutokana na makosa na kufahamu njia za kuyaepuka huko mbeleni. Hivi ndivyo wajasiriamali wengi wanavyojifunza na kukua. Unapokuwa kwenye biashara ni lazima ufahamu makosa ambayo yanaweza kuathiri biashara au uwekezaji wako; ili ujitahidi kuyaepuka ama kuyapunguza kadri iwezekanavyo. Ni dhahiri kuwa wajasiriamali wengi wamekwama kutokana na kupuuzia au kutofahamu makosa haya 15 ambayo hata wewe unatakiwa kuyafahamu na kuyaepuka.
1.Kujifanya unafahamu kila kitu
Usijifanye unajua kila kitu, hasa kama ndiyo umeingia kwenye ulimwengu wa kibiashara. Kwanini? Kwa sababu kuendesha biashara ni kujifunza na kupata uzoefu. Jitahidi kujifunza na kujijengea uzoefu kupitia maarifa mbalimbali ili uweze kuendesha biashara yako vyema kama mjasiriamali.
2. Kuanza biashara bila miundombinu
Ni dhahiri kuwa wengi husema “mwanzo ni mgumu” lakini ni lazima utengeneze miundombinu kadhaa. Unapoanzisha biashara kama mjasiriamali jitahidi kuweka miundombinu kadhaa ya muhimu kwanza kabla hujaanza kufanya biashara. Kuendesha biashara kunahitaji vifaa na rasilimali kadha wa kadha ambazo ni muhimu ziandaliwe kabla. Miundombinu hii inaweza kuhusisha mtaji, vifaa muhimu, ofisi ndogo ya kuanzia, n.k Kumbuka hivi ni vile vitu vya msingi tu na siyo mbwembwe zisizokuwa na msingi.
Soma pia: Jinsi ya kuanza biashara na mtaji mdogo.
3. Kuchagua mshirika asiyefaa
Awali ya yote, siyo lazima kuanza biashara kwa ushirika wa mtu mwingine. Kama umejiandaa vyema unaweza kumudu kusimamia na kuendesha biashara yako vyema bila tatizo. Lakini kama unahisi ni muhimu kuwa na mshirika basi chagua mshirika ambaye mnaendana kifikra. Huyu atakuwezesha na kukuunga mkono na kukusaidia kutimiza malengo na maono yako. Lakini ukichagua mshirika siyefaa ni dhahiri atakuzamisha.
4. Kutazama mafanikio pekee
Biashara yako au mradi hauwezi kukua ikiwa mipango yako haibadiliki. Wewe kama mjasiriamali unatakiwa ufikiri kwa upana unapokuwa unafanya maamuzi. Kutazama tu mafanikio bila kuzingatia ubora wa huduma ni kujizamisha majini wewe mwenyewe. Ni dhahiri kuwa kuzingatia kumudu kuwa na ubora wa huduma pamoja na ukuaji wa biashara ni jambo zuri zaidi.
5. Kutaka wateja wakutafute
Je ni kweli kuwa unataka wateja wakutafute na wakati soko limejaa wajasiriamali wengine na huduma? Hapana! Kama unataka kukuza msingi wako wa wateja ni lazima uwe pale ambapo wateja wapo. Kwa kufanya hivi watakutambua na kununua huduma au bidhaa yako.
6. Kupuuza nafasi ya teknolojia
Wajasiriamali wengi wa Kiafrika wanadhani kuwa teknolojia ni kwa ajili ya wazungu au kampuni kubwa. Haijalishi ni biashara au mradi gani unaoufanya ni lazima uzingatie nafasi ya teknolojia. Teknolojia iko kila mahali; hivyo ni vyema ukatumia teknolojia kama vile intaneti kutangaza, kuuza, na hata kuwasiliana na wateja wako.
7. Matumizi mabaya ya fedha
Watu wengi hawana matumizi mazuri ya fedha hasa wao binafsi. Tatizo hili limekuwa pia likijitokeza pale mtu anapotakiwa kusimamia na kutunza pesa za mradi au biashara. Wengi huishia kuzitumia kwenye mambo yao binafsi au kwa mambo ambayo hayana tija kwa kampuni au mradi. Ni lazima uwe na nidhamu ya pesa kama mjasiriamali ili uweze kuiwezesha biashara yako kukua; tambua hii ni pesa ya mradi au biashara na si ya matumizi yangu binafsi.
Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema.
8. Kujipanua bila mipango
Wajasiriamali wengi huwa wana mawazo makubwa na mazuri lakini wanakosa mikakati na mipango mizuri ya kuitekeleza. Unafungua mradi fulani leo na unafanikiwa ndani ya muda mfupi, nawe bila hata kujenga msingi imara wa kiuchumi na rasilimali nyingine unakimbilia kufungua mwingine au tawi. Hili ni kosa ambalo limeua maduka mengi yanayoanzishwa na wajasiriamali. Jifunze kujiandaa na kuweka misingi imara pale unapotaka kupanua au kuongeza mradi wako ili ule wa awali usife.
