Mambo 10 ya Kuzingatia Kabla na Wakati wa Kuendesha Gari Umbali Mrefu - Fahamu Hili
Friday, June 2Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 ya Kuzingatia Kabla na Wakati wa Kuendesha Gari Umbali Mrefu

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kuendesha Gari Umbali Mrefu

Kuendesha gari ni suala linalohitaji umakini na utulivu mkubwa, hasa pale unapoendesha gari umbali mrefu. Mara kwa mara kumeshuhudiwa ajali mbalimbali ambazo kimsingi zinatokana na madereva kutokuzingatia kanuni muhimu katika utumiaji wa vyombo vya usafiri.

Ili kuhakikisha usalama wako pamoja na watumiaji wengine wa barabara, yapo mambo kadhaa unayopaswa kuyazingatia kabla na wakati wa kuendesha gari umbali mrefu.

1. Kagua na andaa gari

Kabla ya safari yoyote gari linahitaji kukaguliwa na kuandaliwa, hasa kabla ya safari ndefu. Kuna mambo kadhaa unayohitaji kuyakagua kwenye gari lako:

  • Kagua hali na ubora wa magurudumu. Hakikisha magurudumu yamejaa vizuri na hayajazeeka.
  • Kagua mafuta lainishi (oil). Hakikisha gari yako ina mafuta lainishi ya kutosha tena ya ubora unaotakiwa.
  • Kagua kiasi cha maji. Maji? Ndiyo maji ni muhimu sana kwenye gari kwa ajili ya kupooza injini ya gari pamoja na kusafishia vioo.
  • Kagua utendajikazi wa injini. Hakikisha injini yako inafanya kazi vizuri.
  • Kagua sehemu nyingine za gari kama vile breki, kiongeza mwendo (accelerator), usukani, taa, honi, viashiria (indicators), n.k.
  • Usibebe mizigo isiyokuwa ya lazima kwenye gari. Hii itakupotezea mafuta na nafasi bila sababu.

Hakikisha unalikagua gari lako vyema na kuliandaa kwa ajili ya safari. Unaweza pia kumtumia mtaalamu wa magari ili akusaidie kulikagua na kuliandaa kwa safari yako.

2. Pumzika

Ili uweze kuendesha gari vyema wakati wa safari ndefu ni muhimu kupumzika kwa kiasi cha kutosha kabla na wakati wa safari.

Hakikisha kabla ya safari unapata muda wa kutosha wa kulala ili kuepusha kusinzia barabarani kunakoweza kusababisha ajali. Unapokuwa barabarani unaweza pia kupumzika baada ya umbali fulani ili usichoke sana.

Kumbuka! Kupumzika uwapo safarini kutakuwezesha kupata nguvu zaidi na kutoa nafasi ya gari lako kupoa ili kuepusha ajali ya gari kuwaka moto.

3. Fahamu sheria na kanuni

Kuna kanuni zinazotawala matumizi ya barabara pamoja na vyombo vya usafiri. Ili kuepuka kuingia kwenye matatizo, hakikisha unafahamu vyema sheria za barabarani za eneo unalokwenda. Unaweza kuzingatia haya:

  • Beba vibali na nyaraka muhimu za dereva na gari Mf. leseni, bima, n.k.
  • Kama utavuka mipaka ya nchi beba pasi ya kusafiria pamoja na Visa kama inahitajika.

Soma pia: Mambo 17 ya Kuzingatia Kabla ya Kusafiri Kwenda Nchi Nyingine

4. Beba vitu muhimu

Kama ilivyo ada, safari inahitaji maandalizi. Hakikisha unabeba vitu muhimu unavyoweza kuvitumia kwenye safari yako kama hivi vifuatavyo:

  • Chakula na vinywaji. Ikiwa hutonunua chakula au kupata mahali pa uhakika pa kununua chakula na vinywaji, basi beba chakula chako utakachokula mara uwapo safarini.
  • Beba kisanduku cha huduma ya kwanza. Ni muhimu kuwa na kisanduku cha huduma ya kwanza kwenye gari ili upatapo tatizo la kiafya kikusaidie.
  • Beba vifaa vya msingi vya matengenezo ya gari. Vifaa kama vile jeki, spana, tochi, n.k. ni muhimu sana.

