Mambo 10 ya Kufanya Ili Kuepuka Ajali Unapoendesha Pikipiki - Fahamu Hili
Thursday, March 28Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 ya Kufanya Ili Kuepuka Ajali Unapoendesha Pikipiki

Washirikishe Wengine Makala Hii:
Pikipiki
Picha inamilikiwa na Simisa (talk · contribs)

Pikipiki au kwa jina maarufu bodaboda, zinatumiwa na watu wengi sana kwa usafiri. Licha ya pikipiki kutumiwa kama usafiri, wengine huzitumia kama chanzo cha kipato chao cha kila siku.

Hata hivyo kila mmoja amewahi kusikia au kushudia juu ya changamoto kubwa ya ajali inayokabili usafiri wa pikipiki au bodaboda. Wengine wamepata majeraha, kupoteza maisha, kupoteza mali au hata kupata ulemavu wa kudumu.

Pasipo shaka sasa ni wakati wa kutazama ni nini hasa chanzo cha ongezeko kubwa la ajali za pikipiki ili kikabiliwe.

Ikiwa unaendesha pikipiki au unataka kuongeza maarifa yako, basi fahamu mambo 10 ya kufanya ili kuepuka ajali unapoendesha pikipiki au bodaboda.

1. Pata elimu sahihi ya kuendesha pikipiki

Pikipiki ni chombo cha kitaalamu kinachohitaji maarifa sahihi ya kukitumia. Ajali nyingi zinatokana na watu kuendesha pikipiki bila maarifa sahihi ya kutumia chombo hicho pamoja na kanuni  muhimu za usalama barabarani.

Hivi leo kijana hujifunza pikipiki kichochoroni kwa siku mbili na kuingia kwenye barabara kuu za mji, hili limefanya wengi kugongwa au kugonga watumiaji wengine wa barabara.

Ni muhimu kuhudhuria mafunzo stahiki ya kuendesha chombo cha moto ili kuepuka ajali.

2. Tumia pikipiki bora na salama

Vifaa badia au feki vimetawala soko. Baadhi ya pikipiki zimetengenezwa kwa viwango duni, jambo ambalo linaweza kusababisha ajali.

Ni muhimu kuhakikisha unatumia pikipiki bora ambayo haitakuletea hatari kama vile kukatika breki au kupasuka gurudumu kirahisi. Unaweza kuzingatia haya yafuatayo:

  • Nunua pikipiki kutoka kwa watengenezaji wanaoaminika.
  • Fanyia matengenezo pikipiki yako kwa wakati.
  • Kagua pikipiki yako vyema kabla ya kuanza safari. Hakikisha kila kitu kinafanya kazi vyema.

Soma pia: Njia 8 za Kutambua Bidhaa Feki au Bandia

3. Usitumie kilevi

Kilevi au pombe ni chanzo kikubwa cha ajali. Ili kuepuka ajali unapoendesha pikipiki, ni muhimu kuepuka matumizi ya pombe kwani hukufanya ushindwe kumudu vyema pikipiki yako uwapo barabarani.

Soma pia: Madhara 12 ya Pombe Kiafya

4. Vaa kofia ngumu

Usalama wa mtumiaji wa usafiri wa pikipiki au bodaboda, unategemea kwa kiasi kikubwa uvaaji wa kofia ngumu. Kofia ngumu hukinga kichwa chako mara upatapo ajali, pia kofia ngumu hukulinda na athari za kimazingira kama vile upepo na vumbi.

Ili kuepuka kifo au majeraha makubwa wakati wa ajali, ni vyema kuhakikisha unatumia kofia ngumu.

Soma pia: Faida 5 za Kuvaa Kofia Ngumu (Helmet)

5. Tambua hali ya hewa

Usafiri wa pikipiki huathiriwa sana na hali ya hewa. Ni muhimu sana kuchunguza  hali ya hewa ya eneo unalotaka kwenda kabla ya kuanza safari.

Kumbuka unapokwenda eneo lenye mvua unaweza kukutana na changamoto ya utelezi ambayo inaweza kusababisha ajali.

6. Beba mzigo sahihi

Bodaboda au pikipiki siyo gari. Kuna tabia ya baadhi ya watu hupenda kubeba mizigo mingi au abiria kupita kiasi cha uwezo wa pikipiki zao.

Hili huwasababishia kupata ajali kwani hushindwa kumudu pikipiki zao wanapokutana na kitu cha ghafla barabarani. Hakikisha huzidishi mzigo kwenye pikipiki yako ili kuepuka ajali.

7. Epuka mwendo kasi

“Mwendo kasi unaua.”

Chanzo cha ajali nyingi za pikipiki ni madereva wa pikipiki kuendesha pikipiki zao kwa mwendo mkubwa. Hili huwafanya washindwe kuzimudu mara kunapotokea kitu cha ghafla barabarani. Ikiwa huna haraka sana, basi nenda kwa mwendo wa wastani ili ufike salama kule uendako

8. Endesha kwa kujihami

Unapoendesha pikipiki epuka mawazo kama vile “ananiona” au “ni haki yangu kupita”. Kumbuka pikipiki ni rahisi zaidi kugongwa na kupata madhara makubwa kuliko gari.

Hakikisha unajihami, akili yako yote inakuwa barabarani huku ukichukua tahadhari za kiusalama. Hakikisha maamuzi na matendo yote unayoyafanya ni salama.

9. Kuwa makini unapompita mwingine (overtake)

Chanzo kingine kikubwa cha ajali za barabarani kwa magari na pikipiki ni kupita (overtake) vyombo vingine. Kumbuka kuovertake ni jambo linalohitaji umakini mkubwa, la sivyo utagongana na gari au pikipiki nyingine. Unaweza kuzingatia haya yafuatayo:

  • Overtake mahali sahihi. Usiovertake kwenye kona, kwenye mteremko mkali au mlima, mahali usipoona vizuri au mahali ambapo haparuhusiwi.
  • Punguza mwendo wakati wa kuovertake.
  • Mjulishe dereva mwingine kuwa unataka kuovertake.
  • Usiovertake kwa kushtukiza.

10. Tabua hatari za barabarani

Kuna hatari mbalimbali zinazoweza kuwepo barabarani. Pikipiki huathiriwa zaidi na hatari za barabarani kuliko gari, hivyo ni vyema kuwa makini.

Kwa mfano kukanyaga jiwe au tunda lililooza barabarani kunaweza kukusababishia ajali mbaya. Hivyo ni vyema ukajihadhari na vitu kama vile mashimo, mawe, makopo, kamba au waya n.k.

Neno la mwisho

Pasipo shaka, ajali za pikipiki zinaweza kuepukika au kupunguzwa kwa kiasi kikuwa ikiwa madereva pamoja na watumiaji wa pikipiki watazingatia mambo yaliyoelezwa hapa.

Ni muhimu kujali uhai na afya yako kabla ya kitu kingine chochote. Hakikisha usalama kwanza uwapo barabarani ndipo vitu vingine vifuate.

Je wewe huwa unazingatia mambo haya?

Tafadhali washirikishe wengine makala hii pamoja na kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

0 0 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Patrick Alfred
Patrick Alfred
3 years ago

Elimu nzuri Sana 🙏

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x