9. Kutokuajiri wafanyakazi wenye uwezo
Kama ni lazima kuajiri watu basi epuka kosa hili ambalo mara nyingi wajasiriamali hulifanya kwa huogopa garama za kuajiri watu wenye uwezo kwa ajili ya kufanya nao kazi. Ni dhahiri kuwa “rahisi inaumiza”; hivyo ni vyema ukaajiri hata mtu mmoja bora kuliko kuajiri watano wenye uwezo duni. Ukizingatia hili utajikuta unapata matokeo stahiki kutoka na kile ulichowekeza.
10. Kupuuza maoni ya wateja
“Mteja ni mfalme”; je unalifahamu hili? Wajasiriamali wengi hupuuzia maoni ya wateja bila kujua kuwa maoni ya wateja ndiyo huwawezesha kujirekebisha na kuweza kuwapa wateja wao kile wanachokihitaji. Kosa hili lisiposhughulikiwa litakupotezea kiasi kikubwa cha wateja na kuleta matokeo mabaya kwenye biashara au mradi wako.
11. Kuacha fursa zipite
Wajasiriamali wengi hupenda kungojea mazingira yawe mazuri bila hata kujali fursa zinazopotea. Ni dhahiri kuwa hakuna mtu atakaye kutengenezea mazingira unayotaka; ukiona fursa itumie na mambo yatakaa vyema mbele ya safari. Inawezekana fursa unayoiona leo kesho isiwepo tena.
12. Kukataa ushauri wa kitaalamu
Kila kitu kizuri kinahitaji maarifa stahiki ili kiweze kutokea. Ni dhahiri kuwa wajasiriamali wengi wanafanya kosa la kupuuza ushauri wa kitaalamu katika kazi zao kwa kuona kuwa hauna nafasi. Kwa mfano kama unafuga kuku au unalima mazao fulani kwanini usimwite mtaalamu wa kilimo au mifugo ili akushauri? Ni dhahiri kuwa ukipata ushauri wa kitaalamu utakuwa mwenye tija zaidi.
13. Kutokwenda na soko
Mjasiriamali mzuri ni yule anayefahamu kuwa kwa sasa soko linataka nini. Ni lazima uweze kuepuka kosa la kutokutazama mahitaji ya soko, ili uhakikishe mauzo ya bidhaa au huduma yako hayaathiriki. Kwa mfano zamani watu walinunua zaidi kuku walio hai, lakini leo soko la kuku waliochinjwa ni kubwa pia; kwanini wewe bado unauza tu kuku walio hai? Ni dhahiri ukitazama mfano huu utaona jinsi kosa hili linavyowaathiri wajasiriamali wengi katika maeneo mbalimbali.
14. Kushindwa kubaini wateja lengwa
Ni lazima wewe kama mjasiriamali uwabaini wateja wako ili huduma au bidhaa yako iuzike. Kwa mfano umetengeneza dawa ya kuua mbu, kisha unaiuza mikoa ya baridi badala ya mikoa yenye joto (kwenye mbu wengi); ni dhahiri kuwa hutoweza kupata wateja wa bidhaa yako sawa sawa. Chukua hatua leo watafute na uwafuate wateja sahihi wa huduma au mradi unaoufanya.
15. Mbinu duni za masoko
Maswala ya masoko ni taaluma kamili ambayo watu hujifunza katika shule na vyuo mbalimbali. Hivyo ni muhimu wewe kama mjasiriamali kutokupuuzia taaluma hii kwani ndiyo itakayokuwezesha kubaini njia bora na sahihi za kuuza huduma au bidhaa yako. Hakikisha mbinu za masoko unazifahamu vyema tena zinaendana na soko husika la bidhaa yako. Hakikisha pia mbinu zako zinabadilika kulingana na mazingira na hali ya soko.
Neno la Mwisho: Maarifa sahihi ni msingi wa kufanya vitu kwa ubora. Ni dhahiri kuwa makosa mengi yaliyoelezwa hapa yanatokana na ukosefu wa maarifa stahiki ya ujasiriamali. Nakushauri ujifunze kila siku ili kupanua uwezo na uzoefu wako wa kiujasiriamali. Pia usisahau kuweka kwenye matendo yale yote unayojifunza.
Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuadhikie hapo chini kisha washirikishe wengine elimu hii. Pia usisahau kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.
Eston ni mtafiti na mwandishi wa makala mbalimbali zinazohusu tija, maendeleo binafsi pamoja na afya bora. Analenga kuwahamasisha wengine pamoja na kuubadili ulimwengu kwa kupitia maarifa stahiki.
Nashukuru sana kwa haya machache nlio yapitia na mungu waongoze katika uelimishaji wenu. Maana mkiulizwa na mungu juu ya Elimu zunu mlizitumiaje. Kupitia elimu hii. Nikifanikisha malengo nitakuwa shuhuda wa Elimu hii.
Nashkruu sanae kwa ushairu ,nimejifuza vyema ubarikiwe sana
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; na kwa kuwa msomaji wetu. Karibu sana Fahamuhili.com
Asante Sana mkuu kwà madini haya nazidi kupanuka kifikra.
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; na kwa kuwa msomaji wetu. Karibu sana Fahamuhili.com