5. Tumia mafuta vizuri

Hakikisha unatumia mafuta vizuri mara uendeshapo gari umbali mrefu ili kuhakikisha unapunguza gharama zisizokuwa za lazima.

Hakikisha pia huachi kiwango cha mafuta kipungue sana ili usije ukaishiwa mafuta kwenye eneo ambalo liko mbali na kituo cha mafuta.

Soma pia: Njia 8 za Kuokoa Mafuta Unapoendesha Gari

6. Usitumie kilevi

Chanzo kikubwa cha ajali ni ulevi au matumizi ya pombe kwa madereva. Pombe hukufanya ushindwe kumudu gari vyema, hivyo usitumie kilevi kabla na wakati wa safari.

Soma pia: Madhara 12 ya Pombe Kiafya

7. Fahamu kuhusu hali ya hewa

Safari yako inaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya hewa. Hivyo ni vyema ukahakikisha unafahamu hali ya hewa ya eneo unalokwenda ili ujiandae mapema.

Kwa mfano kama kunatarajiwa kunyesha mvua, ni vyema ukachunguza kama barabara utakayoitumia kama huwa inapitika wakati wa mvua ili usije ukakwama.

Unaweza kutumia vyombo vya habari au mtandao wa Google ili kufahamu hali ya hewa ya eneo unalokwenda.

Soma pia: Mambo 10 Usiyojua Kama Unaweza Kuyafanya kwa Kutumia Google

8. Endesha kwa mwendo wa wastani

Mwendokasi ni chanzo kikubwa cha ajali na matatizo mengi barabarani. Ni muhimu kuendesha gari kwa mwendo wa wastani ili kuepusha matatizo yasiyokuwa na ulazima.

Kumbuka! Unapoendesha gari kwa mwendo wa wastani ni rahisi kujihami mara kunapotokea tatizo barabarani.

9. Zingatia burudani

Burudani tena? Ndiyo, unaweza kubeba miziki ambayo itakuburudisha wewe pamoja na wale unaosafiri nao ili msichoke muwapo safarini. Kusikiliza mziki wakati wa kuendesha gari kutakuweka katika hali (mood) nzuri sana.

Soma pia: Faida 9 za Kusikiliza Mziki

10. Fahamu vyema eneo unalokwenda

Je unafahamu vyema barabara utakayoitumia kufika kwenye eneo unalokwenda? Ili kuepuka kupotea au kukwama kwenye safari yako, ni muhimu ukafahamu vyema eneo unalokwenda.

Unaweza kuwauliza watu wanaofahamu eneo hilo au kutumia ramani mbalimbali kama vile Ramani za Google.

Neno la Mwisho

Pasipo shaka naamini umeona jinsi ambavyo kuendesha gari umbali mrefu kunavyohitaji maandalizi na mikakati muhimu. Kwa hakika ukizingatia mambo haya yaliyoelezwa hapa utaweza kuwa na safari salama yenye amani na furaha.

Je una swali au maoni? Tafadhali tuandikie maoni na maswali yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza pia kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

4.8 6 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
guest

6 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Felix Nyella
Felix Nyella
5 years ago

Makala nzuri sana kwa kweli nime-fahamuhili. Hongera mwandishi Kornel M.

Thomas kawonga
Thomas kawonga
Reply to  Kornelio Maanga
3 years ago

Nimependa na nmejifunza coz mm Bado cjui kuendesha ndo nataka kwenda driving hiv soon kwa hiki nmeongeza kitu

Omary
Omary
11 months ago

Hii ni nzuri kujikumbusha

6
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x