Mambo 7 ya Kuzingatia Unapoendesha Gari Wakati wa Mvua au Ukungu - Fahamu Hili
Saturday, April 20Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 7 ya Kuzingatia Unapoendesha Gari Wakati wa Mvua au Ukungu

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Mvua na ukungu

Kama ambavyo nimekuwa nikieleza kwenye makala nyingine kuwa gari ni chombo kinachorahisisha usafiri lakini kinatakiwa kutumiwa kwa umakini na tahadhari kubwa.

Umakini na tahadhari zaidi vinahitajika ikiwa utaamua kuendesha gari wakati hali ya hewa ikiwa siyo nzuri, yaani kuna maswala kama vile mvua au ukungu.

Taarifa mbalimbali za usalama barabarani zinaeleza kuwa zipo ajali nyingi zinazogharimu maisha na mali za watu ambazo husababishwa na mvua au ukungu.

Hivyo ikiwa unataka kuongeza maarifa pamoja na kulinda usalama wako, basi fahamu mambo ya kuzingatia unapoendesha gari wakati wa mvua  au ukungu.

1. Punguza mwendo

Mwendokasi unaua!

Mwendo mkubwa ni hatari sana, lakini ni hatari zaidi mara hali ya hewa inapokuwa mbaya. Kumbuka kuwa wakati wa mvua au ukungu barabara huteleza na ni vigumu kuona njia vyema.

Hivyo inashauriwa kupunguza mwendo mara unapoendesha gari wakati wa mvua au ukungu ili uweze kulimudu gari vyema. Pia ukiendesha gari kwa mwendo mdogo utaweza kujihami mara kinapotokea kitu cha ghafla barabarani.

2. Washa taa pale mvua au ukungu unapozidi

Mara nyingi mvua pamoja na ukungu hukufanya ushindwe kuona barabara vyema. Hivyo ni muhimu kuwasha taa za ukungu (fog lights) mara zinapokuwa na umuhimu; inashauriwa kuwasha taa hizi ikiwa hauwezi kuona mita 100 mbele.

Taa hizi hazikusaidii tu wewe kuona mbele bali huwasaidia watumiaji wengine wa barabara kuona gari lako ili kuepusha kugongana na chombo kingine cha usafiri, kugogwa au hata kugonga mtembea kwa miguu.

3. Usikaribie gari jingine sana

Kwasababu ya kutokuona vyema pamoja na utelezi wakati wa mvua au ukungu, inashauriwa kutokulikaribia gari lingine sana.

Hili litakuepushia kugongana na gari lingine kunapotokea swala kama vile gari kuteleza au kurudi nyuma ghafla.

4. Usipite kwenye mafuriko

Maji yanayopita juu yabarabara, hasa juu ya daraja ni hatari sana. Kumekuwepo na matukio kadhaa ya magari kuzolewa na maji na kusababisha vifo pamoja na uharibifu wa mali.

Hii ni kutokana na sababu kuwa magurudumu ya gari huelea kwenye maji kutokana na kuwa na upepo ndani yake; hivyo hulifanya gari liwe rahisi kuzolewa na maji.

Pia ni vigumu kutambua kama mahali unapotaka kupita pana korongo au daraja limevunjika, kwani maji huwa yamefunika eneo husika.

Ni vyema kusubiri maji yapungue au yakauke kabisa ndipo upite kwenye eneo hili ili kuepuka ajali.

5. Kagua gari kabla ya safari

Kabla ya safari yoyote, gari kama chombo cha moto linahitaji kuandaliwa. Ni muhimu kuhakikisha taa, breki, injini, visafisha vioo (wiper blades), pamoja na sehemu nyingine za gari zinafanya kazi vyema kabla ya safari.

Kwa mfano utahitaji taa pamoja na visafisha vioo unapoendesha gari wakati wa mvua au ukungu ili uone mbele vyema. Hivyo swala la ukaguzi wa gari kabla ya safari haliepukiki.

Soma pia: Mambo 10 ya Kuzingatia Kabla na Wakati wa Kuendesha Gari Umbali Mrefu

6. Epuka kupita magari mengine

Moja kati ya chanzo kikubwa kinachosababisha ajali hivi leo ni kupita magari mengine (overtaking). Kutokana na kupungua kwa uwezekapo wa kuona pamoja na utelezi wakati wa mvua au ukungu, inashauriwa kutokupita magari mengine ikiwa hakuna ulazima.

Hili litaepusha ajali ambazo zingeweza kuepukwa; hata hivyo ikiwa ni lazima kupita magari mengine, basi ni vyema kuchukua tahadhari kubwa pamoja na kuzingatia kanuni za kupita magari mengine.

7. Zingatia kanuni nyingine za barabarani

Kuna kanuni lukuki zinazotawala matumizi ya barabara, kanuni hizi zinapaswa kuzingatiwa vyema hasa wakati wa mvua na ukungu.

Hakikisha unasoma maelekezo unayopewa kwenye alama za barabarani, kutoka kwa askari wa usalama barabarani pamoja na madereva wengine na kuyatekeleza vyema.

Panapotakiwa kupunguza mwendo punguza, panapotakiwa kusimama simama, panapotakiwa kupisha pisha ili usisababishe matatizo yasiyokuwa na ulazima.

Hitimisho

Naamini umeona jinsi ambavyo swala la kuendesha gari wakati wa mvua na ukungu linahitaji umakini na tahadhari kubwa. Inashauriwa kama hakuna ulazima wa kuendesha gari wakati wa mvua au ukungu, basi subiri hali ya hewa iwe nzuri ndipo ufanye safari yako.

Je wewe huwa unayazingatia haya? Je kuna mambo mengine unayoyazingatia wakati wa kuendesha gari wakati wa mvua au ukungu?

Tafadhali andika maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine.

5 1 vote
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x