Mambo 7 ya Kuzingatia ili Kuhifadhi Nyaraka Muhimu Salama - Fahamu Hili
Thursday, April 25Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 7 ya Kuzingatia ili Kuhifadhi Nyaraka Muhimu Salama

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Nyaraka muhimu

Katika maisha yetu ya kila siku hatuwezi kuepuka kuwa na nyaraka mbalimbali. Baadhi ya nyaraka ni za muhimu sana kwetu kiasi cha kutoweza kuzipata tena iwapo zitaharibika au kupotea.

Ni ukweli usiopingika kuwa nyaraka kama vile vyeti ya taaluma, bima, hati za kusafiria, leseni, wosia, vyeti vya ndoa, talaka, mikataba, hati za nyumba na viwanja ni baadhi ya nyaraka zinazotakiwa kutunzwa sana.

Kutokana na watu wengi kutofahamu umuhimu wa nyaraka mbalimbali au kutokuzihifadhi vyema, wengi wamejikuta kwenye matatizo makubwa baada ya nyaraka zao muhimu kuharibika au kupotea.

Ikiwa basi unataka kuweka nyaraka zako salama, karibu nikushirikishe mambo 7 ya kuzingatia ili kuhifadhi nyaraka muhimu salama.

1. Tumia kabati au sanduku maalumu ya kuhifadhi nyaraka

Safe
Kabati maalumu la kuhifadhia fedha na nyaraka muhimu.

Zipo kabati na masanduku maalumu yaliyotengenezwa kwa mfumo ambao unalinda vilivyomo ndani dhidi ya maji, moto, wadudu, au hata wezi.

Ili kuepuka kuibiwa au kuharibika kwa nyaraka zako muhimu, ni vyema ukanunua na kutumia masanduku haya maalumu ya kuhifadhia nyaraka.

2. Weka nyaraka muhimu mahali pamoja

Watu wengi hupoteza nyaraka zao muhimu kwa sababu hawaziweki mahali pamoja peke yake; wengi huzichanganya na vitu vingine visivyo na thamani.

Kuweka nyaraka mahali pamoja peke yake kunakuepushia hatari ya kusahau zilipo au kuzipoteza ndani ya makaratasi au vitu vingine visivyokuwa na thamani.

Kwa mfano mtu anaweka nyaraka muhimu ndani ya gazeti, ni wazi kuwa gazeti hilo linaweza kuchomwa au kuraruliwa na ukapoteza nyaraka zako.

3. Rudisha nyaraka mahali pake mara umalizapo kuzitumia

Kutokurudisha nyaraka mahali pake kumewasababishia watu wengi kupoteza nyaraka zao. Watu huchukua nyaraka mara zinapohitajika lakini husahau kuzirejesha kwa wakati na mahali sahihi walipozichukua.

Ili kuhakikisha usalama wa nyaraka zako, usiziache kwenye begi, juu ya kabati au meza mara umalizapo kuzitumia. Hakikisha unazirudisha mahali salama unapozihifadhi.

4. Tumia hazina za kwenye mtandao

Teknolojia imerahisisha na kuboresha maisha. Hakuna haja ya kubeba vyeti au nyaraka muhimu kila mahali. Unaweza kuscan na kuweka nyaraka zako kwenye hazina za data za kwenye mtandao na ukazipata popote pale mara unapozihitaji.

Unaweza kutumia hazina ya barua pepe au hazina nyingine kama vile Google Drive: 15GB bure, Box: 10GB bure, OneDrive: 5GB bure (1TB Kwa wanafunzi), iCloud: 5GB bure ili kuhifadhi nakala za nyaraka zako muhimu.

5. Tumia taasisi za kuhifadhi nyaraka

Kuna taasisi na kampuni mbalimbali ambazo hutoa huduma za kuhifadhi nyaraka muhimu. Taasisi hasa zile za kifedha, yaani benki, nyingi hutoa huduma ya kuhifadhi nyaraka muhimu kwa gharama nafuu.

Unaweza kuuliza kwenye benki yako au ile iliyo karibu nawe ili kufahamu kama wanatoa huduma hii ili uhifadhi nyaraka zako dhidi ya wezi au majanga kama vile moto na mafuriko.

6. Kuwa na nakala za nyaraka zako

Ili kulinda na kuhifadhi nyaraka zako katika hali ya usalama, ni vyema kuhakikisha unakuwa na nakala za nyaraka zako muhimu.

Hili litakusaidia sana kwani hutobeba nyaraka halisi kila mahali, pia nyaraka halisi zikipotea bado utakuwa na nakala za nyaraka zako muhimu.

7. Usimwachie mtu nyaraka zako

Kuna watu wanawaamini watu wengine kiasi cha kuthubutu kuwaachia nyaraka zao muhimu. Kumbuka mtu mwingine anaweza kupoteza au hata kuharibu nyaraka zako muhimu.

Nimeshuhudia pia baadhi ya taasisi au kampuni zikitaka kushikilia nyaraka muhimu za mwajiriwa kama vile vyeti vya taaluma ili asiache kazi kabla ya mkataba kwisha.

Ni muhimu Kuwa makini na taasisi au kampuni hizi kwani lolote linaweza kutokea na ukapoteza nyaraka zako.

Neno la mwisho

Ni wazi kuwa mara nyingi umuhimu wa kitu haufahamiki hadi pale mtu anapokikosa kitu hicho. Kupoteza nyaraka muhimu ni jambo baya lenye usumbufu na changamoto nyingi.

Hivyo ni vyema ukahakikisha unazingatia mambo yaliyoelezwa kwenye makala hii ili kuhakikisha usalama wa nyaraka zako muhimu.

Je una swali au maoni yoyote? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii. Unaweza kulike ukurasa wetu wa Facebook ili kufahamu mengi zaidi.

0 0 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

2 Maoni
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Said Haroun Singano
Said Haroun Singano
5 years ago

Asante nashukuru sana kwa somo zuri la mambo ambayo nilikuwa siyajui. Mungu akubariki ndugu yangu

2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x