Faida 10 za Kusafiri Unazotakiwa Kuzifahamu - Fahamu Hili
Thursday, May 23Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Faida 10 za Kusafiri Unazotakiwa Kuzifahamu

Washirikishe Wengine Makala Hii:

tembo

Najua umeshajiuliza faida za kusafiri? Ndiyo, kusafiri kuna faida nyingi unazopaswa kuzifahamu. Swala la kusafiri au kutembelea maeneo mbalimbali halijazoeleka sana kwetu waafrika kama ilivyo kwa wenzetu wazungu.

Kusafiri siyo lazima kwenda nchi nyingine, bali hata safari za ndani ya nchi au za ndani ya eneo lako zina maana kubwa. Kwa hakika zipo sababu kuntu zinazowafanya wenzetu wa magharibi kusafiri kwenda sehemu mbalimbali duniani. Ikiwa basi unataka kufahamu faida za kusafiri ili uzifanyie kazi, basi karibu nikushirikishe faida 10 za kusafiri.

1. Kujifunza mambo mbalimbali

Unaposafiri unajifunza mambo mbalimbali ambayo isingekuwa rahisi kujifunza mambo hayo ukiwa nyumbani.

Unaposafiri utajifunza jografia, utamaduni au hata mtindo wa maisha wa watu wa eneo utakalotembelea. Hivyo basi, kusafiri ni shule nzuri ya kuongeza maarifa yako.

2. Kupata marafiki

Kwa njia ya kusafiri utapata marafiki mbalimbali ambao watatokana na watu uliokutana nao safarini. Zipo shuhuda kadhaa za watu waliopata marafiki kwenye safari zao waliowafaa katika maisha yao yote.

Pia wapo watu waliopata wenzi wa maisha kutokana na kusafiri; hivyo faida hii ya kusafiri haiwezi kuachwa nyuma.

3. Kufahamu fursa mpya

Huwezi kufahamu vyema fursa zilizoko kwenye eneo fulani kama hutokwenda kwenye eneo hilo. Kwa njia ya kusafiri utaweza kuona fursa mbalimbali ambazo unaweza kuzifanyia kazi na ukajipatia kipato au ukaongeza kipato chako.

Hapa naikumbuka kampuni ya kitalii ya Bob Africa ambayo ilianzishwa na wanandoa wawili waliokuja Afrika kama watalii na baadaye wakaona fursa ya kuwekeza kwenye utalii.

4. Kujifunza lugha mpya

Unaposafiri kwenda nchi nyingine inayozungumza lugha tofauti na ya kwako ni lazima ujifunze lugha ya nchi husika angalau kwa uchache.

Hivyo, kwa njia hii utaongeza idadi ya lugha unazozifahamu na kuwa mwenye tija zaidi.

Soma pia: Mambo 17 ya Kuzingatia Kabla ya Kusafiri Kwenda Nchi Nyingine

5. Hukupa mtazamo mpya

Faida nyingine ya kusafiri ni kupata mtazamo mpya tofauti na ule uliokuwa nao awali. Inawezekana kuna mambo ambayo huwa huyathamini uwapo nyumbani, lakini utayathamini uwapo safarini.

Inawezekana pia ulikuwa na mtazamo fulani kuhusu watu au eneo fulani, lakini utapata mtazamo mpya baada ya kusafiri kwenda eneo husika.

6. Hukuwezesha kutumia muda vyema

Inawezekana umepata likizo fupi au una muda fulani wa mapumziko kila baada ya kipindi fulani; badala ya kutumia muda wako kulala au kutazama televisheni siku nzima, unaweza kuutumia muda huo kwa kusafiri.

Hivyo, hutopoteza tena muda wako kwenye mambo yasiyo na tija, bali utautumia muda wako kwa mambo yenye manufaa kwako.

7. Huondoa msongo wa mawazo

Msongo wa mawazo ni tatizo kubwa linalowatesa watu wengi kwenye dunia hii ya leo. Kwa njia ya kusafiri utaweza kuondoka kwenye mazingira au katikati ya watu wanaokufanya upate msongo wa mawazo.

Hivyo, unaposafiri utaona mambo au mazingira tofauti ambayo yatabadili hali yako ya kisaikolojia na kukuepushia msongo wa mawazo.

8. Hukuwekea kumbukumbu ya kipekee

Hebu fikiri ukisafiri na kwenda kukwea mlima Kilimanjaro au Evarest, naamini hili litakutengenezea kumbukumbu ambayo siyo rahisi kusahaulika.

Mambo uliyoyafanya na kuyaona au hata jinsi ulivyokabiliana na changamoto mbalimbali kutakutengenezea kumbukumbu nzuri ya kipekee.

9. Hukuburudisha.

Kusafiri ni burudani ya aina yake hasa kama unasafiri kwenda kwenye eneo sahihi. Unaposafiri utapata faida ya kupata burudani bora na ya kipekee.

Uwapo safarini utaweza kuona vitu vya kuvutia kama vile mazingira ya asili (mito, milima, mabonde, n.k.), wanyama pamoja na sanaa za eneo husika kama vile ngoma, maigizo, mavazi ya kitamaduni, n.k.

10. Huboresha maisha ya wengine

Unaposafiri unaweza kuboresha maisha ya watu wengine kwa njia moja au nyingine.

Hebu fikiri juu ya vyombo vya usafiri unavyovitumia, hoteli, viingilio utakavyolipa, n.k. Hivi vyote vinawapa kipato watu wengine na kuboresha maisha yao.

Hivyo, kusafiri hakukunufaishi wewe peke yako bali hata na wengine wanaohusika kwenye safari yako.

Hitimisho

Kwa hakika unaweza kutazama swala la kusafiri kwa juu juu na kufikiri halina faida yoyote. Ni ukweli usiopingika kuwa wenzetu wazungu wanafahamu vyema umuhimu wa kusafiri ndiyo mana wako tayari kulipa gharama kubwa ili watimize lengo lao.

Je wewe huwa unasafiri? Je unanufaika vipi? Tafadhali andika maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

5 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x