Mambo 17 ya Kuzingatia Kabla ya Kusafiri Kwenda Nchi Nyingine - Fahamu Hili
Friday, June 2Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 17 ya Kuzingatia Kabla ya Kusafiri Kwenda Nchi Nyingine

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Ndege

Safari ni jambo linalohitaji maandalizi, hasa safari ya kwenda nchi nyingine. Watu wengi hujikuta wakiingia kwenye matatizo mbalimbali kutokana na kutokufahamu mambo ya kuzingatia kabla ya safari.

Ikiwa umeshasafiri, au ni mara yako ya kwanza kusafiri kwenda nchi nyingine, basi karibu nikushirikishe mambo 17 ya kuzingatia kabla ya kusafiri kwenda nchi nyingine.

1. Hakiki muda wa mwisho wa pasi yako ya kusafiria

Kama una pasi ya kusafiria, hakikisha muda wake wa matumizi haujakaribia kwisha. Hakikisha pia kurasa zilizo wazi hazijakaribia kwisha.

Kumbuka kuwa baadhi ya nchi haziruhusu watu kuingia au kutoka kwa kutumia pasi za kusafiria zilizobakiza muda wa miezi 6 kuisha muda wake.

2. Fahamu nyaraka zinazohitajika

Kila nchi ina taratibu na sheria zake. Hivyo hakikisha nyaraka kama vile VISA unazifuatilia kabla ya kwenda kwenye nchi inayohitaji nyaraka hizo.

3. Fahamu hali ya kisiasa na kiafya ya nchi husika

Hali ya kisiasa na kiafya inatofautiana kati ya nchi moja hadi nyingine. Kusafiri kwenda kwenye nchi yenye machafuko ya kisiasa au magonjwa hatari kama vile Ebola, unatakiwa kuchukua tahadharikubwa zaidi.

Hakikisha unaweza kustahimili na umejiandaa vyema kukabiliana na hali ya kisiasa na kiafya ya nchi unayokwenda kabla ya kuanza safari.

4. Fanya uchunguzi wa kiafya

Ni muhimu kumwona daktari kabla ya kusafiri ili achunguze kama kuna tatizo linaloweza kukukabili utakapokuwa nchi ya kigeni.

Pia chunguza kama utaweza kupata huduma za kimatibabu pindi uwapo katika nchi husika unayokwenda.

5. Kuwa na nakala za nyaraka muhimu

Lolote linaweza kutokea pindi uwapo safarini, nyaraka zako muhimu zinaweza kuibiwa au kupotea; hivyo ni muhimu kuwa na nakala za nyaraka zako muhimu.

6. Kuwa na fedha za dharura mkononi

Usitegemee sana mifumo ya kielektroniki kupata pesa pindi uwapo nje ya nchi.

Hakikisha unabeba kiasi fulani cha pesa mkononi mwako ili uweze kukidhi mahitaji yako pale utakapokosa pesa kwa kupitia njia za kawaida.

Chunguza kama utaweza kubadilisha pesa zako katika nchi unayokwenda ili kupata pesa za nchi husika. Ikiwa haiwezekani kubadilisha pesa zako katika nchi husika, basi badili pesa zako kabla ya safari.

7. Chunguza mambo au vitu vinavyoruhusiwa katika nchi husika

Vitu, mambo au tabia fulani ambazo ni halali au za kawaida kwenye nchi yako zinaweza zikawa mbaya au zisizo halali kwenye nchi nyingine.

Kwa mfano kuna nchi ambazo ni marufuku kumkumbatia mwanamke au mwanamke kuendesha gari. Pia kuna nchi ambazo huwezi kubeba vitu kama mbegu fulani, mawe au hata dawa fulani. Hivyo chunguza hili kwanza.

8. Tafiti kuhusu hoteli na vyakula

Ikiwa umepanga kwenda kukaa hotelini, ni muhimu kuhakikisha unafahamu utakavyofika hotelini na gharama husika za kukaa hapo.

Ni muhimu pia kufahamu kuhusu vyakula, kwani baadhi ya vyakula vya kigeni vinaweza visikufae; hivyo chunguza utakachokula na utakavyokipata.

9. Fahamu kanuni za usafiri utakaoutumia

Kwa mfano kama utatumia usafiri wa ndege ni muhimu ukafahamu sheria za ndege husika. Mara nyingi ndege haziruhusu kubeba madawa, silaha, mizigo mikubwa au hata baadhi ya vifaa vya kielektroniki.

