Mambo 10 ya Kujifunza Kutoka Kwenye Maisha ya Watoto - Fahamu Hili
Thursday, April 18Maarifa Bila Kikomo
Shadow

Mambo 10 ya Kujifunza Kutoka Kwenye Maisha ya Watoto

Washirikishe Wengine Makala Hii:

Mtoto

Ingawa watu wengine huwachukulia watoto kama watu wasiofaa, watoto ni malaika wa kweli wanaoweza kutufundisha jinsi ya kuishi maisha mazuri. Ingawa wakati mwingine hawatambui wanachokuwa wakikifanya, lakini wanatupa nafasi ya kujifunza vitu vingi ambavyo tunavisahau tunapokuwa watu wazima.

Kuna sababu ya kwanini watoto wanaitwa zawadi kutoka kwa Mungu. Wanatufundisha kuboresha maisha yetu, kuona vitu vizuri kwenye maisha pamoja na kujaa tabasamu kila siku. Ni wazi kuwa yapo mambo mengi mazuri na yenye manufaa makubwa ambayo kila mtu anaweza kujifunza kutoka kwa watoto; yafahamu mambo hayo sasa.

1. Kuwa na furaha

Maisha ya watoto yamejaa furaha. Mara nyingi utawakuta watoto wakiimba, wakikimbia, wakiruka, wakitaniana kwa furaha bila wasiwasi. Hili limefanya maisha ya utoto kuwa sawa na kito cha thamani. Jambo hili ni tofauti na watu wazima, kwani wao huwaza na kuhangaikia mengi huku wakiwa hawana furaha. Hali hii hufanya maisha ya watu wengi kukosa ladha na tija. Ni muhimu kujifunza kuwa na furaha kama watoto ili uweze kuwa na tija zaidi.Watoto wana Furaha

2. Kusamehe na kuomba msamaha

“… nisamehe nimekosa sitarudia tena” ni kauli rahisi sana kuisikia kutoka kwa watoto. Watoto hawapendi kukaa bila kusamehewa kwani hawana nafasi ya kubeba maumivu na uchungu mioyoni mwao. Mara nyingi hata watoto wanapokoseana husameheana kirahisi kabisa bila hata kuomba msamaha. Jambo hili limeyafanya maisha ya watoto kuwa na furaha na upendo wakati wote. Ni muhimu kujifunza kusamehe na kuomba msamaha pale tunapokoseana na mtu mwingine.

Soma pia: Sababu 9 za Kwanini Umsamehe Aliyekukosea.

3. Upendo wa kipekee

Upendo ulioko kwa watoto ni wakushangaza. Mtoto atamjali mwenzake kama yeye mwenyewe. Mtoto anapopata zawadi au kitu fulani, ni wazi atatamani kugawana au kukitumia na marafiki zake. Hali ni tofauti kwenye maisha ya watu wazima kwani maisha yao yamejaa ubinafsi, choyo na chuki zisizokuwa na sababu. Jifunze kuwa na upendo kama wa mtoto; upendo siyo vitu bali ni moyo uliyo tayari.Watoto marafiki

4. Kuheshimu hisia zako

Mtoto akiwa na hasira ataonyesha, akitaka kulia atalia, akiwa na furaha pia ataonyesha. Halii hi ni kinyume kwa watu wazima kwani wao wanaweza kuwa wanacheka lakini moyoni wanalia; au wanalia kumbe moyoni wanacheka. Ni vyema ukafahamu umuhimu wa kuheshimu hisia zako; usibebe uchungu ndani ya moyo wako. Kama unahuzuni basi itoe, kama unafuraha pia ionyeshe furaha yako.

5. Ni sawa kuomba msaada

Ni wazi kuwa watoto ni watu ambao hawaoni aibu au shida kuomba msaada pale wanapokuwa na tatizo. Mtoto akikosa pesa, chakula, nguo, vifaa vya shule n.k ni rahisi kuomba vitu hivyo kuliko mtu mzima anapopata shida. Je unafikiri watu wataota au kufunuliwa mahitaji yako ili wakusaidie? Jifunze kusema pale unapohitaji msaada. Jambo la kuzingatia tu hapa ni kuhakikisha unamwambia mtu sahihi.

6. Kuzungumza ukweli

Katika mambo ambayo huwa yananipa raha kuhusu watoto, ni tabia yao ya kupenda kusema ukweli. Watoto ni kama malaika wasiopenda giza; wao hawaoni maana yoyote ya kusema uwongo. Ni wazi kuwa hii ndiyo sababu hata vyombo vingi vya kisheria hupendelea ushahidi wa watoto. Mtoto akiiba atasema ameiba; akimwona mwizi pia atamtaja. Ni vyema ukajifunza kusema kweli kwenye maisha yako kwani uongo hauna maana na unaweza kukuumbua wakati wowote.

7. Kujiamini

Mara nyingi watoto wanajiamini sana. Hufanya vitu hadi pale wanaposhindwa. Hata kama jambo ni jipya, mtoto atataka kulijaribu. Kwa mfano ukiwa na gari na ukamuuliza mtoto kama anaweza kuliendesha atakujibu ndiyo. Ni wazi kuwa ni muhimu kujiamini; tusishindwe kabla ya kujaribu.Watoto Wakicheza

8. Kuwa na ndoto kubwa

Ninapenda sana kusikiliza mawazo na ndoto za watoto. Mara huyu anataka kuwa rubani, huyu raisi, huyu daktari n.k. Ni ukweli usiopingika kuwa kadri unavyowaza mawazo makubwa ndivyo unavyoongeza nafasi yako ya kuwa na mafanikio makubwa. Jiulize kama mtoto hana msingi wowote lakini anawaza ndoto kubwa kwanini wewe mtu mzima uwaze ndoto ndogo?

9. Haufahamu kila kitu

Kama nilivyoeleza juu ya mtoto kuwa mkweli, pia mtoto yuko tayari kujifunza na kusema hafahamu. Kama kweli mtoto hakifahamu kitu, yupo tayari kusema hakifahamu. Ni vyema watu wazima kujifunza kuwa hawajui kila kitu kuliko kutarazia mambo kwa kujifanya wajuaji na mwishoni wakaharibu.

10. Udhubutu wa kujaribu

Udhubutu ni jambo muhimu katika kufanikiwa kwenye kazi yoyote. Watoto ni mfano bora wa udhubutu kwani wao hufanya mambo mengine bila hata kujali kama ni salama kwao ama wanayaweza au laa. Kwa mfano mtoto anaweza kuchukua baiskeli au hata pikipiki na kujaribu kuiendesha bila hata kujali kama anaweza au laa. Ni muhimu kudhubutu kufanya mambo ambayo haujayafanya kwani huwezi kujua kama ndipo kufanikiwa kwako kulikofichwa.

Neno la Mwisho:

Hakuna ubishi sasa, kuwa watoto ni malaika wanaotufundisha somo kubwa. Maisha ya watoto yamejaa furaha na amani kwa kuwa wao wanafanya mambo ambayo kwa namna nyingine watu wazima huyapuuzia. Ni heri kujitahidi kuwa na moyo kama wa mtoto ili uwe na maisha yenye amani, furaha na tija zaidi.

Naamini umejifunza mengi katika makala hii, tafadhali tupe maoni yako hapo chini kisha usisahau kuwashirikisha wengine.

5 2 votes
Pendekeza Ubora wa Makala Hii
Washirikishe Wengine Makala Hii:
Subscribe
Notify of
guest

0 Maoni
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x