Wakati mwingine tunatazama tu mambo ambayo hatuna kwenye maisha, kuliko yale tuliyo nayo. Mara nyingi huwa hatutambui umuhimu wa kitu hadi pale tunapokikosa. Niwazi kuwa wapo watu wanaotafuta vile tunavyoviona ni vidogo lakini hawavipati.
Ni muhimu kutenga muda wa kukumbuka yale mambo yote ambayo tunapaswa kushukuru kwa ajili yake. Kama una chochote kati ya hivi basi yakupasa kushukuru.
- Afya njema
Mara nyingi hatutambui kuwa na afya njema pekee ni jambo muhimu na kubwa sana. Kuna wengi wanaotamani kuwa na afya kama ya kwako lakini hawana; hivyo yakupasa kushukuru kwa afya njema. - Pesa ulizonazo
Unaweza kufikiri kiasi cha pesa ulizonazo ni kidogo sana hivyo hauhitaji kushukuru. Kuna mahali pengine wewe ni tajiri mkubwa sana. Wapo wasiokuwa na pesa wala chochote kile wanachoweza kukigeuza kuwa pesa. - Marafiki wema
Marafiki ni muhimu sana kwenye maisha, hasa marafiki wema. Kama una marafiki wanaokutia moyo, kukufariji, kushauri na hata kukusaidia kwa njia moja au nyingine ni jambo la kushukuru. - Wazazi
Wapo ambao hawakufanikiwa hata kuwafahamu wazazi wao. Lakini kama una nafasi angalau ya kuwa na mzazi hata mmoja ni neema kubwa ambayo yakupasa kushukuru kila wakati. - Kuamka leo
Je unafahamu kuna wengine walilala lakini hawakuamka? Ni lazima kushukuru kwa kupewa neema ya kuamka tena leo ukiwa mzima. Siyo kwamba wewe unayeishi ni mwema au bora sana bali, ni neema tu. - Makazi na malazi
Una mahali ambapo unapaita nyumbani? Kama jibu ni Ndiyo, basi una sababu ya kushukuru. Wengine wanahangaika huko na huko bila utulilivu wala mahali ambapo wanaweza kupaita nyumbani. Hawana pa kulala wa pakupumzika. - Mwenzi wa maisha
Inawezekana uko na mwenzi wako kwenye ndoa lakini unaona ni jambo la kawaida sana; lakini ukumbuke kuwa wapo wengi wanaotamani nafasi hiyo hawaipati. Hivyo ni vyema ukawa na shukurani hata kwa jambo hilo. - Fursa ya kupata elimu
Sio wote wenye fursa ya kupata elimu. Wengi hukosa fedha au mahitaji muhimu ili kupata hata elimu ya msingi pekee. Hivyo kama umepata elimu kwa kiwango fulani ni jambo la kushukuru pia. - Ulinzi na usalama
Dunia leo imejaa machafuko ya uhalifu, ugaidi na hata vita. Ikiwa wewe upo kwenye eneo lenye amani na utulivu basi ni jambo la kushukuru. - Maji safi
Takwimu zinaonyesha kuwa ni watu wachache sana ndiyo wenye fursa ya kupata maji safi duniani. Ikiwa wewe una nafasi ya kupata maji safi kwa ajili ya matumizi yako basi ni jambo la kushukuru - Uwezo wa kuona
Unaweza kutazama mazingira, watu, wanyama na mambo mengine bila shida? Kama jibu ni ndiyo, basi yakupasa kushukuru kwa hilo pia. - Usafiri binafsi
Kama una baiskeli, pikipiki au gari basi inakupasa kushukuru kwani wapo wengi wanaopambana usiku na mchana kuvipata lakini bado hawajafanikiwa. - Uhuru wa kujieleza
Kuna nchi na maeneo ambayo uhuru wa watu wa kujieleza umebanwa sana. Hivyo ukiwa na uhuru wa kuongea na kujieleza basi yakupasa kushukuru kwa hilo. - Uhuru wa kuabudu
Je unaweza kuabudu mahali upatakapo au kwa namna unayopenda bila shida? Hili ni jambo ambalo watu wengi wanalikosa. Wengi hulazimishwa kuabudu sehemu fulani au huzuiwa kuabudu kabisa. Ikiwa una uhuru wa kuabudu basi yakupasa kushukuru. - Uwezo wa kusikia
Wapo watu wanaotamani kusikia nyimbo nzuri au sauti nzuri za ndege na wanyama lakini hawawezi. Hivyo ni vyema ukashukuru ikiwa wewe una uwezo wa kusikia vyema. - Watoto
Watoto ni baraka na zawadi kubwa. Wengi huwaona kama watu wasiofa lakini kwa wengine ni lulu. Mara nyingi watu hawatambui thamani ya watoto hadi pale wanapowakosa. Ni muhimu kushukuru kwa zawadi hii kubwa.
Soma pia: Mambo 10 ya Kujifunza Kutoka Kwenye Maisha ya Watoto. - Mawasiliano
Una simu, kompyuta, tablate n.k vinavyokuwezesha kuwasiliana au eneo ulilopo lina mawasiliao mazuri? Kama una vitu hivi ni muhimu kushukuru kwani dunia ama ulimwengu usiokuwa na mawasiliano ni mgumu sana. - Changamoto
Changamoto? Ndiyo, changamoto ni jambo la kushukuru kwa ajili yake kwa kuwa zinakupa hamasa ya kuendelea mbele ili uwe bora zaidi. Kusingekuwa na changamoto watu wasingefanya jitihada zozote kuboresha maisha yao. - Mavazi
Umeshafikiri kuwa fasheni au mitindo katika mavazi siyo lazima? Jambo la msingi ni kufunika mwili wako dhidi ya jua, mvua, wadudu pamoja na kutunza staha yako tu. Ikiwa una mavazi kwa ajili ya kujisitiri ni jambo kubwa sana linalo kupasa kushukuru. - Uhuru wa kupiga kura
Kutokana na kiu na uchu wa madaraka, mifumo halali ya kupata viongozi imeingiliwa sana. Siyo kila mtu duniani ana uhuru wa kupiga kura kwa amani ili kumchagua kiongozi anayemtaka. Ikiwa wewe una nafasi hiyo, hata kama hauitumii ni jambo la kushukuru pia.
Neno la Mwisho
Naamini yapo mengi zaidi na zaidi yakushukuriwa. Ni vyema tukajifunza kushukuru ili tufungue milango ya kupata mengine mazuri zaidi. Kuacha kulalamika na kuona angalau yale mazuri mchache ni jambo la msingi.
Je wewe huwa unashukuru kwa haya? Je kuna jambo gani jingine muhimu la kushukuru? Tafadhali tuandikie maoni yako kisha washirikishe wengine makala hii.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.