Madhara 6 ya Kutazama Televisheni (TV) Unayopaswa Kuyafahamu - Fahamu Hili
Friday, May 24Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Madhara 6 ya Kutazama Televisheni (TV) Unayopaswa Kuyafahamu

Washirikishe Wengine Makala Hii:
televisheni
Watu wakitazama Televisheni: Chanzo cha picha: http://pazarlama30.com

Miaka ya nyuma televisheni ilikuwa ni kitu adimu sana. Lakini hivi leo takriban kila familia au mtu ana televisheni nyumbani kwake; inaweza kuwa sebuleni, chumbani au hata kwenye simu yake ya kisasa.

Hata wale wasiokuwa na televisheni nyumbani kwao bado wanapata nafasi ya kutazama televisheni kwenye migahawa, mabasi au hata kwenye ofisi za kampuni au taasisi mbalimbali.

Televisheni imekuwa ni kifaa muhimu kwa ajili ya habari na burudani; hata hivyo televisheni inaweza kuwa na madhara kadha wa kadha kwako ikiwa haitotawaliwa vyema. Basi karibu ufahamu madhara ya kutazama televisheni (TV)

1. Hupoteza muda

Unapokaa na kuangalia televisheni ni wazi kuwa unatumia muda mwingi na wa muhimu sana. Hii ni kutokana na sababu kuwa watu wengi hutazama televisheni kwa muda mrefu au hata siku nzima.

Utazamaji wa televisheni wa muda mrefu unaweza kukupotezea muda mwingi ambao ungeweza kuutumia kufanya kazi nyingine hasa zile zinazokuongezea kipato na maarifa.

Soma pia: Kanuni 9 za Kufanikiwa katika Matumizi ya Muda

2. Hukuondolea mahusiano na watu

Unapokaa muda mrefu kwenye televisheni ni wazi kuwa utajitenga na watu wengi. Hutopata muda wa kushirikishana hili au lile na watu wengine wala kuwasaidia wale wanaohitaji msaada wako.

Kukaa karibu na watu wengine kwenye jamii hukufundisha mambo mbalimbali pamoja na kuboresha mahusiano yako ya kijamii. Hili ni tofauti na kukaa mbele ya televisheni siku nzima ukitazama filamu au mziki.

3. Hupoteza pesa

Chaneli bora za televisheni zinapatikana kwa gharama kubwa; ikizingatiwa pia televisheni huhitaji umeme ili iweze kujiendesha, hili pia litaendelea kukugharimu fedha.

Ikiwa wewe unapenda kutazama televisheni sana, utatumia fedha nyingi kwa ajili ya kukidhi kile unachokipenda. Hata hivyo, ungeweza kuzitumia pesa hizi kwa kuwekeza, kuweka akiba au kufanya kitu kingine chenye tija zaidi kwako.

Soma pia: Njia 10 Zitakazokuwezesha Kutumia Pesa Vyema

4. Taarifa za uongo

Siyo taarifa zote au vitu vyote vinavyoonekana kwenye televisheni ni vya kweli. Hivyo kutazama na kuiamini sana televisheni kunaweza kukusababishia kupata taarifa za uwongo.

Watu wengi unaowaona kwenye televisheni huishi maisha ya mbele ya kamera; yaani maisha ambayo siyo halisi; hivyo pia kuiga maisha haya kunaweza pia kukupoteza.

5. Huathiri afya

Binadamu hatakiwi akae kwa muda mrefu sana; hivyo kwa wale wanaokaa kwenye televisheni muda mrefu sana au hata siku nzima, hawazitendei haki afya zao.

Ni muhimu kufanya kazi za kuuchangamsha mwili au kufanya mazoezi mara kwa mara ili kulinda afya yako kuliko kukaa tu mbele ya televisheni.

Ikumbukwe pia tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa televisheni ni chanzo kikubwa cha ongezeko la unene kwa watu wengi duniani.

6. Huaribu usingizi

Watu wengi hukosa usingizi kwa sababu ya kukesha wakitazama televisheni. Usingizi wa kutosha ni swala muhimu sana kwa ajili ya afya ya mwili na akili yako. Usingizi bora utakuongezea pia ufanisi katika yale unayoyafanya.

Ni muhimu kuzingatia kulala kwa saa 6 hadi 8 ili kuweka afya yako katika hali nzuri.

Soma pia: Njia 13 za Kupata Usingizi Mzuri/Kulala Vizuri

Hitimisho

Katika makala hii sikuwa na lengo la kukuambia kuwa televisheni (TV) ni mbaya au haina manufaa kwako, bali nilitaka nikupe mtazamo mpana zaidi. Ni wazi kuwa televisheni ina manufaa mengi sana lakini pia ina madhara mengi ikiwa haitatawaliwa vyema. Hivyo ni muhimu sana kuwa na kiasi na utawala wa kutosha katika matumizi yako ya televisheni.

Je una maoni au swali? Tafadhali andika maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii.

4 3 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Msengiselemani
Msengiselemani
3 years ago

Somo zuri

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x