Njia 8 za Kuokoa Mafuta Unapoendesha Gari - Fahamu Hili
Friday, April 19Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Njia 8 za Kuokoa Mafuta Unapoendesha Gari

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kujaza Mafuta ya gari

Ni wazi kuwa gari linahitaji mafuta ili kusafiri toka sehemu moja hadi nyingine. Lakini swali ni je, unaweza kutawala kiwango cha mafuta kinachotumika? Ndiyo, unawea kutawana kiwango cha mafuta na kupunguza garama za matumizi ya mafuta zisizokuwa na ulazima.

Kama unapenda kuokoa kiasi cha mafuta yanayopotea bila sababu ya msingi katika gari lako, basi tumia njia hizi 8 zifuatazo.

1. Kabili upepo

Unapoendesha gari upepo hukinzana na gari; hivyo kadri gari linavyokinzana zaidi na upepo ndiyo pia unavyotumia mafuta mengi zaidi. Hivyo basi, usipende kuweka mizigo juu ya gari kwa nje (carrier) au kufungua vioo kwani kutasabisha ukinzani zaidi kati ya gari na upepo.

Kwa kukabili upepo vyema utapunguza ukinzani na kuokoa mafuta ambayo yangetumika kukabili ukinzani huo wa upepo.

2. Punguza mwendo

Hakuna haja ya kukimbia wakati huna jambo la haraka unaloliwahi; pia hakuna haja ya kukimbia ili uwe mbele ya gari linalofuata.

Kufanya hivi kutakupotezea kiasi kikubwa cha mafuta bila sababu yoyote ya msingi. Endesha mwendo wa wastani kama hakuna ulazima wa kuchochea mwendo na kupoteza mafuta mengi bila sababu.

3. Zingatia Matengenezo

Gari linahitaji matengenezo ya mara kwa mara. Kutofanyia mifumo kama vile injini na magurudumu matengenezo kwa wakati kutakufanya kupoteza kiasi kikubwa cha mafuta.

Unahitajika kuhakikisha mafuta lainishi (oil) yapo katika hali nzuri na katika kiwango cha kutosha katika injini yako. Pia unatakiwa kukagua ujazo wa magurudumu ya gari lako; kwani kadri gurudumu linavyokuwa na ujazo mdogo, ndivo linavyohitaji mafuta mengi zaidi kulizungusha.

4. Punguza uzito

Kadri gari linavyokuwa na uzito mwingi ndivyo linavyohitaji mafuta zaidi kuliendesha. Ikiwa hakuna haja ya kuongeza uzito usio na sababu kwenye gari basi upunguze.

Hakuna haja ya kubeba mizigo na vifaa usivyovitumia mara kwa mara kila ufanyapo safari. Jitahidi kupunguza mizigo isiyo ya lazima katika gari lako ili kuokoa matumizi yasiyo ya lazima ya mafuta.

5. Zingatia matuta

Matuta huwekwa katika barabara ili kutawala mwendo. Hivyo kufunga breki ghafla mara ukutapo tuta na kuchochea mwendo ghafla baada ya tuta kutakufanya utumie kiasi kikubwa zaidi cha mafuta.

Unaweza kupunguza mwendo taratibu na kuuongeza taratibu mara ufikapo kwenye matuta ili kuokoa kiasi cha mafuta kinachopotea.

6. Zima kiyoyozi

Ufanyaji kazi wa kiyoyozi (AC) katika magari mengi hutegemea nishati inayozalishwa na kifaa kiitwacho Alternator ambacho huzalisha umeme kwa msaada wa injini ya gari.

Hivyo basi, kuwasha kiyoyozi kutahitaji mafuta zaidi ili kuendesha kifaa hiki kiitwacho Alternator. Inashauriwa kuwasha kwa muda au kuzima kiyoyozi pale ambapo hakina ulazima ili kuokoa matumizi ya mafuta yasiyo ya lazima.

7. Tumia kiongeza mwendo vyema

Matumizi mazuri ya kiongeza mwendo (Accelerator), kutakuokolea kiasi kikubwa cha mafuta mara uendeshapo gari. Mambo ya kuzingatia katika swala hili:

  • Ongeza mwendo (Accelerate) taratibu. Kuongeza mwendo au kukanyaga mafuta kwa kasi kutasabisha utumizi mkubwa zaidi wa mafuta.
  • Usikanyage kiongeza mwendo (Accelerator) hadi mwisho. Unapokanyaga kiongeza mwendo hadi mwisho unasababisha matumizi makubwa sana ya mafuta. Hivyo kupelekea upotevu wa mafuta usiokuwa na ulazima.

8. Punguza matumizi ya gari

Njia bora zaidi na yenye matokeo makubwa katika swala la kuokoa mafuta katika gari ni kupunguza matumizi ya gari. Kakuna haja ya kwenda kila mahali kwa kutumia gari.

Unaweza kutembea kama sehemu ya mazoezi au hata ukatumia usafiri mwingine kama baisiketi au hata daladala.

Hitimisho

Zilizojadiliwa hapa ni njia anuwai zitakazokuwezesha kuokoa mafuta unapoendesha gari. Ni dhahiri kuwa kupunguza matumizi ya mafuta ni jambo linalowezekana ikiwa utafanyia kazi hoja jadiliwa hapo juu, ikiwemo matengenezo ya gari kwa wakati pamoja na uendeshaji sahihi.

Je wewe hutumia njia gani kuokoa mafuta? Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Usisahau pia kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

4.5 4 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Sinde
Sinde
3 years ago

I like this way of deducting fuel in my car

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x