Hakuna uandishi bora au andiko bora pasipo uhariri bora. Hivyo uandishi mzuri hauwezi kutengwa na uhariri bora. Ni dhahiri kuwa makala au andiko lililohaririwa vyema na kwa ustadi wa hali ya juu litakubalika na kupendwa na wasomaji wengi zaidi. Watu wengi wamekuwa wakitamani kuandika matini zilizohaririwa vyema lakini wamekuwa wakikwama juu ya ni njia gani wanaweza kuwa wahariri bora. Pengine umekuwa ukitamani kunufaika kupitia kazi ya uhariri lakini hujui ufanyeje ili uweze kuwa mhariri bora. Fuatana nami katika makala hii nikueleze njia 10 zitakazokufanya kuwa mhariri bora.
1. Jifunze sarufi ya lugha na kanuni za uandishi
Uhariri ni taaluma kama ilivyo kwa taaluma nyingine. Hivyo ili uwe mhariri bora basi huna budi kujifunza kanuni za sarufi ya lugha husika pamoja na kanuni za uandishi katika lugha. Hili litakuwezesha kufahamu mpangilio na matumizi ya maneno katika sentensi pamoja na utumizi wa alama mbalimbali za uandishi kama vile nukta, koma, kistari, mabano, nusu mkato n.k.
Mfano:
Kabla ya uhariri:
Juma na roza ni watoto wazuri wanapenda kusoma na kuchezaga pamoja
Baada ya uhariri:
Juma na Roza ni watoto wazuri, wanapenda kusoma na kuchezaga pamoja.
Katika mfano huu inaonyesha dhahiri nafasi ya sarufi ya lugha pamoja na alama za uandishi katika uhariri.
Soma pia: Mbinu 7 za Kuwa Mwandishi Bora.
2. Soma kwa sauti
Kuna tofauti kubwa kati ya kusoma kwa sauti na kusoma kimya. Unaposoma kwa sauti unaweza kubaini makosa ambayo macho yameshindwa kuyabaini. Jizoeze kusoma matini husika kwa sauti ili kuweza kubaini pia mtiririko wa mawazo na maneno usio sahihi. Unaweza kutumia mtu mwingine au programu za kopyuta kama vile Google Translate na Balabolka kufanya kazi hii. Utashangaa jinsi ambavyo utaweza kubaini makosa ambayo hukuweza kuyabaini kwa macho.
3. Acha andiko kwa muda
Unaposoma andiko au matini muda mrefu huifanya matini husika ikae kichwani; hivyo kukufanya kuwa vigumu kubaini dosari. Kadri unavyoacha matini au andiko kwa muda, ndivyo unavyotoa nafasi ya andiko kuwa jipya zaidi kwenye ubongo wako. Hivyo inashauriwa kuliacha andiko baada ya muda na kulihariri tena ili uweze kubaini makosa ambayo hukuyabaini awali.
4. Punguza zaidi kuliko kuongeza
Mara nyingi waandishi wana maneno mengi, lakini si yote yanafaa katika matini husika. Hivyo, mara uhariripo matini jizoeze kupunguza zaidi kuliko kuongeza ili kuhakikisha mawazo yanaeleweka kwa urahisi. Epuka maneno ya kuzunguka na kujaza nafasi.
Mfano.
Kabla ya uhariri:
Yule babu yangu mzee aliyekuja jana jioni ni babu yangu wa karibu sana kuliko babu zangu wengine wote.
Baada ya uhariri:
Babu aliyekuja jana jioni ni wa karibu kwangu kuliko wote.
Au
Babu aliyekuja jana jioni ni wa karibu kwangu kuliko babu zangu wote.
Ni dhahiri kuwa, mfano huu umekuonyesha maana halisi ya kuondoa zaidi kuliko kuongeza katika uhariri.
5. Jifunze kutoka kwa wahariri mashuhuri
Kama ilivyo kwa taaluma nyingine ambazo watu hujifunza kwa magwiji, basi ndivyo ilivyo pia katika uhariri. Tafuta wahariri mashuhuri unaowapenda kisha fuatilia mtindo na mbinu wanazozitumia katika kufanya kazi ya uhariri. Kwa kufanya hivi, utajifunza namna unavyoweza kukabili mazingira na changamoto mbalimbali za kiuhariri; hivyo kuwa mhariri bora zaidi.
