Kufanya biashara kwenye mtandao ni jambo lenye faida na changamoto zake. Unaweza ukawa na bidhaa nzuri sana, lakini ukumbuke kuwa kila siku kunaanzishwa tovuti za kuuza bidhaa mtandaoni. Haijalishi kuwa wewe ni muuzaji wa bidhaa wa siku nyingi au wa karibuni, ni wazi kuwa utakutana na changamoto kadha wa kadha. Sasa utafanyaje?
Hakuna jibu rahisi, bali ni wazi kuwa makosa unayofanya wakati wa kuendesha biashara kwenye mtandao, ndiyo yanayokugharimu wewe na mapato yako. Yafuatayo ni makosa 8 ambayo unatakiwa kufanya juu chini ili kuhakikisha unayaepuka unapofanya biashara kwenye mtandao.
1. Kukosa kitengo cha huduma kwa wateja
Ni rahisi mtu kukaa dukani kwake siku nzima ili kuwahudumia wateja; lakini unaona hakuna umuhimu wa kukaa karibu na wateja wake wa kwenye mtandao. Kumbuka hawa ni wateja kama wateja wengine, wanaweza kuwa wana maswali, maombi au mapendekezo wanayotaka kuyafikisha kwako. Wateja watakufikia vipi na wewe hujaweka mfumo mzuri wa huduma kwa wateja? Je watanunua tu vitu kwa sababu unapenda wanunue? La hasha! Kutokana na kosa hili hutoweza kupata wateja na kufanikiwa katika biashara yako.
2. Tovuti iliyosanifiwa vibaya au duni
Katika jambo muhimu kwenye biashara ya kwenye mtandao ni tovuti iliyotengenezwa au kusanifiwa vizuri. Watu wengi hutengeneza tovuti mbaya ambazo siyo rafiki kwa wateja na vifaa vyao. Hili huwagharimu wengi kwa kupoteza wateja wengi. Zingatia mambo haya katika kutengeneza tovuti nzuri ya kufanyia biashara ya kwenye mtandao:
- Hakikisha inaweza kuonekana vyema kwenye vifaa vyote kama vile simu, tablet na kompyuta.
- Hakikisha ina mfumo mzuri wa viungo (Menu and Navigation) kwa njiaa hii mteja ataweza kuperuzi vyema kwenye tovuti yako.
- Hakikisha inasehemu ya utafutaji.
- Boresha tovuti kwa ajili ya injini pekuzi (Search Engine Optimization – SEO)
Ukizingatia mambo haya tovuti yako itakuwa nzuri kwa wateja na kukufanya kupata mauzo zaidi.
3. Ufafanuzi duni wa bidhaa
Hakuna mtu anayenunua kitu ambacho hajakifahamu vizuri au kukiona. Kosa la ufafanuzi au maelezo duni ya bidhaa limewafanya wateja wengi kutonunua bidhaa za wafanya biashara wengi. Hakikisha bidhaa ina picha nzuri na maelezo ya kutosha kumfanya mteja aielewe bidhaa yako ili awe tayari kuinunua.
Kwa mfano mtu unaweka picha ya bidhaa fulani kwenye tovuti au mtandao wa kijamii bila hata maelezo yoyote, je unafikiri kwa sababu umeiweka kama cover au profile picture ndiyo itanunuliwa? Ni lazima watu wapate maelezo ya kutosha na jinsi bidhaa husika itakavyowasaidia ndipo watainunua.

4. Kutokutumia au kujali mitandao ya kijamii
Wafanya biashara wengi hawajui umuhimu wa mitandao ya kijamii wala matumizi yake kwenye biashara zao. Biashara ya kwenye mtandao inahitaji ufahamu matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii ili kupata wateja wengi zaidi kwa ajili ya bidhaa zako.
Hakikisha unawajulisha watu jinsi bidhaa zako zitakavyotatua matatizo yao; pia usisahau kuwajulisha punguzo (offer), bei na njia ya kuzipata bidhaa zako.
