Madhara 8 ya Kunakili Machapisho kutoka Kwenye Blog au Tovuti Nyingine - Fahamu Hili
Friday, May 24Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Madhara 8 ya Kunakili Machapisho kutoka Kwenye Blog au Tovuti Nyingine

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kunakili

Uandishi ni kazi ngumu na inayochosha, uandishi unahitaji kutafiti, muda, maarifa sahihi na hata rasilimali fedha. Kutokana na sababu hizi wamiliki wengi wa blog au tovuti hujikuta wakinakili maudhui kutoka kwenye blog au tovuti nyingine.

Swala la kunakili maudhui kutoka kwenye blog au tovuti nyingine limekuwa likisababishwa pia na kukosa lengo, uvivu, kukosa ubunifu pamoja na kutokujua madhara ya kunakili.

Ikiwa wewe ni blogger au mmiliki wa tovuti, basi karibu nikushirikishe madhara 8 yatokanayo na kunakili machapisho (post) kutoka kwenye blog au tovuti nyingine.

“Ni bora kushindwa kwenye kitu halisi kuliko kufanikiwa kwenye kitu cha kuiga.”

Herman Melville

1. Hukufanya uonekane duni

Unaponakili machapisho kutoka kwenye tovuti au blog nyingine, moja kwa moja unawaambia wasomaji wako kuwa huna cha kuwaambia kama usipomnakili mtu mwingine.

Hivyo wasomaji wako watakuona uko duni na watataka kumfahamu unayemnakili ili wasome machapisho yake moja kwa moja badala ya kusubiri uwaletee wewe.

2. Utakosa nafasi kwenye injini pekuzi

Google inafahamu chapisho liliwekwa wapi kwanza. Kwa hiyo ukurasa uliokuwa wa kwanza kuchapisha chapisho hilo ndio utakaopata nafasi zaidi kwenye matokeo ya utafutaji ya Google.

Ikumbukwe kuwa kadri unavyokuwa wa kipekee, ndivyo Google inavyokupa nafasi zaiidi.

Google huzichukulia blog au tovuti zinazonakili machapisho kama blog zinazokusanya matakataka “blog scraping”, na kuzipa adhabu “Google penalt” au kuzipa nafasi (Google rank) ndogo.

3. Utakosa matangazo ya maana

Hakuna mtu anayetaka kupoteza pesa zake kujitangaza kwenye blog au tovuti isiyokuwa na wasomaji na maudhui ya maana. Kampuni nyingi huchunguza ubora na upekee wa tovuti kabla hawajakubali kuweka matangazo yao.

Ikumbukwe pia kampuni zinazolipa vizuri za matangazo kama vile Google Adsenes, Media net, Amazon, n.k. hawakubali kupokea blogs zinazonakili machapisho.

4. Tovuti yako kufungiwa

Dunia ya leo mambo yamebadilika, tovuti au blog iliyojisajili kwenye huduma za ulinzi wa maundui kama vile DMCA, wakitaka kumkabili mwizi wa maudhui yao wanaweza kufanya hivyo.

Mamlaka kama DMCA ina dhamana ya kuiagiza web host yoyote kuzima au kufungia tovuti au blog inayoshitakiwa kwa wizi wa maudhui.

Je huoni kuwa unaweza kufungiwa tovuti yako kutokana na uvivu na uzembe?

5. Kuingia kwenye matatizo ya kisheria

Hii ni kutokana na kuwa kuna baadi ya tovuti zinahati miliki ya maudhui yake, tena hatari inazidi pale ambapo tovuti au blog iko kwenye nchi inayolinda hatimiliki.

Kunakili maudhui kutoka kwenye tovuti au blog hizi kunaweza kukuingiza kwenye matatizo makubwa ya kisheria kama vile kifungo au kulipa faini.

6. Kuwa mwizi wa jasho la mtu

Kwangu mimi nafahamu kuwa uandishi wa kwenye blog au tovuti ni kazi kama kazi nyingine zinazogharimu na kutoa jasho.

Kunakili makala kutoka kwenye blog nyingine kunakufanya uwe mwizi na usiethamini kazi aliyoifanya mtu mwingine.

7. Kupoteza wasomaji

Nani atakayekuja kwenye tovuti yako kama anafahamu kuwa kazi yako ni kunakili tu? Ni wazi kuwa watu wakijua wewe unanakili na huna jipya unalowashirikisha, hawatakuja tena kusoma tovuti yako.

Ni vyema kujitahidi kuwa mbunifu ili uwe tofauti na wengine, ni lazima msomaji afahamu kuwa vitu vinavyopatikana kwenye blog au tovuti yako hawezi kuvipata sehemu nyingine.

8. Kutokuaminika

Unanakili kila kitu, hata vitu vya uwongo wewe unanakili tu alimradi ujaze blog au tovuti yako; je unafikiri kwa njia hii wasomaji au watembeleaji watakuamini?

Kumbuka! Ingekuwa kunakili machapisho hakuna madhara, wamiliki wa blog na tovuti wangengojea tovuti au blog moja iandike na wao wanakili. Hakuna mtu angetumia muda na gharama kuandika makala mpya.

Kwa kufahamu athari za kunakili zilivyo nyingi, ni muhimu kuandika hata makala moja tu nzuri kwa wiki au kwa mwezi kuliko 100 za hovyo.

Neno la Mwisho

Kuna wakati mwingine mtu  hutamani makala aliyoiona mahali fulani wasomaji wake waifahamu, lakini mara nyingi watu hukosea njia bora ya kutimiza lengo hili.

Badala ya kunakili kila kitu unaweza kuandika dondoo au ukaweka kiunganishi cha makala hiyo ili wasomaji wako wafikie chapisho halisi. Unaweza pia kuwasiliana na mmiliki ili kama inawezekana akupe ruhusa halali ya kuchapisha chapisho lake kwenye blog au tovuti yako.

Naamini sasa umefunguka macho na hutoweka tena makala za kunakili akilini mwako. Katika makala zijazo nitaeleza jinsi unavyoweza kuboresha tovuti au blog yako zaidi.

Je una swali au maoni? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha usisahau kuwashirikisha wengine makala hii. Unaweza kujiunga nasi kwa barua pepe au kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

5 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x