6. Tambua matini(andiko) husika
Kila matini ina utofauti wake wa kimuundo na mtindo. Hivyo kuielewa matini ni hatua ya kwanza na muhimu ili kuweza kuihariri vyema. Kwa mfano mtindo na muundo wa matini za kidini ni tofauti kabisa na matini za burudani au za fasihi. Hivyo basi, kumbuka kutambua matini husika kutakuwezesha kuchagua njia na mtindo utakaotumika katika kuihariri.
7. Hariri matini mbalimbali
Uzoefu hutokana na mtu kukifanya kitu mara kwa mara ndani ya kipindi fulani cha muda. Hivyo kuhariri matini mbalimbali kutakupa uzoefu juu ya matini mbalimbali na kukufanya kuwa mhariri bora.
8. Kagua zaidi  ya mara moja
Binadamu hawezi kufanya kazi bila makosa. Hivyo ni muhimu ukajizoesha kurudia kukagua matini yako zaidi ya mara moja ili kuweza kubaini makosa uliyoyasahanu.
9. Mfahamu mwandishi
Ikiwa unahariri matini ya mtu mwingine, kumfahamu mwandishi ni hatua muhimu katika uhariri kwani kutakuwezesha kuhariri matini kwa urahisi zaidi. Usipomfahamu mwandishi ana msimamo na mtazamo gani pia anapendelea muundo upi unaweza ukafanya kazi ambayo haitakubaliwa na mwandishi. Ni vyema ukamuuliza mwandishi maswali pale ambapo umeona kuna jambo ambalo linakutatiza katika kazi yake.
10. Pokea maoni
Wahariri wengi wanapenda kusikilizwa zaidi kuliko kusikiliza. Ni vyema ukajifunza kupokea maoni kutoka kwa watu wengine kwani yatakuwezesha kuboresha zaidi shuguli yako ya uhariri. Kumbuka, wanaokupima pia ni watu wengine na siyo wewe mwenyewe. Hivyo kwa kusikiliza maoni ya watu wengine wakiwemo wasomaji na waandishi utaweza kuboresha utendaji kazi wako.
Hitimisho
Ni dhahiri kuwa uhariri ni taaluma rasimi na kamili. Hivyo inahitaji maarifa na maandalizi stahiki ili uweze kuimudu vyema. Hakikisha unajifunza mambo na kanuni mbalimbali zihusuzo uhariri, pia usisahau kufanya mazoezi ya kutosha ili uweze kujinoa zaidi.
Naamini sasa utaweza kuwa mhariri aliyebobea. Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie hapo chini kisha washirikishe wengine.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
dhima ya uhariri ni ipi
Asante ndugu Christopher kwa swali lako; tafadhali tutajitahidi kukujilisha hivi karibuni; endelea kutufuatilia; asante.
Yes
Asante; karibu sana Fahamuhili.com
Inapendeza sana
Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Katika taaluma ya uhariri ni mtu yeyote anaweza kuifanya au mbaka usomee? Nakama kusomea ni masomo yapi yanayokuongoza ili uweze kuhariri?
Tafadhali zingatia zaidi mbinu tajwa kwenye makala husika; hata hivyo unaweza kusoma sarufi ya lugha husika unayotaka kuitumia kwa uhariri.
Uhariri ni taaluma inayosomewa darasani. Ili uimudu lazima uipende lugha ya Kiswahili na kuisoma katika viwango mbalimbali.
Kuna uhusiano upi kati ya mhariri na wafanyikazi wengine katika shirika la uchapishaji
Mhariri hupima ubora wa kazi ya mwandishi ili kuona kama inakidhi viwango vya uchapishaji na kuhakikisha kuwa inawafaa wasomaji; hivyo wafanyakazi wegine hawawezi kuchapisha kazi dhaifu bila kupata tathimini ya mhariri. asante.
Asante lakini sifa za mhariri n zipi na sheria kuhusu haki za kunakili ni gani?
Asante kwa swali lako tutaandaa makala juu ya hilo. Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
sifa za mhariri bora/mzuri au mhariri duni rejelea swali lako n
tofauti kati ya uhariri na usarifu matini
swali la pili ni jadili madhara yanayoweza kutokana na uhariri mbaya katika vitabu vya shuleni na magazetini na katika habari za vyombo vya habari
Join
Sifa za mhariri bora
Tutaandika makala kuhusu sifa za mhariri bora. Asante sana kwa maoni yako ya thamani; na kwa kuwa msomaji wetu. Karibu sana Fahamuhili.com
Kwa kutumia mifano eleza nafasi ya uhariri katika kuboresha usomekaji wa andiko
Zipi ni alama anazozitumia mhariri katika uhariri?