5. Kutokufahamu wateja na soko lako
Kufahamu wateja na soko ni hatua mojawapo ya kukuwezesha kukuza mauzo ya bidhaa zako. Hebu fikiri unatangaza bidhaa za urembo za wanawake kwenye group la wa Whatsapp, je utapata wateja kweli? Naamini hutopata wateja jinsi ipasavyo. Ni wazi kuwa ni muhimu ujue soko lako liko wapi na ulilenge ipasaavyo.
6. Mfumo duni wa kulipia na kusafirisha bidhaa
Mara nyingi unapouza vitu kupitia mtandao wateja watalipia bidhaa zao moja kwa moja, pia watafahamu jisi watakavyopata bidhaa husika.
Wauzaji wengi hawaweki mfumo rahisi kwa wateja ili waweze kufanya malipo; kwamfano tovuti za Afrika Mashariki tunategemea kuona njia za malipo kama vile M-Pesa, Airtel Money, Tigo pesa, MTN n.k. Pia ni lazima kuwe na mfumo mzuri wa kuwasafirishia au kuwafikishia wateja bidhaa zao. Kwa kufanya hivi utaaminika zaidi na kujiongezea wateja
7. Kulenga zaidi kuuza bidhaa kuliko kutatua matatizo ya watu
Mara nyingi nimekuwa nikisisitiza kuwa pesa ni matokeo ya kutatua shida za watu. Pamoja na kulenga kuuza bidhaa zako na kupata pesa, ni lazima kwanza uhakikishe unatatua matatizo ya watu kupitia bidhaa zako kwanza.
Ni muhimu pia kujenga imani kwa wateja kwa kuwapa garantii na punguzo (offer) kwa ajili ya bidhaa zako. Kwa kufanya hivi utaongeza imani ya watu kwenye bidhaa na biashara yako.
8. Kutokujitangaza ipasavyo
Biashara ni matangazo. Jinsi matangazo yalivyo muhimu katika biashara za aina nyingine, ndivyo ilivyo pia kwenye biashara ya kwenye mtandao. Ni lazima utumie njia mbalimbali za kuzitangaza bidhaa zako, ukihusisha njia za bure na zile zakulipiwa. Kwa njiaa hii utawezakutambulika kati ya washindani wako, hivyo kufikia wateja wengi zaidi. Kamwe usifanye kosa la kuupuuzia matangazo kwenye biashara ya kwenye mtandao kwani kuna ushindani mkubwa.
Hitimisho
Naamini sasa umefahamu mambo ya kufanya ili uweze kuendesha biashara ya kwenye mtandao itakayokuwa na tija zaidi. Ni wazi kuwa ukiepuka makosa yaliyojadiliwa hapo juu utaweza kukuza biashara yako na kujipatia faida zaidi.
Je una swali au maoni yoyote kuhusiana na makala hii? Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini kisha usisahau kuwashirikisha wengine makala hii. Karibu ufuatilie pia ukurasa wetu wa Facebook.
Kornelio ni mjasiriamali, mfuasi mkubwa wa masuala ya kompyuta na msanifu mtandao toka mwaka 2008. Amekuwa akifanya kazi mbalimbali zinazohusiana na Teknolojia ya Habari Mawasiliano (TEHAMA), bila kusahau uandishi wa makala kadha wa kadha katika tovuti na blog mbalimbali. Anapenda kujifunza na kuwafundisha watu wengine mambo mbalimbali pamoja na mbinu za kuboresha maisha ya kila siku.
Naitwa Frank jeremia npo monduli.
Sina elim ya kutosha ya kimtandandao na napenda fanya biashara mtandaon.ntasaifikaje kwa hl
Tutaandaa makala kamili yenye muongozo wa kujibu swali lako. Asante sana kwa maoni yako ya thamani; karibu sana Fahamuhili.com
Je biashara nini naomba kufahamu
Tadhali ndugu Vicent fafanua swali lako.