Faida 5 za Kuvaa Kofia Ngumu (Helmet) - Fahamu Hili
Tuesday, October 3Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Faida 5 za Kuvaa Kofia Ngumu (Helmet)

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Kofia Ngumu

Usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda, umeenea sana hivi leo. Karibu kila mtu ameshatumia au anatumia usafiri huu. Hata hivyo kumekuwepo na changamoto kubwa ya ajali zitokanazo na pikipiki.

Kutokana na tatizo hili, mara nyingi tumekuwa tukisikia vyombo mbalimbali hasa vile vya usalama barabarani, vikisisitiza juu ya kuvaa kofia ngumu (helmet). Je kuna manufaa gani yaliyoko kwenye swala hili?

Ni ukweli usiopingika kuwa kuna manufaa makubwa sana kwenye swala la kuvaa kofia ngumu. Karibu nikushirikishe faida 5 za kuvaa kofia ngumu.

1. Unatii sheria

Kabla ya kuzungumzia faida binafsi anazozipata mtu anayevaa kofia ngumu; kwanza anapata faida ya kutii sheria. Hii ina maana kuwa ataepuka adhabu ya tozo au kifungo.

Sheria zimewekwa ili zifuatwe, hivyo kutokufuata au kutii sheria ni kujiweka kwenye matatizo. Kwa kuvaa kofia ngumu ni kuheshimu sheria za usalama barabarani zinazokutaka kufanya hivyo.

2. Unalinda kichwa chako wakati wa ajali

Sehemu hatari zaidi kupata majeraha wakati wa ajali ya pikipiki ni kichwa. Kofia ngumu imetengenezwa kwa mfumo ambao inalinda kichwa chako dhidi ya majeraha.

Hivyo kuvaa kofia ngumu kunakuepushia majeraha hatari au hata kifo wakati wa ajali.

Unaweza kulishuhudia hili kwa kutazama picha zilizowekwa hapo chini.

kofia
Kofia ngumu ya dereva aliyepata ajali.
Chanzo cha picha: https://www.boredpanda.com

 

kofia
Kofia ngumu ya dereva mwingine aliyepata ajali.
Chanzo cha picha: https://www.boredpanda.com

Hebu fikiri madereva hawa wasingekuwa wamevaa kofia ngumu, ni wazi wangepata athari kubwa sana.

3. Unajikinga na madhara ya kimazingira

Unapoendesha gari ni tofauti na unapoendesha pikipiki au baisikeli kwani umbo la gari hukukinga na madhara ya kimazingira.

Unapoendesha pikipiki, upepo, vumbi, jua au hata barafu hukupiga moja kwa moja. Kwa kuvaa kofia ngumu utajikinga na vumbi, upepo, jua na hata barafu.

4. Inakufanya uone vizuri

kofia ngumu
Kofia ngumu yenye kioo kizuri.
Chanzo cha picha: http://drivinglife.net

Kofia ngumu yenye ubora mzuri huwekwa kioo kinachomsaidia dereva kuona vizuri. Kioo hiki hukinga macho ya dereva dhidi ya vumbi na upepo, hivyo kumuwezesha kuona vyema kule anakoelekea.

Kumbuka kuona vyema barabarani ni jambo muhimu sana ambalo husaidia kuepusha ajali.

5. Inaboresha mwonekano wako

Dereva wa pikipiki aliyevalia vizuri kofia yake ngumu pamoja na mavazi yake huonekana nadhifu na mwenye kuvutia. Unaweza kutazama picha hapo chini ili kulidhibitisha hili.

mama na mtoto

Neno la Mwisho

Uwe ni abiria au dereva, ni muhimu ufahamu kuwa uhai na afya yako ni muhimu kuliko hata pesa. Madereva wengi wa pikipiki hawajali uhai wala afya zao, wao hulenga kupata pesa pekee.

Baadhi ya abiria hudai kuwa kofia ngumu hazifanyiwi usafi ndiyo maana hawapendi kuzivaa; ni muhimu madereva wa pikipiki kuhakikisha wanaweka kofia zao na za abiria katika hali ya usafi.

Kamwe usikubali kupanda pikipiki bila kofia ngumu; linda afya na uhai wako kwa kuvaa kofia ngumu leo.

Je wewe huwa unavaa kofia ngumu? Tafadhali tupe maoni yako kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza pia kujiunga nasi kwa barua pepe au kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

0 0 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x