Mark Zuckerberg akiwa chuoni Harvard
Ukimuuliza Mark Zuckerberg juu ya alichokikamilisha alipokuwa akisoma chuoni Harvard jibu lake linaweza kukushangaza. Unaweza kufikiri ni Facemash ambayo baadaye ilikuja kuwa Facebook lakini siyo.
“Priscilla ni mtu muhimu zaidi katika maisha yangu, na jambo muhimu zaidi nililojenga wakati wangu hapa.” Zuckerberg alisema hayo kuhusu mke wake wakati wa hotuba ya ufunguzi wa mahafali huko kwenye chuo cha Harvard mwaka huu.
Mkurugenzi huyu mkuu wa Facebook mwenye miaka 33 alitumia kiasi kikubwa cha muda wake wakati wa hotuba hiyo akionyesha jinsi alivyokutana na Priscilla Chan, daktari wa watoto ambaye hatimaye walifunga ndoa mwaka 2012.
Mark Zuckerberg na mke wake Priscilla Chan
Zuckerberg alikutana na Chan kwenye sherehe na akampenda. Chan ameonekana kuwa na sehemu kubwa kwenye maisha yake kwani yeye ndiye aliyemshauri afundishe wanafunzi wa shule ya kati masomo ya ujasiriamali jioni baada ya masomo.
Zuckerberg alieleza kuwa alijifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wanafunzi hao kuhusu maisha. Pia aliwashirikisha masimulizi yake, pia aliwatia moyo kuwa kuna siku pia nao watafika chuo kikuu.
Alieleza kuwa kwa mika mitano amekuwa akila chakula cha jioni pamoja na wanafunzi hao kila mwezi. Alisema pia, mmoja wa wanafunzi hao ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuwazawadia walipopata mtoto wao wa kwanza.
Mark Zuckerberg na Chan wana watoto wawili Maxima na August. Pamoja na hayo, Mark Zuckerberg na mkewe wamepanga kuanzisha mradi mkubwa wa kusaidia huduma za kimatibabu za watoto ujulikanao kama “Chan Zuckerberg Science” wenye thamani ya zaidi ya dola bilio tatu za kimarekani.
Harvard itabaki kuwa sehemu muhimu kwa Zuckerberg ambaye aliacha chuo mnamo mwaka 2004 akiwa mwaka wa mwisho wa masomo ili kuifanyia kazi Facebook kikamilifu.
Tangu wakati huo, mtandao huu wa kijamii umekuwa tovuti ya tatu inayotembelewa zaidi duniani. Sasa Facebook imeajiri watu zaidi ya 18,000 na inaripotiwa kuwa na watumiaji hai zaidi ya 1.28 bilioni kila siku, ambapo 86% wanaishi nje ya Marekani na Canada.
Neno la mwisho:
Ni dhahiri kuwa wakati mwingine watu sahihi hasa wenzi wa maisha ni muhimu zaidi kwetu kuliko pesa au vitu. Ni dhahiri kuwa mafanikio makubwa aliyoyapata Mark Zuckerberg yana uhusiano mkubwa na mchango na msaada anaoupata kutoka kwa mke wake Chan.
Soma pia: Dondoo 5 za Kuishi Ndoto Zako.
Je wewe umechagua na kupata mtu au watu sahihi? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.