Ili kuepuka kukwama kwenye safari yako. Ni muhimu ukafahamu swala hili mapema.

10. Fahamu utakavyopata huduma zako za kifedha

Kama unatumia kadi za kibenki kupata pesa, ni muhimu ukahakikisha kama utaweza kuzitumia kwenye nchi unayokwenda. Kwa mfano nchini Iran hakuna huduma za fedha za kimataifa.

Hivyo ni muhimu kuchukua hatua mapema kuhakikisha huduma au njia unayoitumia kupata pesa inapatikana kwenye nchi husika.

11. Beba vifaa vya mbadala vya kielektroniki

Viwango vya umeme (voltage) pamoja na viunganishi vyake (plugs) hutofautiana baina ya nchi moja na nyingine. Kwa mfano nchini Marekani, viwango vya umeme pamoja na viunganishi vyake ni tofauti sana na vile vya nchi za Afrika Mashariki.

Hivyo ili kuhakikisha unaweza kutumia vifaa vyako vya kielektroniki, ni vyema ukabeba vifaa vitakavyokuwezesha kuendana na mazingira husika. Mf. World travel adapter au multipurpose adapter

12. Fahamu kuhusu huduma za mawasiliano

Ni wazi kuwa uwapo katika nchi nyingine utahitaji huduma za mawasiliano kama vile intaneti na simu. Ni muhimu ukafahamu njia utakazotumia kupata huduma hizi pamoja na gharama zake.

Hakikisha kama eneo utakalokuwa lina mawasiliano, na kama halina mawasiliano fahamu njia mbadala utakayoitumia kuwasiliana.

13. Tafuta washauri wa safari

Zipo kampuni kadha wa kadha kwenye kila nchi zinazojihusisha na utalii au kuongoza safari. Unaweza kutafuta kampuni moja ikakupa muongozo au taarifa za muhimu kuhusu safari pamoja na nchi unayokwenda.

Ikiwa pia una mtu unayemfahamu katika nchi unayokwenda, unaweza kumtumia kupata taarifa.

14. Tafiti kuhusu hali ya hewa

Hebu fikiri unaenda kwenye nchi ya baridi kali bila nguo za kujikinga na baridi; je huoni kuwa utapata shida?

Hakikisha unafahamu vyema hali ya hewa ya eneo unalokwenda kama ni ya joto, baridi, mvua, upepo, barafu  n.k. Kwa njia hii utaweza kujiandaa na kuchukua tahadhari stahiki mapema.

15. Jifunze misamiati michache ya kigeni

Inawezekana unakwenda kwenye nchi inayotumia lugha tofauti na ya kwako; hakikisha unajifunza misamiati michache ya lugha ya nchi hiyo hatakama utakuwa na mkalimani.

Kujifunza misamiati michache ya lugha ya nchi husika kutakusaidia kujiandaa kwa lolote litakalotokea, ukipata shida uweze kujieleza au hata kuoyesha ukaribu kwa wenyeji wako.

16. Beba dawa muhimu

Nibebe dawa tena? Ndiyo, kwani uzima uko mikononi mwako? Kumbuka ni muhimu kubeba dawa za muhimu kama vile dawa za kutuliza maumivu.

Unapokuwa katika nchi nyingine unaweza kupatwa na maumivu na ukakosa dawa kwa karibu; hivyo kubeba dawa kutakusaidia sana.

17. Tafuta vitabu vya miongozo ya safari

Vipo vitabu mbalimbali vinavyotoa miongozo ya safari katika nchi mbalimbali duniani. Vitabu hivi hupatikana pia kwenye mtandao au maghala ya programu za simu za kisasa (App Store na Play store).

Kwa kuwa na vitabu hivi, utaweza kupata taarifa na miongozo mbalimbali kabla na uwapo safarini.

Hitimisho

Naamini sasa umefahamu au kukumbushwa juu ya mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kusafiri kwenda nchi nyingine. Naamini ukizingatia mambo haya kwa makini, utaweza kuwa na safari njema yenye amani na furaha.

Ninajua unajiandaa na safari au utajiandaa hivi karibuni; hivyo ninakutakia safari njema yenye amani na furaha.

Ikiwa una swali au maoni tafadhali tuandikie hapo chini. Usisahau kuwashirikisha wengine makala hii pamoja na kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

 

3.5 2 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Musa Ramadhani
Musa Ramadhani
2 years ago

Je kusafili kwenda inch za inje kuna tegemeana na elimu mfano mtu ajasoma kiwango kikubwa kaishia form 4 au darasa la basa harusuwi kusafili

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x