Mambo 10 ya Kuepuka Unapokuwa Kwenye Nchi ya Kigeni - Fahamu Hili
Friday, May 24Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 ya Kuepuka Unapokuwa Kwenye Nchi ya Kigeni

Washirikishe Wengine Makala Hii:
Ufaransa
Mnara wa Eiffel nchini Ufaransa.

Kila mahali pana taratibu na mambo yake. Mtindo wa maisha ulioouzoea kwenye nchi yako ya nyumbani, unaweza usikubalike kwenye nchi ya kigeni.

Inawezekana umepanga kutembelea nchi ya kigeni hivi karibuni, au tayari uko kwenye nchi ya kigeni. Karibu nikufahamishe mambo 10 ambayo kama utayaepuka utaweza kukaa kwenye nchi ya kigeni bila tatizo.

1. Kukiuka utamaduni wa nchi husika

Kila nchi ina tamaduni na taratibu zake. Kuna nchi haziruhusu kuvaa mavazi fulani au kufanya matendo fulani. Ni vyema ukahakikisha mambo unayoyafanya hayakiuki tamaduni za nchi husika.

Kwa mfano nchi nyingi za Kiarabu haziruhusu kubusu au kukumbatiana hadharani baina ya mwanamke na mwanaume. Ukikamatwa ukifanya kosa hili, unaweza kuchukuliwa hatua kali.

Soma pia: Maeneo 10 Ambayo ni Marufuku Kubusu au Kukumbatiana Hadharani

2. Kukashifu siasa au viongozi

Kuna watu wanapenda kuzungumzia siasa hata wakiwa usingizini. Epuka kuzungumzia siasa hasa kwa kukashifu viongozi au siasa za nchi ya ugenini.

Kufanya hivi kunaweza kukusababishia matatizo kama vile kugombana na wananchi wa nchi husika au kuwekwa chini ya sheria.

3. Epuka michezo au burudani usizozijua

Ugenini kuna mengi mageni. Yawezekana huwa unasikia maswala kama vile kuogelea au kuteleza kwenye barafu lakini hujawahi kufanya mambo haya.

Unapokwenda katika nchi ya kigeni na kuanza kuyafanya bila uangalizi au kujifunza vyema, unaweza kupatwa  na ajali mbaya inayoweza kugharimu maisha yako. Hivyo kuwa makini na michezo au burudani usizozijua.

4. Kukashifu dini au imani za wengine

Mara nyingi watu huona kuwa imani zao ni bora kuliko za wengine kiasi cha kuthubutu hata kukashifu imani nyingine hadharani.

Kufanya kosa hili katika nchi za kigeni kunaweza kukuletea matatizo makubwa kama vile kupigwa hadi kufa au kufukuzwa kwenye nchi husika.

5. Kutembea au kukaa na vitu vya gharama kubwa

Wahalifu wapo kila mahali duniani. Kutembea na vitu vya gharama kama vile pesa nyingi, simu, au hata vito vya thamani, kunaweza kuvutia wahalifu.

Ikiwa hakuna umuhimu wa kubeba vitu hivi uwapo katika nchi ya kigeni, basi viache mahali salama.

6. Kutokutii sheria

Kila nchi ina sheria zake zinazotawala wananchi wake. Hakikisha mambo unayoyafanya kwenye nchi husika hayakiuki sheria.

Kwa mfano kuna nchi ambazo uvutaji bangi na ukahaba unaruhusiwa, lakini nchi nyingine matendo kama hayo ni kinyume cha sheria.

7. Kutembelea maeneo siku za sikukuu

Mara nyingi watu hupenda kutembelea maeneo mbalimbali siku za sikukuu. Kutembelea maeneo kama vile vivutio vya utalii kwako wewe mgeni kunaweza kuwa na matatizo.

Kumbuka maeneo haya huwa na msongamano na hduma duni kipindi cha sikukuu.

Msongamano
Ukuta Mkuu wa China Ukiwa Umejaa Watalii Siku ya Sikukuu
Chanzo cha picha: https://buzzfeed.com

8. Kununua vyakula karibu na vivutio vya kitalii

Mara nyingi vyakula na vinywaji vinavyouzwa karibu na vivutio vya kitalii huwa vya gharama kubwa. Hivyo kununua vyakula katika maeneo haya kutakugharimu pesa nyingi.

9. Ulaji na unywaji holela

Hakikisha kila unachokula au kunywa kwenye nchi ya kigeni unakifahamu na kukimudu vyema. Watu wengi wamekuwa wakinunua vyakula na kushindwa kula au vikawaletea matatizo makubwa ya kiafya.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha hata vinywaji unavyovinunua unavimudu na vinakufaa vyema.

10. Kutokufahamu vituo vya taarifa au misaada

Unapokuwa kwenye nchi ya kigeni, hasa unapokuwa huna mwenyeji, ni muhimu kufahamu vituo vya taarifa au msaada.

Vituo hivi vitakuwezesha kupata mwongozo na msaada pindi upatapo shida. Ikiwa kuna ofisi ya ubalozi wa nchi yako ya nyumbani, unaweza kuitumia pia kama kituo chako cha msaada.

Hitimisho

Naamini baada ya kusoma makala hii, maisha yako kwenye nchi ya kigeni yatakuwa murwa sana. Siku zote kumbuka kuwa maisha kwenye nchi ya kigeni ni tofauti na yale uliyoyazoea, hivyo usitafute sana kuishi kama ulivyokuwa unaishi kwenye nchi yako ya nyumbani, bali elewa mtindo wa maisha wa nchi husika na uufuate.

Je una maswali au maoni? Tafadhali tuandikie maoni na maswali yako hapo chini. Usisahau pia kuwashirikisha wengine makala hii pamoja na kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

0 0 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x