Mbinu 7 za Kuwa Mwandishi Bora - Fahamu Hili
Tuesday, October 3Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mbinu 7 za Kuwa Mwandishi Bora

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Mwandishi

Kama umewahi kuwa na ndoto au matamanio ya kuwa mwandishi mkubwa kama vile Wole Soyinka, Ngũgĩ wa Thiong’o au pengine hata kuwa mwandishi bora kitaaluma au katika blogu yako, basi ni vyema ukajifunza namna ya kuwa mwandishi bora.

Kuwa mwandishi bora si jambo la mzaha; ni jambo linalalowezekana ikiwa utaweka jitihada stahiki.

Ni dhahiri kuwa jitihada utakazozifanya hazitakuwa bure kwani hivi leo kuna fursa mabalimbali zinazohitaji watu wenye uwezo mzuri wa uandishi.

Hivyo basi, fuatana nami nikujuze mbinu zitakazokuwezesha kuwa mwandishi bora kabisa na kufikia malengo yako ya mbeleni.

1. Soma maandiko bora

Ni dhahiri kuwa ukihitaji kufahamu nini mana ya uandishi bora ni lazima usome maandiko bora yaliyoandikwa na waandishi mahiri. Soma maandiko bora kadri uwezavyo kwani utajifunza mambo mbalimbali yakiwemo mpangilio wa hoja, uwasilishaji, matumizi ya lugha n.k. Kama una tatizo la kifedha unaweza kusoma maandiko mbalimbali yanayopatikana kwenye mtandao kwa gharama nafuu kabisa kuliko kununua vitabu au machapisho mengine.

2. Jifunze kanuni bora za uandishi

Uandishi una kanuni zake kama ilivyo kwa taaluma nyingine. Unatakiwa kufahamu maswala kama vile matumizi ya lugha, alama za uandishi, upangaji wa hoja, mbinu za uhariri n.k. Kwa kufanya hivi utaweza kuboresha uandishi wako na kuufanya kuwa wa kiwango cha juu kabisa.

3. Andika sana

Mazoezi hukufanya kuwa mahiri – practice makes perfect. Kadri unavyoandika kwa wingi ndivyo unavyojenga uzoefu wako zaidi. Uzoefu hupatikana kwa kufanya jambo fulani kwa muda mrefu. Hivyo jitahidi kuandika maandiko/matini mengi kadri uwezavyo ili uweze kunoa uwezo wako wa uandishi. Kupitia mbinu hii utaweza kubaini changamoto mbalimbali za kiuandishi na njia ya kuzitatua.

4. Tenga muda bora wa kuandika

Siyo wakati wote unafaa kwa ajili ya shughuli za uandishi. Ni vyema ukajitengea muda ambao uko vyema kiafya na kiakili. Mara nyingi asubuhi ndipo mtu anapokuwa na nguvu za kimwili na kiakili kufanya kazi mbalimbali. Hivyo ni vyema ukabainisha muda ambao wewe mwenyewe unaona ni bora kwako kufanya shughuli za uandishi bila matatizo.

5. Ondoa vitu vinavyokuvuruga

Maisha yetu yamejaa vitu mbalimbali. Vingine hutawala sehemu kubwa ya maisha yetu kiasi cha kutaka kuingilia au kuvuruga kila tunachokifanya. Ili kuwa na ufanisi katika uandishi ni vyema ukaodoa vitu mbalimbali vinavyoweza kukuvuruga kama vile mitandao ya kijamii, simu, televisheni, michezo ya kielektroniki, watu n.k. Unaweza kuzima simu au data katika vifaa vyako ili kuzuia kuvurugwa na mambo ya mtandao. Unaweza kutafuta chumba au eneo maalumu lenye utulivu litakalokuruhusu kufanya kazi yako ya uandishi kwa utulivu. Kwa mfano ninapoandika makala hii nimekaa katika chumba cha kusomea ili kuhakikisha ninapata utulivu wa kutosha.

6. Orodhesha mawazo

Ni jambo zuri ukajizoesha kuorodhesha mawazo kabla ya kuanza kuandika. Kwa kufanya hivi utakuwa umejiwekea mwongozo mdogo utakao kuongoza juu ya yale unayoyandikia. Unaweza kutumia kipande cha karatasi, shajara, au hata programu za kompyuta kama vile MS Word na Google Docs ili kuorodhesha mawazo yako.

7. Andika tu bila kuacha

Ni vigumu kujikita katika uandishi bila kuacha kama hujajiwekea lengo na kuwa na mtindo anuwai wa uandishi. Ni dhahiri utazamapo karatasi nyeupe au ukurasa mweupe kwenye kompyuta unaweza ukasita au ukakata tamaa ya kuandika mapema. Hivyo, unaweza kufanya haya yafuatayao ili kuweza kuandika bila kuacha.

  • Andika tu mawazo kadri yanavyokuja akilini mwako kwani utayahariri baadaye.
  • Usifanye mambo mengi kwa wakati mmoja; yaani jikite tu kwenye kuandika bila kujihusisha na mambo mengine.
  • Usihariri; unapohariri wakati unaandika utapunguza ufanisi katika uandishi wako. Andika kwanza na utahariri baadaye.

Ukitumia mbinu hii utaweza kuandika mambo mengi kwa muda mfupi kwa urahisi zaidi bila kuacha au kukata tamaa.

Hitimisho

Zilizoelezwa hapa ni mbinu ambazo zitakuwezesha kuwa mwandishi bora. Mbinu hizi zinatumiwa na mwandishi kuandika makala kadha wa kadha katika blogu mbalimbali na zimempa ufanisi mkubwa. Hivyo unaweza kufanya maamuzi magumu ya kubadilika na kuwekeza katika kuboresha uwezo wako wa uandishi. Naamini hutojutia maamuzi utakayoyafanya kwani utakuwa na tija kubwa sana.

Soma pia: Njia 10 za Kuwa Mhariri Bora.

Naamini makala hii imekuwa na manufaa kwako? Je una swali au ungehitaji usaidizi wowote? Tafadhali tuandike hapo chini; pia washirikishe wengine.

4 10 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

8 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
EDWIN JAMBO
EDWIN JAMBO
4 years ago

Nawezaje kupata mafunzo zaidi ili niweze kujisimamia kuandika kitabu changu

binhishma
binhishma
3 years ago

Endeleeni na utaratibu wa kuelimisha uwandish wa makala

binhishma
binhishma
3 years ago

Je makala hayana ida ya maneno

Mkuu
Mkuu
3 years ago

Napenda matini haya, yamenipa motisha katika sekta hii ya uandishi. Shukran za dhati.

8
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x